Kuelekea michezo ya mwisho Ligi Kuu, Gamondi awapa neno wachezaji wake

By Faustine Feliciane ,, Saada Akida , Nipashe
Published at 05:58 PM May 09 2024
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha: Yanga SC
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.

BAADA ya ushindi wa juzi wa dakika za mwisho wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ametoa neno kwa wachezaji wake akiwataka kuongeza umakini na kutodharau mpinzani kwenye michezo iliyobakia kuhitimisha Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Gamondi amekiri kuwa kwa sasa kila mchezo ni mgumu kutokana na umuhimu wa pointi tatu kwa kila timu hivyo wanapaswa kuwa makini katika kila mchezo hasa ile watakayocheza ugenini.

Yanga imebakisha michezo minne kumaliza ligi ambapo michezo miwili watacheza ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma United na michezo miwili watacheza nyumbani dhidi ya Tabora United na Tanzania Prisons.

Akizungumza jana, Gamondi alisema michezo hiyo iliyobakia ni muhimu sana kwao lakini haitakuwa michezo rahisi kwao kutokana na wapinzani wao kuhitaji pointi tatu ili kujinasua katika nafasi walizopo sasa kwenye msimamo.

"Tunatakiwa kuongeza umakini zaidi, mchezo dhidi ya Kagera Sugar umetupa picha ya ugumu wa michezo ya mwishoni mwa ligi, kila timu inapambana kujinasua katika nafasi walizopo sasa hivi lazima wachezaji wangu wawe makini na kupambana muda wote wa mchezo ili kufikia malengo ya kutetea ubingwa wetu," alisema Gamondi na kuongeza, 

"Ni ngumu sana kupata pointi tatu kirahisi kwa timu zilizo kwenye eneo la hatari kwenye msimamo kwa sababu wanahitaji kujiondoa huko, kufanya hivyo wanapambana sana hasa wanapocheza na timu kubwa kama Yanga.

Alisema ana hofu na michezo ya ugenini kutokana na aina ya viwanja wanavyoenda kuchezea pamoja na umuhimu wa pointi tatu kwa wapinzani wao.

"Tuna michezo ya ugenini, pamoja na upinzani kutoka kwa wenyeji wetu, lakini pia viwanja vimekuwa changamoto kwetu, hivyo lazima tuhakikishe tunacheza kwa malengo na kujituma zaidi, baada ya mchezo na Kagera nimewaambia wachezaji wangu nini nataka kwenye michezo hiyo iliyobaki," alisema Gamondi.

Yanga wanaongoza wakiwa na pointi 68 huku wakibakiza michezo minne kabla ya ligi kumalizika ambapo watakuwa na michezo miwili ugenini wakianza na Mtibwa Mei 13.

Baada ya mchezo huo watakuwa na kibarua kingine cha mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Ihefu FC utakaochezwa kati ya Mei 17 au 18.

Mei 22 watakuwa ugenini dhidi ya Dodoma Jiji FC baada ya hapo watarudi nyumbani kucheza na Tanzania Prisons na baadaye kumalizana na Tabora United.