Pamba Jiji yaota makubwa, nyota wapya wafikia saba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:22 AM Jan 10 2025
Shassir Nahimana.
Picha: Pamba Jiji
Shassir Nahimana.

KATIKA kuhakikisha inajiimarisha na kuwa na kikosi imara kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Pamba Jiji imefanikiwa kumsajili kiungo mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Burundi, Shassir Nahimana, imefahamika.

Taarifa iliyotolewa na Pamba FC jana imesema Nahimana amesajiliwa na timu hiyo akitokea Bandari inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya na inaamini atakuwa na msaada katika timu yao.

Ilisema pia klabu inaendelea kuimarisha kikosi chake kwa kuongeza nguvu katika maeneo yote yaliyokuwa na mapungufu.

"Tunatangaza rasmi tumemsajili kiungo mshambuliaji wa timu ya taifa ya Burundi na nahodha wa Bandari ya Kenya, Shassir (Nahimana). Amejiunga nasi katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili  akitokea Bandari, ambapo alikuwa tegemezi, akihudumu kwa miaka mitano kwenye kikosi cha Burundi," ilisema sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.

Nahimana anakuwa mchezaji wa saba kutua Pamba kipindi cha dirisha dogo linalotarajiwa kufungwa ifikapo Jumatano ujayo.

Wachezaji wengine ambao wamesajiliwa na Pamba Jiji mpaka sasa ni kiungo mshambuliaji, Zabona Mayombya kutoka Prisons, beki wa kushoto, Cherif Ibrahim (Coton Sport ya Cameroon), winga, Deus Kaseke (huru), mastraika, Hamad Majimengi na Habib Kyombo kutoka Singida Black Stars, lakini pia ikiwa imempata kwa mkopo kipa, Mohamed Kamara, kutoka Singida Black Stars.

Mpaka kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Pamba Jiji inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 12 kibindoni, imecheza michezo 16 na kati ya hiyo imeshinda miwili, imepata sare michezo sita na kupoteza minane.

Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imesimama kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar, mechi za michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, pamoja na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), itarejea tena ifikapo Machi Mosi.

Hadi ligi hiyo inasimama, Simba yenye pointi 40 ndio vinara ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga yenye pointi 39, kila timu ikicheza michezo 15.