KUELEKEA DABI: Simba, Yanga hatari zaidi maeneo haya

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:38 AM Oct 17 2024
Nembo ya Simba na Yanga.
Picha:Mtandao
Nembo ya Simba na Yanga.

ZIKIWA zimebakia siku chache kabla ya mechi ya watani wa jadi, vigogo hao wa soka nchini wameonekana kuwa na sifa tofauti za kuleta hatari na kufunga mabao msimu huu, Wekundu wa Msimbazi wanaonekana hatari zaidi wanapoingia ndani ya eneo la hatari, huku Yanga wao hawana masihara kwa kupiga mashuti kutoka mbali.

Mbali na hilo, mabao ya Simba msimu huu inaonekana kupata mabao mengi wakitumia mipira ya pembeni, krosi, huku Yanga ikifunga kwa pasi za kupenyeza pamoja na faulo.

Kwa mujibu wa dawati la takwimu la Nipashe, Simba ambao mpaka sasa imepachika mabao 12 katika Ligi Kuu Tanzania Bara, magoli yake 11 wameyafunga na wachezaji wakiwa ndani ya boksi.

Wachezaji wa Simba waliopachika mabao hayo ndani ya boksi ni pamoja na Che Fondoh Malone, Valentino Mashaka, Awesu Awesu, Edwin Balua, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua (amefunga mawili),  Leonel Ateba (amepachika pia mawili), Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' na Fabrice Ngoma.

Kwa maana hiyo, mabeki wa Yanga wanatakiwa kutowaruhusu wachezaji wa Simba kuwa huru na mpira wanapokuwa ndani ya eneo la hatari.

Mabao sita, ambayo ni nusu ya mabao yote ya timu hiyo yamefungwa na faulo tatu zilizopigwa na Ahoua mara mbili, Zimbwe Jr na Shomari Kapombe.

Iwapo mabeki wa Yanga wanataka kuwadhibiti Simba ili wasifunge, wanapaswa pia kuchunga maeneo yao ya pembeni kutowaruhusu kutembea sana huko, kwa sababu wanaonekana ni hatari na mpango mkakati wao wa mabao unatokea huko.

Kwa upande wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wao wanaonekana ni hatari zaidi kufunga mabao wakiwa nje ya eneo la hatari.

Wakati Simba wana bao moja tu wakifunga nje ya boksi, likiwekwa na Mashaka, Yanga wana mabao mawili waliyofunga wakiwa nje ya hatari, tena yote yakifungwa na Mkongomani Maxi Nzengeli.

Kiungo huyo mwenye mabao matatu, mawili akipachika akiwa nje ya eneo la hatari, akifanya hivyo, Agosti 29, mwaka huu, Yanga ilipoifunga Kagera Sugar mabao 2-0, Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera na Oktoba 3, mwaka huu walipoichakaza Pamba Jiji magoli 4-0.

Kwa takwimu hii, inaonyesha licha ya Yanga kuwa na mabao mengi ya nje ya boksi kuliko wapinzani wao Simba, lakini Maxi ndiye mchezaji wa kuchungwa na mabeki wa Wekundu wa Msimbazi, asitazame mapana ya lango akiwa mbali. Ndiye mchezaji aliyefunga bao katika mchezo wa mwisho timu hizo zilipokutana Agosti 8, mwaka huu kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, Simba ikilala kwa bao 1-0.

Wakati pia Simba ikiwa haina bao lolote kwa faulo ya moja kwa moja, au lililopatikana kwa kuunganishwa kwa mpira hiyo, Yanga ina mabao mawili yaliyotokana na mipira ya adhabu.

Ingawa si ya faulo ya moja kwa moja, lakini mipira iliyopigwa na Stephane Aziz Ki na Nzengeli, yote ilitua kichwani kwa beki, Ibrahim Hamad 'Bacca' na kuiweka wavuni katika michezo miwili tofauti.

Ilikuwa ni katika mchezo wa kwanza uliochezwa ni Septemba 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Yanga ikishinda bao 1-0 dhidi ya wenyeji KenGold, na Oktoba 3, mwaka kwenye Uwanja wa Azam Complex, Yanga ikiichapa bila huruma Pamba Jiji mabao.

Hili ni angalizo kwa wachezaji wa Simba kuongeza umakini pale faulo za Yanga zinapopigwa kuelekea langoni kwao, wapinzani wao wakiongozwa na Bacca, wanaonekana wana uwezo mkubwa wa kuunganisha mipira hiyo iliyokufa.

Wakati huo huo, Kampuni ya Ujenzi ya Knauf imeingia mkataba wa mwaka mmoja na Simba ambayo hivi karibuni itashiriki hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mkurugenzi wa Knauf wa Kanda Afrika Mashariki, Ilse Boshoff, alisema jijini jana  uhusiano huo na Simba ni mkubwa na utakuwa na faida kwa pande zote mbili kitaifa na kimataifa.

"Tupo nchi zaidi ya 90 duniani na malengo yetu ni kuzidi kujitanua zaidi, matumaini yetu uhusiano huu na Simba utakuwa msaada kwetu kuendelea kujulikana huku  tukiendelea kuzalisha bidhaa bora za ujenzi kutoka Ujerumani," alisema Boshoff.

Naye Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, alisema mkataba huo utakuza chapa ya Knauf pamoja na Simba na kuongeza hawakuangalia thamani yake bali umuhimu wa kuendelea kujitangaza kimataifa.

"Sisi kama Simba hatukuangalia zaidi thamani ya mkataba bali tumeangalia kujitangaza na kuyavutia makampuni mengine ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza kwetu na tunawakaribisha," alisema Mangungu.