SARE ya bao 1-1 iliyoipata Simba kwenye Uwanja wa Novemba 11, Luanda nchini Angola juzi dhidi ya Bravos do Maquis, imeifanya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa mara sita ndani ya misimu saba, huku Kocha Kuu, Fadlu Davids, akisema kazi haijaisha kwani lengo la pili ni kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya CS Constantine ya Algeria na kuongoza kundi.
Akizungumza baada ya kutamatika kwa mchezo huo wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika, Fadlu raia wa Afrika Kusini, alisema kufuzu lilikuwa lengo la kwanza, la pili ni kushinda mchezo ujao kwa sababu moja tu, ya kuongoza kundi kitu ambacho kitakuwa faida kubwa kwa timu hiyo.
Alisema mara kwa mara Simba huishia hatua ya robo fainali kwenye mechi za kimataifa zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), hivyo kama safari hii ikiongoza kundi itakuwa na nafasi nzuri na kuanzia ugenini na kumalizia nyumbani, kitu ambacho kinaweza kuwa faida kubwa ya kuweza kutinga hatua ya nusu fainali.
"Nawapongeza Wanasimba wote kwa kuweza kufuzu kutinga hatua ya robo fainali. Tulitaka kufuzu kabla ya mchezo mmoja na tumeweza kufanya hivyo, nawashukuru sana wasaidizi wangu kwenye benchi la ufundi pamoja na madaktari wangu, wote hawa wamefanya kazi kubwa sana.
"Kwa sasa tunaangalia mechi ya mwisho, tunataka kushinda ili kuongoza kundi, umuhimu wa mchezo wa mwisho ni mkubwa sana, kwani tutapata faida ya kuanzia ugenini, ukifanikiwa kuwabana wapinzani wako kwao, halafu ukamalizia nyumbani, unakuwa na faida kubwa, kama tunataka kuvunja rekodi yetu na kufuzu hatua ya nusu fainali, ushindi dhidi ya CS Constantine ni muhimu sana," alisema Fadlu.
Simba itacheza mchezo wa mwisho Jumapili ijayo dhidi ya CS Constantine katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, saa 10:00 alasiri, mechi ambayo inahitaji ushindi ili ifikishe pointi 13, na kuwaacha wapinzani wao na pointi zao 12 kama inataka kuwa kinara wa Kundi A.
Akizungumzia mchezo huo, alisema walimiliki mpira kwa kiasi kikubwa huku wapinzani wao wakitegemea zaidi mashambulizi ya kushtukiza na mipira iliyokufa tu.
"Tumefanya makosa, tumewapa bao, lakini muda mwingi wa mchezo tumekuwa bora, tumepiga mashuti 26 langoni mwao, tumemiliki kwa asilimia 56.
"Wapinzani wetu walikuwa hatari zaidi kwenye mipira ya faulo na kushambulia kwa kushtukiza tu, hawakuwa na kitu kingine zaidi ya nafasi ya bao tulilowapa," alisema.
Hii ni mara ya sita kwa Simba kufuzu hatua hiyo kwa misimu saba ya michuano ya CAF tangu 2018.
Rekodi zinaonesha kuwa tangu msimu wa 2018/19, Simba imekosa kutinga hatua hiyo msimu wa 2019/20 tu ilipotolewa hatua ya awali na UD Songo ya Msumbiji, lakini baada ya hapo imekuwa ikitinga hatua za robo fainali, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, mara tano mfululizo.
Imetinga Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne, 2018/19, 2020/21, 2022/23 na 2023/24, huku msimu wa 2021/22 na 2024/25 ikitinda robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
"Tumefanikiwa kudumisha utamaduni wetu wa kutinga hatua ya robo fainali si jambo dogo, wachezaji wanaingia na kutoka, wengine wanapungua viwango, lakini taasisi imeweza kusimamia mwendelezo huu jambo ambalo si dogo, ukiangalia tangu kipindi chote hicho mpaka sasa timu ambazo zimeweza kuwa na mwendelezo wa kiwango hiki hazizidi tatu, labda Al Ahly, na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, zingine zinaingia na kutoka, angalia Wydad Casablanca na baadhi ya nyingine kuwa hazipo kwenye hatua hii msimu huu," alisema Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.
Wakati huo huo, beki Fondoh Che Malone, ameomba radhi wanachama na mashabiki wa Simba kutokana na kosa alilofanya lililosababisha bao la kwanza kwa Bravos do Maquis, kabla ya Leonel Ateba kusawazisha.
"Ningependa kuomba msamaha kwa familia nzima ya Simba kwa kusababisha madhara mara mbili kwenye mechi za kimataifa.
"Nabeba lawama kwa makosa yangu, na naahidi kufanya kazi kwa bidii ili kufanya vizuri zaidi katika siku zijazo. Ninaomba radhi kwa dhati. Asante Simba. Asanteni mashabiki kwa kunitia moyo kila wakati licha ya makosa yangu," alisema beki huyo wa kati raia wa Cameroon.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED