SIKU moja baada ya kurejea nchini, Wasanii wa filamu na Tamthilia wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kugharamia safari yao ya Korea iliyokuwa na lengo la kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya sanaa ya filamu na tamthilia duniani.
Wakizungumza na mwandishi wa habari jana baada ya kurejea kutoka Korea walipokwenda huko tangu Julai mosi, walisema wamejifunza namna ya kufanya kazi zao za kisanii kama njia ya kujiletea maendeleo na kukuza sekta hiyo nchini Tanzania.
Baadhi ya wasanii waliokwenda Korea ambao walizungumza na waandishi wa habari na kumshukuru Rais Samia, ni pamoja na Steve Nyerere kama Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Idris Sultan, Wema Sepetu, Irene Uwoya, Monalisa, Irene Paul, Gertrude Mwita na Godliver Gordian.
Wasanii hao kwa umoja wao wamempongeza Rais Samia kwa kuwapa fursa kwenda kujifunza zaidi kuhusu sanaa na wanaamini walichojifunza huko kitawasaidia katika shughuli zao.
Kwa upande wa maboresho ya sekta hiyo, wasanii hao waliitaka serikali kuweka mikakati zaidi kugharamia utendaji kazi wa Sanaa wa Tanzania kama walivyofanya Korea kwa kuweka bajeti ya uandaaji wa filamu zao hali iliyoibua na kuendeleza sekta hiyo.
"Ili kuwa wakubwa na kutangaza makampuni na viwanda vyetu, watumike wasanii wa ndani kutangaza shughuli zao," alisema Steve,
Safari ya wasanii hao imekuja wakati ambao Rais Samia alitangaza neema kubwa kwa wasanii ya kugharamia safari zao pindi atakapokuwa na ziara za kikazi nje ya nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED