Fadlu awataka mabeki Simba kuamua mechi Tabora United

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:03 AM Jan 29 2025
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

WAKATI wachezaji wote wa Simba waliokuwa wemepewa mapumziko baada ya majukumu ya mechi za kimataifa wakirejea jana na kufanya mazoezi ya pamoja kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu mzunguko wa pili dhidi ya Tabora United, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema safu yake ya ulinzi ndiyo itakayoubeba zaidi mchezo huo Jumapili wiki hii.

Timu hizo zinakutana Jumapili katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Simba ikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Agosti 18, mwaka jana, Dimba la KMC Complex, Dar es Salaam, yaliyofungwa na Che Fondoh Malone, Valentino Mashaka na Awesu Awesu.

Akuzungumza kuelekea kwenye mchezo huo, Fadlu alisema kwa sasa safu yake ya ulinzi imezidi kuimarika, ikiwa haina rekodi ya kuruhusu sana mabao kwenye viwanja vya ugenini, kitu kinachomfanya kuwa na imani ya kufanya vizuri katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alisema anatarajia utakuwa mgumu kama ilivyokuwa michezo mingine ya ligi huko nyuma, lakini anakiona kikosi chake kikiimarisha siku hadi siku, hasa kila kinapocheza michezo ya kimataifa, huku sehemu ya ulinzi ikiwa imara zaidi.

Fadlu alifafanua kuwa hapo nyuma kidogo kulikuwa na matatizo ya kuruhusu bao au mabao hata kama timu ikishinda, lakini kwa sasa hali hiyo imetengemaa, jambo ambalo ni zuri kwenye mchezo wa soka.

"Tumekuwa tukiruhusu mabao ambayo ukiyaangalia ni ya makosa binafsi ya mchezo mmoja mmoja, ina maana hatukuwa tunaruhusu mabao ya kimfumo kwa maana hiyo hapo tupo vizuri, baadaye nikaanza kazi ya kufanya kwa mabeki wangu wasiwe wanafanya makosa binafsi ambayo yanasababisha turuhusu mabao mepesi. 

"Tumeona kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya CS Constantine, pia Kombe la FA dhidi ya Kilimanjaro Wonders, hatukuruhusu bao, liwe la binafsi au la mfumo," alisema kocha huyo.

Hata hivyo, alisema katika michezo mingi ya ugenini ya Ligi Kuu ambayo Simba ilicheza nje ya Dar es Salaam, iliruhusu mabao mawili tu dhidi ya Kagera Sugar, uliochezwa Desemba 21, mwaka jana, ambao walishinda 5-2.

"Tumecheza mechi za nje, huko mara nyingi tumepata ushindi wa mabao machache na hatukuwa tunaruhusu sana mabao, hii inaonesha staili yetu pia inategemea na viwanja tunavyocheza, kuna vingine haviruhusu kucheza sana nyuma," alisema kocha huyo.

Alisema kama mabeki wake watacheza kama walivyofanya katika michezo hiyo miwili, wana uhakika wa ushindi kwani hawatoruhusu wavu wao kuguswa na pia wana uhakika wa kupata bao moja au zaidi kwenye mchezo huo.

Wakati huo huo wachezaji wote wa Simba waliokuwa wemepewa mapumziko baada ya majukumu ya mechi za kimataifa wamerejea na jana wamefanya mazoezi ya pamoja kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Tabora United.

Akizungumza na Nipashe jana, Meneja Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema baada ya mchezo wao wa mwisho wa Kombe la Shirikisho hatua ya makundi dhidi ya CS Costanine, Simba iliwapa mapumziko wachezaji wote waliohusika katika mchezo huo ambapo mapumziko yao yameisha juzi na jana wote walihudhuria mazoezi ya timu hiyo.

"Kulikuwa na makundi mawili ya wachezaji kwenye mapumziko, wale ambao wenyewe hawakuhusika au hawakutumika kwenye michezo yetu miwili ya mwisho ya Kombe la Shirikisho Afrika wenyewe mazoezi walianza Januari 24, wengine walioshiriki michuano hiyo ya CAF likizo yao imeisha jana (juzi) na leo (jana), wameripoti mazoezini kujiandaa na mchezo dhidi ya Tabora United," alisema.

Naye Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Murtaza Mangungu, amesema mechi dhidi ya Tabora United ni mechi kama zingine tu za Ligi Kuu, hawatoenda kwa kuhofia kwani Simba ni timu kubwa inayoweza kucheza mchezo wowote ndani na nje ya nchi.

"Tutakwenda kucheza kama tunacheza mechi nyingine yoyote, Simba haiwezi kuhofia kwenda kucheza  soka Tabora, kama tunatoka hapa kwenda nje ya nchi na timu kubwa zenye viwango vikubwa Afrika, na wakati mwingine inashinda, Simba itacheza na timu yoyote popote, kama walizifunga Yanga, Azam ni wao, sisi tumewafunga kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza," alitamba.