WAJIKI, Polisi wanavyokoleza moto kampeni maalum vita ukatili kijinsia

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:27 PM Dec 19 2024
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi, akiwa katika tukio hilo. 

·
Picha: Sabato Kasika
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi, akiwa katika tukio hilo. ·

VITENDO vya ukatili wa kijinsia ni moja ya changamoto inayoendelea kutesa ndani ya jamii. Katikati ya vitendo hivyo, wapo wadau wanaoendelea kupambana navyo kupitia kampeni maalum.

Baadhi ya wadau ni Shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), linaloendesha kampeni ya 'Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono Inawezekana'.
 
 Wakati WAJIKI wakiendesha kampeni hiyo, Jeshi la Polisi nalo limekuja na kampeni iitwayo 'Tumwambie Kabla Hajaharibiwa'. Kampeni hizo zote zinalenga kukomesha vitendo vya ukatili ndani ya jamii.
 
 Hivi karibuni kwenye maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, wadau hao waliungana kufanya maandamano wakiwa na mabango ya kuelezea madhara ya vitendo hivyo.
 
 Siku ya kwanza, WAJIKI waliungana na Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, kisha siku ya pili wakaungana na Polisi Mkoa wa Kinondoni Dar es Salaam, kuendelea na maadhimisho hayo, huku wakuu wa polisi wa mikoa wakitoa taarifa kuhusu vita hiyo, mafanikio na changamoto zake.
 
 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, ACP Yuston Mgonja, anasema kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu, watu 25 wamehukumiwa kwa makosa mbalimbali, mengi yakiwa ni ya ubakaji.
 
 ACP Mgonja anafafanua kuwa, makosa ya ukatili katika kipindi cha mwaka 2024 yamepungua ikilinganishwa na mwaka jana na kwamba makosa ya ubakaji yako juu kuliko mengine.
 
 "Mwaka jana makosa ya ubakaji yalikuwa 198, mwaka huu ni 77 ingawa bado yako juu kuliko mengine. Makosa ya ulawiti yalikuwa 87 lakini mwaka huu ni 51, makosa kipigo yalikuwa 79, mwaka huu ni 30, makosa ya kutelekeza familia yalikuwa 57, lakini mwaka huu ni 23," anasema.
 
 Kamanda huyo anaongeza kuwa watu 25 wamehukumiwa vifungo vya miaka 30 na wengine. Maisha baada ya kukutwa na makosa mbalimbali, ina mengi ni ya ubakaji na ulawiti.
 
 Wakati Ilala wakifungwa watu 25, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, SACP Mtatiro Kitinkwi, anasema katika mkoa wake kuna watu 25 wametumikia kifungo aina hiyo.
 
 "Taarifa hii ni kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu. Vitendo vya ukatili wa kijinsia vipo, ndio maana tumepata idadi hiyo, hivyo tuendelee kushirikiana katika vita hii," anasema SACP Kitinkwi.
 
 CHANGAMOTO ILIVYO 

 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, ACP Mgonja, anasema pamoja na mafanikio ambayo jeshi hilo limepata kupitia kampeni ya ‘Tumwambie Kabla Hajaharibiwa', bado kuna changamoto zinazotakiwa kutatuliwa.
 
 "Jeshi la Polisi limekuwa likiendesha kampeni kwa kutoa elimu ndani ya jamii kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo husika, shuleni.

“Katika vijiwe vya bodaboda na kwingine, lakini bado kuna watu hawatoi ushirikiano wanapoitwa mahakamani kutoa ushahidi," anasema.
 
 ACP Mgonja anataja kikwazo kingine kuwa ni watu kutofika kwa wakati katika vituo vya polisi kutoa taarifa wanapofanyiwa ukatili na kusababisha ushahidi kuvurugika.
 
 "Changamoto nyingine, ni baadhi ya wazazi na walezi kumalizana na wahalifu vinapotokea vitendo vya ukatili, lakini wanapopishana kiswahili ndipo wanapokuja kutoa taarifa wakati muda umeshapita na kusababisha ukusanyaji wa taarifa kuwa mgumu," anasema.
 
 Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza, anaunga mkono kauli ya kamanda huyo kwa kusema kuwa hata shirika lake katika vita hiyo limekumbana na vikwazo vya kukosa ushirikiano toka kwa jamii.
 
 "Watu wanalalamika watoto wao kufanyiwa ukatili, lakini taarifa za matukio hayo zinapokusanya na kufikishwa polisi na kisha mahakamani, hawafiki kutoa ushahidi," anasema Janeth.

WAJIKI wakiwa katika maadhimisho hayo.
SAFARI SALAMA

Mkurugenzi huyo anasema kwa muda mrefu, WAJIKI imekuwa ikiendesha kampeni ya 'Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono Inawezekana' katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke.
 
Anasema, kampeni hiyo inashirikisha madereva wa bodaboda, bajaji, daladala, viongozi wa serikali za mitaa, manispaa, TAKUKURU, walimu, wanafunzi na jamii, ikilenga kukomesha rushwa ya ngono kwa wanafunzi na wanawake.
 
"Ushirikiano huu na vyombo vya dola ni ishara tosha kuwa vita dhidi ya ukatili wa kijinsia inazidi kupamba moto. Sisi tunapiga vita rushwa ya ngono ambayo kimsingi ni ukatili wa kijinsia," anasema Janeth.
 
Anafafanua kuwa, hivi karibuni walizindua awamu ya sita ya kampeni hiyo eneo la Bunju ‘A’ Dar es Salaam, ili kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu madhara ya rushwa ya ngono itakayofikia wanafunzi 100,000.
 
"Women Fund Tanzania Trust (WFT-T), wametufadhili katika kampeni hii kwa kutupa Sh. milioni 80 ambazo tutazitumia kuokoa afya za Watanzania kwa miaka miwili," anasema.
 
Anafafanua kwamba walishamaliza kampeni katika Kata ya Bunju A na sasa wanaendelea na kata nyingine mpya, walizokuwa hawajazifikia za Kitunda wilayani Ilala na Mbagala Kibonde Maji, wilaya ya Temeke.
 
Anafafanua kuwa katika kampeni yao hiyo inayotarajia kudumu kwa miaka miwili, kila kata watafikia wanafunzi 35,000, walimu 100 na madereva 200 na kuwapa elimu ili wajue umuhimu wa kumlinda mtoto wa kike dhidi ya rushwa ya ngono.
 
Mkurugenzi huyo anaongeza kuwa mbali na kutoa elimu ya kupambana na rushwa ya ngono, wanahamasisha wanawake ili wajiandae kujitokza kwa wingi kuwania uongozi katika uchaguzi wa mwaka 2025.