Ramovic ataka kuzoa makombe yote Bongo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:10 AM Jan 29 2025
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic
Picha: Mtandao
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic

WAKATI makocha wa timu zingine wakifikiria kutwaa ubingwa msimu huu, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, ameibuka na kusema anataka kuweka rekodi ya kuzoa makombe yote ya hapa nchini kwa mara ya kwanza kwenye historia yake ya soka.

Kocha huyo ameyasema hayo siku chache kabla ya kuelekea kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa, Jumamosi kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, dhidi ya Kagera Sugar.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ramovic, alisema baada ya kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi chake kitakuwa na muda wa kujiandaa kwa ajili ya michezo ya ndani ambayo hataki kuacha kombe hata moja.

Alisema Yanga ndiyo inayoshikilia makombe yote ya ndani, hivyo atahakikisha yanabaki, huku yeye mwenyewe akitaka kuweka rekodi ya kuyachukua kwa mara ya kwanza akiifundisha timu hiyo kongwe nchini.

"Tunataka kushinda kila kitu, tunataka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA, tumeshatolewa kwenye michuano ya kimataifa, nadhani sasa tuna muda mzuri wa kujiandaa.

Inabidi sasa nguvu zetu zielekezwe huku, huu ndiyo mkakati ambao sasa tunao, na ili lifanikiwe tunatakiwa kushinda kila mchezo ulio mbele yetu, uwe wa Ligi Kuu au Kombe la FA, miguu ya wachezaji wetu inatakiwa kuwa na nguvu, ikimbie kilometa nyingi," alisema.

Alisema yeye kama kocha kazi yake itakuwa moja tu kuwaelekeza wachezaji wake kwenye uwanja wa mazoezi nini cha kufanya watakapokuwa uwanjani, kwani na yeye anataka kuwapa rekodi yake.

"Kama kocha ni lazima unapokwenda sehemu na wewe uache alama," alisema kocha huyo ambaye alichukua nafasi ya Miguel Gamondi.

Ramovic, ameiongoza Yanga kucheza michezo mitano ya Ligi Kuu, akishinda yote, ambapo Jumamosi wiki hii ataiongoza kwenye mechi ya sita.

Alianza kuiongoza kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC, uliopigwa Novemba 30, mwaka jana, Uwanja wa Ruangwa, Lindi, ikishinda mabao 2-0, Desemba 19, mwaka jana, kwenye Uwanja wa KMC Complex ikaizamisha Mashujaa FC 3-2, kisha ikaikanda Prisons 4-0, Desemba 22, mwaka jana, uwanja huo huo, kabla ya kwenda jijini Dodoma na kutoa kipigo kama hicho dhidi ya Dodoma Jiji na kumalizia kwa kutoa dozi ya mabao 5-0 dhidi ya Fountain Gate, Desemba 29, mwaka jana.

Utakuwa ni mchezo wa mzunguko wa pili, ambapo wa kwanza ulichezwa Agosti 29, mwaka jana, Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera, Yanga ikipata ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Maxi Nzengeli na Clement Mzize.