WAKATI Azam FC ikisema inalitaka kwa udi na uvumba Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), maarufu kama FA Cup, Mtibwa Sugar imesema haina haja nalo kwani malengo yao ni kupambana ili kubaki Ligi Kuu.
Akizungumza juzi baada ya mechi ya hatua ya 16-bora dhidi ya Azam FC, nahodha wa Mtibwa Sugar, Oscar Masai, alisema hawakuutilia maanani sana mchezo huo kwa sababu akili yao ipo katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayofuata dhidi ya Geita Gold utakaochezwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Aprili 13, mwaka huu.
Katika mechi hiyo ambayo Mtibwa ilibamizwa mabao 3-0, beki huyo wa kati alisema kocha wao, Zuberi Katwila aliwaambia wakacheze kwa kufurahia soka na wasikamie sana kwa sababu wanaweza kutengeneza majeruha na kuwa hatari kwa mchezo ujao.
"Tumeanza kufungwa bao la mapema, hatukuwa tayari, tulianza chini sana, wao wakatumia nafasi hiyo kupata bao.
"Mechi hii ilikuwa ni maandalizi ya mchezo unaofuata wa Ligi Kuu kwa sababu huko ndiko tunakoangalia sana, tunapambana ili tusishuke daraja.
"Mwalimu wetu alisema tuje kucheza mechi lakini 'tuinjoi' tu 'tusitoe macho' sana na wachezaji tukapata majeraha kwa sababu malengo yetu makubwa ni kwenye Ligi Kuu," alisema Masai.
Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo, alisema wachezaji wake hawakucheza vema katika mchezo huo badala yake kila mmoja alicheza kibinafsi.
"Pamoja na kushinda, lakini timu haikuwa vizuri, ni kawaida wakati mwingine kwa michezo ya aina hii," alisema kocha huyo.
Naye mmoja wa wafungaji wa bao moja kati ya hayo matatu yaliyowapeleka Azam hatua ya robo fainali ya Kombe la FA, Abdul Selemani Sopu, alisema malengo yao ni kutwaa ubingwa na si kitu kingine chochote.
"Tulijua kuwa hii si ligi, hili ni Kombe la FA ukifungwa tu umetolewa, ni mechi inayohitaji ushindi tu, na hicho ndicho tulichojiandaa nacho, ndiyo maana tulianza kwa kasi kubwa lengo ni kupata bao la mapema na kweli ikawa hivyo. Malengo yetu ni kuchukua ubingwa huu wa Kombe la FA," alisema Sopu. Mabao mengine ya Azam yalifungwa na Feisal salum, Ayoub Lyanga.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED