Maxime aigawanya Ligi Kuu ‘mara tatu’

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 06:37 AM May 10 2024
Kocha Mkuu wa Ihefu (Singida Black Stars), Mecky Maxime.
Picha: Maktaba
Kocha Mkuu wa Ihefu (Singida Black Stars), Mecky Maxime.

WAKATI Kocha Mkuu wa Ihefu (Singida Black Stars), Mecky Maxime, akisema mechi zote zilizobakia za Ligi Kuu Tanzania Bara ni fainali, amesema kuna ‘vita’ za aina tatu katika ligi hiyo inayoelekea ukingoni.

Ligi Kuu Tanzania Bara imeingia katika raundi ya 26, zimebakia raundi nne na inatarajiwa kumalizika rasmi Mei 28, mwaka huu kwa timu zote 16 kushuka dimbani.

Maxime aliliambia gazeti hili hakuna mechi rahisi iliyobakia katika ligi hiyo kwa sababu kila timu inapambana kusaka ushindi.

Kocha huyo alisema timu zote zinaendelea kufanya maboresho katika vikosi vyao kwa sababu wanataka kuvuna alama muhimu ambazo zitawasaidia kufikia malengo.

“ Ligi imefikia mahali ambazo kila mechi ni sawa na fainali, kuna vita ya kuwania ubingwa, vita ya kujiweka mahali salama na vita ya kubakia kwenye ligi, kwa maana hiyo hakutakuwa na mechi rahisi, kila mmoja anashuka dimbani na malengo yake,” Maxime, nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars alisema.