MADINI muhimu au kitaalamu ‘critical minerals’ ambayo ni pamoja na shaba, lithiamu, nikeli, kobalti na ‘rare earth elements’ ni malighafi inayohitajika mno duniani kwenye teknolojia za kielektroniki na kidijitali pamoja na kupata vifaa vya kuzalisha nishati mbadala.
Aidha, ni muhimu kwani ndizo malighafi za viwanda vya kielektroniki kuanzia mashine za tiba kama MRI ambayo huundwa na madini jamii ya rare-earth metals.
Ni malighafi za simu za mkononi, kompyuta, roboti, injini za ndege, na pia ndizo zinazotengeneza viambato kwenye mitambo ya kuendesha umeme wa upepo na jua pamoja na betrii za magari.
Lakini kwenye madini hayo hakuna usalama, zinageuka kuwa ukanda wa vita. Ndiyo vita ya kiteknolojia.
Kwa mfano, nchini Congo watu takribani 4,000 wamefariki dunia hivi karibuni kisa vita ndani ya eneo lenye madini ya kimkakati.
Ni mapigano katika jimbo la Kivu Kaskazini kwenye mji wa Goma. Ndilo eneo mojawapo ya miji mikuu ya uchimbaji madini yanayohitajika mno duniani leo. Kuna dhahabu, bati, kobalti na koltani.
Utajiri wa Goma unaweza kuwa ndiyo shida na chanzo cha vifo vya maelfu ya watu wasio na hatia wala wasiojua kinachoendelea kwenye viwanda vya vifaa vya kielektroniki.
Inakadiriwa kuwa Kongo inamiliki asilimia 70 ya madini ya kobalt duniani, ambayo yanahitajika kutengeneza betri za lithiamu-ion za simu za mkononi, magari ya umeme na aina nyingi za sigara za kielektroniki, inasema BBC.
Ndiyo madini ya kimkakati yanayohitajika duniani kote kuanzia Ulaya, China hadi Marekani ili kupunguza utoaji wa gesi chafuzi na kuwezesha kuhama kutoka kwenye nishati chafu za visukuku au ‘fossils’ kama petroli, gesi, dizeli na makaa ya mawe.
Madini hayo yanahitajika, kuongeza vyanzo vya nishati safi kama upepo na jua kwa kuwa ndivyo vinavyotengeneza viambato.
Ndiyo wachambuzi wanasema kinachochochea vita Congo ni utajiri wa madini hayo yanayohitaji zaidi duniani leo ili kuunda vifaa vya kielektroniki kwa gharama nafuu.
Lakini pia kukabiliana na ongezeko la joto duniani linalotokana na kutumia nishati chafu.
Mapigano siyo Congo pekee, itakumbukwa mwaka 2021 Afghanistan ilikuwa uwanja wa vita. Na pia taifa hilo linatajwa kuwa na madini aina nyingi kama chuma, shaba na dhahabu pamoja na akiba ya madini adimu ya ‘lithiamu’ yanayotajwa kuwa ya kutosha na pengine akiba kubwa zaidi duniani.
Kwa sasa mataifa ya China, Congo na Australia ndiyo wazalishaji wakubwa kwa karibu asilimia 75 ya madini adimu hasa ‘lithiam’ na kobalt, inasema BBC.
Hata hivyo, kuyasaka kwa njia rahisi ndicho kinachoyagharimu maisha ya watu hasa Congo.
BBC inaongeza kuwa serikali ya Marekani inakadiria kuwa kiwango cha madini ya lithiam yanayopatikana Afghanistan kinaweza kulingana na kile kinachopatikana nchini Bolivia huko Amerika Kusini.
Bolvia ndiyo inayoongoza kwa kuwa na akiba kubwa ya madini hayo duniani.
Madini ya Lithiam, nikeli na kobalti ndiyo yanayotengeneza betri na mfumo wa umeme kwenye magari na mashine zisizotumia mafuta.
Pamoja nayo pia kinahitajika kiwango kikubwa cha shaba na aliminiamu, huku madini mengine adimu yakitumika kwenye kusuka sumaku zinazosaidia mitambo ya kufua umeme wa upepo.
Madini hayo husakwa kila mahali, mfano mwaka jana India imetangaza harakati za kutafuta madini ya thamani kwenye kina kirefu cha bahari ambayo yanaweza kuwa yenye umuhimu mkubwa kwa mazingira safi na salama duniani, BBC inasema.
Nchi hiyo ambayo tayari ina leseni mbili za utafiti wa kina cha bahari katika Bahari ya Hindi, imetuma maombi ya kupata leseni nyingine huku kukiwa na ongezeko la ushindani kati ya mataifa makubwa kupata madini muhimu ndani ya bahari.
China, Urusi na India zinawania kufikia hifadhi kubwa ya rasilimali za madini yakiwamo kobalti, nikeli, shaba na manganizi ambayo yako chini ya kina kirefu cha bahari.
Madini haya hutumika kuzalisha nishati mbadala kwenye paneli zinazofua umeme jua na upepo, magari ya umeme, simu na vifaa vyote vya kielektroniki na teknolojia zinazohitajika kuachana na nishati chafu kukabili mabadiliko ya tabia nchi, BBC inasema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED