BAADA ya kufunga bao pekee lililoipeleka Tanzania katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), zitakazofanyika mwakani nchini Morocco, na kufikisha idadi ya mabao 24 kuifungia timu hiyo, winga, Simon Msuva, amesema ataifikia rekodi ya kupachika mabao mengi kwa taifa lake.
Bao hilo lililofungwa na Msuva juzi lilifanya afikishe mabao 24, moja nyuma ya kinara, Mrisho Ngasa.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Msuva alisema kwa msaada wa Mungu anaweza akaifikia rekodi ya Ngasa kama atakuwa sehemu ya kikosi cha Stars kitakachoshiriki fainali hizo.
"Kwanza namshukuru Mungu kutuwezesha kufuzu AFCON, cha kwanza ilikuwa kufuzu kabla ya kuangalia rekodi binafsi, naamini kwenye fainali zijazo naweza kufikia rekodi ya kaka yangu Ngasa," alisema Msuva.
Alisema ushindi walioupata ni kwa ajili ya watanzania wote lakini rasmi anaupeleka kwa walioathirika na ajali ya kuporomoka ya ghorofa yalitokea Kariakoo hapa jijini.
"Ushindi huu ni kwa ajili yao, kwa pamoja tunahuzunika na kile kilichotokea kwa wenzetu Kariakoo, natoa pole lakini goli nililofunga nalitoa kwa ajili yao," alisema Msuva.
Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta, anashika nafasi ya tatu akiwa na mabao 22.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED