Kally amtabiria Chilunda kufanya makubwa KMC

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:04 AM Jan 21 2025
Kally amtabiria Chilunda   kufanya makubwa KMC.
Picha: Mtandao
Kally amtabiria Chilunda kufanya makubwa KMC.

KOCHA Mkuu wa KMC, Kalimangonga Ongalla, amesema ana uhakika na straika wake mpya, Shaaban Chilunda, kufanya vizuri Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoingia kwenye mzunguko wa pili, mwanzoni mwa mwezi ujao.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kally alisema usajili wa mchezaji huyo ni pendekezo lake kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji, hivyo ana uhakika na alichokifanya.

Alisema anamfahamu Chilunda kwa sababu alikuwa naye Azam FC, na walifanya naye kazi nzuri, ndiyo maana amemvuta KMC.

"Tumesajili wachezaji kadhaa, wote ni kwa mapendekezo ya benchi la ufundi, tumemsajili Chilunda, ni straika mzuri sana, mimi namfahamu nimefanya naye kazi nikiwa Azam FC, naamini kabisa kuwa kwa kushirikiana na wachezaji wengine ataleta mabadiliko makubwa kwenye kikosi, hasa sehemu ya ushambuliaji," alisema Kally.

Chilunda, amerejea tena KMC kwa mara ya pili, kwani aliichezea timu hiyo kwa mkopo Januari mwaka jana akitokea Simba ingawa aliachana nayo Julai mwaka jana.

Kabla ya hapo, alikuwa mchezaji wa Azam FC, baadaye akaenda kucheza soka la kulipwa Klabu ya CD Tenerife ya Hispania na Moghreb Atletico Tetouan ya Morocco.

Akiwa na Simba, hakufunga bao lolote kwenye Ligi Kuu Bara, na akiwa KMC alifunga moja katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania uliopigwa Februari 27 mwaka jana, timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Klabu ya KMC, Khalid Chukuchuku, timu hiyo imesajili wachezaji watano kipindi cha dirisha dogo la usajili lililofungwa Jumatano iliyopita.

Aaliwataja baadhi yao, mbali na Chilunda kuwa ni Hamad Pipino, kutoka timu ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, na Deusdedith Okoyo akitokea Polisi Tanzania, huku wengine wawili akisema majina yao yatawekwa hadharani baada ya baadhi ya mambo kuwekwa sawa.