Mangungu 'alamba' matapishi yake

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:26 AM Jun 14 2024
Mwenyekiti wa  Simba, Murtaza Mangungu.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu.

SAA chache baada ya Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, kutamba klabu ina uwezo wa kusajili na kujiendesha bila ya kutegemea msaada, ameibuka na kumsifu Mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji 'Mo Dewji' ambaye amerejea katika nafasi yake ni mtu jasiri.

Mo Dewji alitangaza kurejea katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na kumteua tena, Salim Abdallah 'Try Again' kuwa mjumbe wa bodi hiyo na kumaliza sintofahamu ya nani atawaongoza Wekundu wa Msimbazi kuelekea kwenye maandalizi ya msimu mpya.

Mangungu pia amekanusha tetesi yeye ni mwanachama wa Pan African iliyoundwa mwaka 1975 na baadhi ya wachezaji na viongozi waliokuwa Yanga.

Akizungumza jijini jana, Mangungu alisema Mo Dewji ni mtu anayetumia nguvu na fedha zake kuisaidia Simba wakati bado mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu haujakamilika.

Alisema bado hajashindwa kuiongoza Simba kama baadhi ya wanachama na mashabiki wanavyotaka ajiuzulu, alisema hamchukulii Mo Dewji kama mwekezaji pekee bali ni kiongozi anayetumia nguvu na fedha zake kuhudumia shughuli za kila siku za klabu hiyo.

"Mimi simchukulii Mo kama mwekezaji pekee, namchukulia kama mtu jasiri ambaye anatumia nguvu na pesa zake kuisaidia Simba, hapa ni yeye na moyo wake amechagua kufanya hivyo, ingekuwa mtu mwingine angesubiri hadi mchakato ukamilike.

Ameruhusu demokrasia ndani ya klabu yetu, kuna timu zingine hapa hapa nchini mtu mmoja tu anaamua kila kitu akiwa amekaa nyumbani wake, nani afanye nini, nani aende wapi kwa sababu tu anatoa pesa zake," alisema Mangungu.

Kiongozi huyo alikanusha tuhuma kuhusu kuwa mwanachama wa Pan African na kusisitiza yeye ni mwanachama halali wa  Simba ambaye alipata kadi mwaka 1993.

"Unajua sisi watu wa mjini tunajuana, haiwezekani ukawa huku ukaamia kwingine wasikujue, mimi nimepata kadi yangu ya uanachama mwaka 1993, sasa tangu wakati huo, leo nije kuihujumu? Halafu wengine wanaonishutumu hata kadi hawana," Mangungu aliongeza.

Kuhusu kufeli usajili wa wachezaji, Mangungu alisema hata baadhi ya timu kubwa Ulaya huwa zinakosea katika mchakato huo lakini akaongeza wapo nyota waliowasajili ambao walionyesha kiwango bora.

"Wanasema Ismail Sawadogo na Pa Omari Jobe, bahati mbaya Sawadogo wakati anakuja 'pre season' alikuwa majeruhi, lakini alikuwa anatoka katika Timu ya Taifa ya Burkina Faso, sio mchezaji wa kiwango kidogo," alisema.

Wakati huo huo, Simba inatajwa kuwa katika hatua za mwisho kumnasa winga wa kushoto wa Power Dyanamos ya Zambia, Joshua Mutale, katika mikakati ya kuanza kuimarisha kikosi chao kama alivyoagiza Mo Dewji.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema maskauti maalumu wa Wekundu wa Msimbazi tayari wako Zambia ili kukamilisha mazungumzo ya kumsajili nyota huyo.

"Muda wowote kuanzia sasa waliokuwa Zambia watamsajili Mutale, winga mzuri sana ambaye msimu uliopita alifunga mabao nane katika Ligi Kuu yao, lengo letu kuelekea msimu ujao ni kumpata winga mwenye uwezo wa hali ya juu kama yeye, na pia mfunga mabao, kilichotuua msimu uliopita hatukuwa na mawinga wafungaji. Huyu tunamwamini kwa sababu tumemshuhudia katika mechi nyingi," kiliongeza chanzo chetu.

Mutale, raia wa Zambia, aliwachachafya mabeki wa Simba, katika mechi ya Tamasha la Simba Day iliyochezwa Agosti 6, mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wenyeji wakishinda mabao 2-0, lakini pia alionyesha kiwango bora katika mchezo wa raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika.