NBC yamtuza Aziz Ki ikifurahia Kariakoo Dabi na wateja wake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:32 AM Apr 22 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Elvis Ndunguru (kushoto) akikabidhi tuzo kwa mchezaji wa Yanga, Stephano Aziz Ki, aliyetangazwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara kwa mwezi wa Machi.

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC Bank), ambayo ni mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, NBC Premier League, juzi ilinogesha shangwe za mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga kwa kuwapeleka Uwanja wa Benjamin Mkapa wateja wake ili kushuhudia mtanange huo ulioisha kwa timu ya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, huku pia ilikabidhi zawadi kwa mchezaji wa washindi hao, Stephano Azizi Ki, ambaye aliibuka mchezaji bora wa ligi hiyo kwa mwezi Machi,

Zaidi, mdhanimini huyo aliandaa sehemu maalum za kutazama mechi hiyo (viewing points) kwenye baadhi ya mikoa hapa nchini ikiwamo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza,Dodoma, Morogoro, Geita, Mtwara, Kigoma, Meru na Mbinga ili kutoa fursa kwa wapenzi wa mchezo huo ambao hawakuweza kufika uwanjani kufurahia mechi hiyo.  

Jijini Dar es Salaam sehemu maalum zilizoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya kutazama mchezo huo ni Migahawa (Restaurants) za Samaki Samaki zilizopo maeneo ya Mlimani City na Masaki, pia Uvuvi Kempu pamoja na Hoppipola.

Wakizungumza kwenye hafla fupi ya chakula cha mchana na wateja wa benki hiyo kwenye Hoteli ya Hyatt the Kilimanjaro kabla ya kuwapeleka mashabiki hao uwanjani, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa Benki ya NBC, Elibariki Masuke na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji  wa benki hiyo, Elvis Ndunguru, walisema hatua hiyo ni mwendelezo wa utaratibu wa benki hiyo kutumia mechi hizo maarufu kama Derby ya Kariakoo kuandaa matukio kama hayo ili  kutoa fursa kwao  kufurahia ladha ya ligi hiyo inayoendelea kujiongezea umaarufu barani Afrika kutokana na udhamini mnono walioufanya.

Umekuwa ni utaratibu wetu sasa kufurahia na wateja wetu kwenye kila mechi ya Ligi Kuu ya NBC kuanzia Dar es Salaam hadi mikoani kwa kutoa zawadi mbalimbali zikiwamo tiketi za bure kwa baadhi wateja kwa kuzingatia vigezo tofauti. 

"Kwa kutambua uzito wa mechi hii huwa tunaitumia kama siku maalum kufurahia pamoja na wateja wetu kwa kuwaandalia chakula cha mchana, kutoa fursa kwa wao kufahamiana, kubadilishana mawazo yakiwamo ya kibiashara pamoja na kuwakumbusha kuhusu huduma zetu mbalimbali kisha pamoja tunaelekea uwanjani tukiwa kwenye msafara maalum kushuhudia pamoja mechi hiyo, alibainisha Ndunguru.

Zaidi Ndunguru aliongeza kuwa benki hiyo imejipanga zaidi kuendelea kuihudumia ligi hiyo kupitia huduma zake mbalimbali mahususi kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo pamoja na Ligi Daraja la Kwanza (NBC Championship) na Ligi ya Vijana (NBC Youth League) ambazo zote zinadhaminiwa na benki hiyo.

Kwenye hili tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kutoa mikopo ya usafiri kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu kwa masharti nafuu, tunaendelea kutoa huduma za bima za afya kwa wachezaji na mabechi ya ufundi na mikopo mbalimbali kwa kuzingatia vigezo na masharti, aliongeza.

Mbali na matukio hayo pia wateja hao walipata fursa ya kupata huduma mbalimbali za kifedha kutoka NBC kupitia maofisa wa benki hiyo, ikiwamo kufungua akaunti pamoja na kufanya mihamala ya kifedha wakiwa maeneo hayo pamoja na viunga vya vya Uwanja wa Benjamin Mkapa.