Mpanzu kuipaisha Simba Kagera leo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:43 AM Dec 21 2024
Elie Mpanzu.
Picha:Mtandao
Elie Mpanzu.

KIKOSI cha Simba leo kinatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera kucheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar, huku macho na masikio ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo, yakitaka kushuhudia winga machachari, Elie Mpanzu, akishuka dimbani leo.

Wakati hayo yakiendelea, msafara wa makocha, nahodha wa Kagera Sugar ulipata ajali jana wakitoka klabuni kwenda kwenye mkutano wa waandishi wa habari kwa ajili ya mchezo huo.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa wote waliokuwapo kwenye basi hilo la klabu wapo salama na walibaki kwenye eneo la ajali kwa ajili ya taratibu za kisheria.

Simba itaingia Uwanja wa Kaitaba ikiwa na kumbukumbu ya kutofanya vema uwanjani hapo kwenye michezo yake ya Ligi Kuu ikicheza na Kagera Sugar mara kadhaa.

Pamoja na rekodi kuwa si nzuri kwa Simba inapocheza uwanjani hapo, lakini wanachama na mashabiki wa timu hiyo wameonekana kuwa na matumaini kutokana na kuwa na uwezekano mkubwa wa kumuona kwa mara ya kwanza, Mpanzu, aliyesajiliwa miezi kadhaa iliyopita na timu hiyo akitokea Klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, lakini akitokea Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji kwenye majaribio.

Awali, mchezaji huyo alitarajiwa kucheza kwenye mechi ya Jumatano iliyopita dhidi ya KenGold katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, lakini haikuwezekana kutokana na kuchelewa kupatikana Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC), pamoja na leseni inayomruhusu kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Meneja Habari na Mawasiliano ya Klabu hiyo, Ahmed Ally, kila kitu kilikamilika baadaye wakati mchezo unaendelea.

"Kuhusu Mpanzu, mambo yake yote yameshakamilika, iliyobaki ni kocha mwenyewe tu, Fadlu Davids, kama atamtumia, ila yuko tayari kuitumikia Simba, kwa maana hiyo wanachama na mashabiki wawe tayari kumuona mchezaji huyo akiitumikia timu kwa mara ya kwanza," alisema Ahmed.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Mkuu, Fadlu alisema wapo tayari kwa mchezo huo, huku akisema kuna hatihati ya mchezaji wake Valentin Nouma kuukosa.

"Tuko tayari kwa mchezo, nimeiangalia Kagera Sugar ni timu nzuri kwa hiyo haitokuwa mechi rahisi, tutawaheshimu lakini tunataka tuitawale mechi na kuimaliza mapema.

"Tunaweza kumkosa Nouma aliumia kwenye mchezo uliopita, hajaumia sana, lakini yuko kwenye hatihati ya kutocheza leo, tunaona bora asicheze ili tumtumie kwenye mchezo unaofuata," alisema kocha huyo.

Alisema kuwa kutokana na kuwapo kwa michezo mingi iliyofuatana, amekuwa akikibadilisha kikosi chake mara kwa mara ili kila mchezaji asicheze michezo mingi na kusababisha kuchoka na kiwango kupungua.

"Ni muhimu sana kupumzisha wachezaji na kuwachezesha wengine, angalia mfululizo wa michezo yetu, tumecheza dhidi ya CS Sfaxien, siku mbili baadaye tumecheza dhidi ya KenGold, halafu tutacheza dhidi ya Kagera Sugar na baada ya hapa tunakwenda kucheza dhidi ya JKT Tanzania, hakuna mchezaji anayeweza kucheza dakika 90 michezo yote hii kwa kiwango kile kile," alifafanua kocha huyo.

Wakati huo huo, Katibu wa Chama cha Soka Mkoani Kagera, Al-Amin Abdul, amesema kikosi cha Kagera Sugar kilipata ajali wakati kikienda kwenye mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya mchezo wa leo.

Alisema katika kikosi hicho kulikuwa na Kocha Mkuu na wasaidizi wake, nahodha pamoja na wahusika wengine, ingawa hakujaripotiwa madhara makubwa.

"Tumefanya mkutano na timu moja tu ya Simba iliyofanikiwa kutokea, lakini timu wenyeji, Kagera Sugar, kwa masikitiko imepata ajali ikiwa njiani ikitoka klabuni ikija hapa, ilikuwa na Kocha Mkuu na wasaidizi wake, nahodha wa mchezo na wengine, kwa hiyo bado wapo sehemu ya tukio na tunaendelea kuwasiliana nao," alisema.