Gidabuday kuzikwa Manyara Jumamosi, BMT na RT zamlilia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:33 AM Sep 11 2024
KATIBU Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday
Picha: Mtandao
KATIBU Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday

KATIBU Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana kwa ajali ya gari jijini Arusha, anatarajiwa kuzikwa Jumamosi kijijini kwao, Nangwa wilayani Katesh, Manyara.

Taarifa iliyotolewa jana mchana na shirikisho hilo, ilieleza kuwa kwa sasa msiba wa kiongozi huyo wa zamani wa RT, upo nyumbani wake, Maroroni, Maji ya Chai mkoani Arusha.

"Msiba wa kiongozi wa zamani wa RT upo nyumbani kwake Maroroni, Maji ya Chai, Arusha na mazishi yake yanatarajiwa kufanyika Jumamosi Septemba 14, kijijini kwao, Nangwa, Katesh mkoani Manyara," ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na Idara ya Habari ya Shirikisho ya RT.

Wakati huo huo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), limeeleza kusikitishwa na kifo hicho, likisema taifa limepoteza mtu muhimu kwenye nyanja ya riadha.

Katika salamu zake kwenda kwa RT, BMT imetoa pole kwa shirikisho hilo kwa familia na wadau wa riadha nchini.

"Baraza la Michezo (BMT), linatoa pole kwa familia na wadau wa riadha nchini kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Katibu wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Gidabuday kilichotokea Septemba 10, mkoani Arusha, Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa, jina lake lihimidiwe," ilisema BMT katika salamu zake za rambirambi.

Kwa mujibu wa Mjumbe wa Riadha Kanda ya Mashariki, Alfredo Shahanga, kiongozi huyo wa zamani wa shirikisho hilo alifariki dunia saa 7:00 usiku wa kuamkia jana kwa kugongwa na gari jijini Arusha, eneo la Majani ya Chai.

"Ni kweli Gidabuday hatunaye, alipata ajali ya gari, na kwa mujibu wa mashuhuda ni kwamba alifariki dunia hapo hapo, ni masikitiko makubwa kwetu na wapenda michezo, si wa riadha tu, bali michezo yote," alisema Shahanga kwa masikitiko.

Gidabuday, aliutwaa Ukatibu Mkuu wa RT mwaka 2016 katika uchaguzi Mkuu kwa kupata kura 38 na kumshinda mpinzani wake mkubwa, Michael Washa, aliyepata kura 24, na alidumu kwenye kiti hicho hadi 2019, alipojiuzulu mwenyewe kwa kile alichokisema kuwa ni kwa manufaa ya mchezo huo.

Alijiuzulu bila shinikizo lolote na kumkabidhi madaraka Ombeni Zavalla, akiwataka viongozi wengine waige mfano wake.

Akiwa madarakani alifanikiwa kutwaa medali mbili za Shaba zilizoletwa na mwanariadha Alphonce Simbu katika mashindano ya Dunia ya 2017 nchini Uingereza, na Francis Damiano, aliyeshinda medali kama hiyo kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa Vijana mwaka huo huo nchini Bahamas.

Kabla na baada ya madaraka, Gidabuday, alikuwa akiuishi mchezo huo, mara kwa mara akitoa mawazo yake kwenye vyombo vya habari kuhusu maendeleo ya mchezo wenyewe na hata kukosoa baadhi ya mienendo ya viongozi kama akiona mambo hayaendi sawa.