KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema anatengeneza mfumo ambao utawawezesha wachezaji wake wote kuweza kufunga mabao au kutoa pasi za mwisho kwa manufaa ya timu na si kutegemea mastraika kufunga au mchezaji mmoja kutoa pasi ya mwisho 'asisti.'
Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam wakati wa maandalizi ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine unaotarajiwa kucheza nchini Algeria Jumapili wiki hii, Fadlu alisema mafanikio ya timu hayawezi kuletwa na mchezaji mmoja pekee yake, hasa kufunga mabao, hivyo anatengeneza mfumo utakaomwezesha kila mchezaji kuanzia mabeki, viungo mpaka washambuliaji kupachika mipira ndani ya wavu.
"Natengeneza kikosi ambacho kitakuwa na ushirikiano, kitacheza kama timu, mafanikio hayawezi kumtegemea mchezaji mmoja ndiyo afunge mabao, kila mmoja anatakiwa achangie ushindi, ni golikipa tu ndiyo kazi yake itakuwa ni kuzuia mabao yasiingie wavuni kama alivyofanya Moussa Camara katika mchezo dhidi ya Bravo do Maquis, waliobaki wote pamoja na majukumu yao mengine, lakini wanatakiwa wachangie 'asisti' na kufunga mabao pia," alisema kocha huyo.
Alisema mbinu na mfumo huo lengo lake ni kuleta tija katika kupata mabao mengi zaidi kwenye mchezo ili kuleta maendeleo kwenye kikosi chake.
Fadlu alisema hayo siku kadhaa timu yake ikitoka kucheza mchezo wa kwanza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho dhidi ya Bravo do Maquis, ikishinda bao 1-0, ambapo baadhi ya wadau wa soka na mashabiki wanadai kulikuwa na viashiria kwa uchoyo kwa baadhi ya wachezaji kunyimana pasi kwenye maeneo muhimu, huku kila mmoja akipata mpira akionekana kutaka kuamua mchezo mwenyewe.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo dhidi ya CS Constantine, unaotarajiwa kupigwa Jumapili saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui, alisema yanaenda vizuri na wamejiandaa kukabiliana na timu hiyo.
"Katika hatua ya makundi hakuna timu rahisi, tunakwenda kucheza mchezo mgumu ugenini, lakini malengo yetu yapo pale pale, ama kushinda au ikishindikana kutoa sare," alisema.
Fadlu pia alionekana kufurahishwa na ujio wa mchezaji Elie Mpanzu ambaye ataanza kuitumikia timu hiyo kuanzia Desemba 15, mwaka huu akisema ataisaidia sana kwenye mechi zijazo za kimataifa baada ya mchezo wa Jumapili.
"Nadhani kutakuwa na maingizo mapya machache, akiwamo Mpanzu, huyu tayari namfahamu, tunafanya naye mazoezi, ni mchezaji mzuri kwa kweli, anaweza kucheza winga zote mbili, ana uwezo wa kucheza nyuma ya mshambuliaji, yeye mwenyewe binafsi anaweza kufanya kitu kitokee, anaweza kubaki na mabeki mmoja au wawili akavuruga wote, ataingiza kitu kipya kwenye kikosi chetu," alisema Fadlu, raia wa Afrika Kusini.
Kama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa kwa mujibu wa uongozi wa Simba, kikosi hicho kinatarajiwa kuondoka Jumatano kwenda mji wa Constantine, Algeria ambako mchezo huo utafanyika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED