MABAO mawili ya kujifunga katika mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Dodoma Jiji na Azam FC, yameongeza idadi ya mabao ambayo wachezaji wamejifunga wenyewe kufika manne kwenye michezo 97 iliyochezwa mpaka sasa.
Mechi ya juzi, imeweka rekodi ya wachezaji wawili kujifunga wenyewe kwenye mchezo mmoja.
Katika mechi hiyo, iliyochezwa, Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, kiungo mkabaji wa Azam FC, Yannick Bangala, alijifunga mwenyewe dakika ya saba ya mchezo na kuipa Dodoma Jiji bao la kufutia machozi kwenye mchezo huo ambao Wanalambalamba walishinda kwa mabao 3-1.
Beki wa Dodoma Jiji, naye alijifunga dakika ya 60 katika jitihada zake za kutaka kuokoa, akiipa Azam FC bao la tatu kwenye mechi hiyo, timu yake ikipokea kipigo cha mabao 3-1.
Mchezaji wa kwanza kujifunga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ni Fred Tangalo wa KMC, akifanya hivyo Septemba 19, mwaka huu, katika mchezo kati ya timu yake na Azam FC, ukipigwa Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ambao Azam ilishinda mabao 4-0, moja kati ya hilo lilikuwa la KMC kujifunga wenyewe kupitia kwa beki huyo.
Beki wa kulia wa Simba, Kevin Kijili alijifunga, Oktoba 19, mwaka huu, katika mchezo kati ya timu yake na Yanga, uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, na lilikuwa bao pekee, Yanga ikishinda 1-0.
Kwa mujibu wa Kitengo cha Takwimu na Rekodi cha Dawati la Michezo la Nipashe, jumla ya mabao 192 yamefungwa mpaka sasa kwenye Ligi Kuu katika michezo 97 iliyochezwa, 20 yakifungwa kwa mikwaju ya penalti, manne yakiwa ya kujifunga.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED