Makosa yake yawanyima pointi tatu Msimbazi, yabakia nafasi ya pili...

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 08:23 AM Feb 07 2025
Mshambuliaji wa Simba, Elly Mpanzu (kushoto), akiwania mpira dhidi ya mchezaji wa Fountain Gate FC, Shaaban Pandu, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ulioko Babati mkoani, Manyara jana
Picha: Mtandao
Mshambuliaji wa Simba, Elly Mpanzu (kushoto), akiwania mpira dhidi ya mchezaji wa Fountain Gate FC, Shaaban Pandu, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ulioko Babati mkoani, Manyara jana

MAKOSA yaliyofanywa na winga, Ladaki Chasambi dakika ya 75 kwa kurudisha vibaya mpira kwa golikipa, Mussa Camara, yameifanya Simba kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji Fountain Gate katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ulioko Babati mkoani, Manyara jana.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi 44 na kuwaacha mabingwa watetezi, Yanga yenye pointi 45 kibindoni wakitawala kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kila moja ikicheza mechi 17.

Simba walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Leonel Ateba ambaye alipokea pasi safi ya Chasambi ndani ya eneo la 18 na kufunga goli la kuongoza dakika ya 57 kufuatia mpira wa adhabu ndogo ulioanzishwa haraka na Jean Charles Ahoua.

Bao hilo lilimfanya mshambuliaji huyo raia wa Cameroon, Ateba, kufikisha mabao nane msimu huu.

Hata hivyo, Chasambi aliwarudisha mchezoni Fountain Gate baada ya kujifunga kwa mpira mrefu aliourudisha golini huku Camara akishindwa kuokoa hatari hiyo na kuzama nyavuni.

Baada ya bao hilo, wachezaji wa Fountain Gate wakaanza kucheza nyuma ya mpira huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo hata hivyo hakuna shambulizi lolote lililozaa bao.

Simba waliendelea kulishambulia lango la Fountain Gate lakini umakini mdogo wa washambuliaji uliwanyima kupata mabao kwa nyakati tofauti tofauti ambapo dakika za 47 na 50, Ellie Mpanzu, alipoteza nafasi ya kuipatia timu yake magoli.

Fountain Gate walipata pigo baada ya golikipa wake, John Noble, kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyozaa kadi nyekundu dakika ya 81 kufuatia kile kilichotafsiriwa na mwamuzi, Abel William, alikuwa anapoteza muda kwa makusudi.

Noble alionyeshwa kadi nyekundu kipindi ambacho timu yake ilikuwa imemaliza idadi ya wachezaji wanaotakiwa kubadilishwa na kulazimu mchezaji mmoja wa ndani kusimama langoni.

Hata hivyo, mapema Simba iliyoanza kwa kasi dakika ya 11 kupitia beki wake, Mohamed Hussein 'Zimbwe Junior' alifunga bao ambalo lilikataliwa kwa tafsiri mfungaji huyo alikuwa ameotea.

Dakika ya 25, Ahoua, alikaribia kufunga lakini shuti lake kali lilidakwa na Noble kabla ya Che Malobe Fondoh kumjaribu tena golikipa huyo kwa mpira wa kichwa ambao ulitoka nje kidogo ya lango.

Kipindi cha pili Simba ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Ahoua, Chasambi, Ngoma  na Hussein na nafasi zao kuchukuliwa na Debora Fernandez, Mukwala, Joshua Mutale na Orkajepha Nouma, mabadiliko ambayo licha ya kuongeza kasi ya kushambulia lakini hayakubadilisha matokeo.

Wakati huo huo katika mechi ya mapema mchana Pamba Jiji kutoka Mwanza ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji.

Matokeo hayo yanaifanya Pamba Jiji kufikisha pointi 15 na kubakia pale pale kwenye nafasi ya 14 kutokana na Tanzania Prisons kupata ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Mashujaa FC na hivyo kufikisha pointi 17.