VIJANA PASUA KICHWA: Hawataki ndoa, familia wala majukumu

By Dk. Felician Kilahama , Nipashe
Published at 11:38 AM Apr 23 2024
Pete ya ndoa.
Picha:Maktaba
Pete ya ndoa.

TANZANIA ya leo inazo changamoto kuhusu hatima za vijana hasa wa kiume kwa maisha ya sasa na baadaye. Majira yanakwenda, nyakati zinapita na miaka kuongezeka lakini mwelekeo wa vijana wengi siyo wenye kuleta faraja kwenye familia nyingi.

Ikumbukwe tangu mwanzo Mungu aliumba mume na mke, mwanaume akiwa mzaliwa wa kwanza akapewa madaraka ya kuisimamia na kuitunza dunia pamoja na familia, mwanamke akiwa msaidizi maandiko yanaeleza.

Lakini mazingira ya sasa, vijana wa kiume,ingawa siyo wote wamepoteza dira na umuhimu wa kulinda urithi, waliopewa tangu kuumbwa dunia, la kushangaza ni kuona wengi walio na umri wa kuoa waishio mijini na vjijini, wanakwepa kuwa na familia, kuoa au kuzaa watoto. Ukiwadadisi wana jibu jepesi: “hali ya maisha siyo rafiki “. Ni vigumu kwa kijana kuwa na familia hivyo wanasema hawatamani kuoa.

Ni mtazamo hasi unaifanya jamii ipoteze mwelekeo sahihi wa kulitii agizo la Muumba akiwaagiza wanadamu nendeni mkazae, mkaongezeke na kuijaza dunia. Sipati picha kamili maana kujitetea kupitia ‘ugumu wa maisha’ chanzo chake nini? 

Ukiwauliza wapi na vipi wanapohakikishiwa kuwa maisha yatakuwa rahisi au mepesi kula , kunywa, kuvinjari, wanavyotaka  bila kutokwa jasho, hawana  jibu lakini wanabaki kulalamikia serikali na hata wazazi na walezi kuwa wanatelekezwa. Wengi malalamiko ni hakuna ajira, fedha imekuwa vigumu kupatikana na hawana msaada kutoka kwa jamii.

Vitabu vinaeleza kuwa “kwa jasho lako utakula chakula” na zaidi kuonywa kuwa “asiyetaka kufanyakazi wakati ni mzima wa afya asile chakula”. Sasa huo urahisi wa maisha unaingiaje kama siyo kujidanganya na kupelekea kupenya kwa ‘roho’ haribifu hatimaye kuukumbatia ‘uovu’ kwa kutaka kujirahisishia maisha? 

 Mwanamume simama kidete fanyakazi kwa bidii ili uitwe baba wa familia na siyo kinyume chake. Kutaka vya urahisi ni kujidhalilisha na kutothaminiwa vizuri na jamii.

Kwa kukwepa wajibu wa msingi ambao unawataka wanaume wafanyekazi kwa malengo maalumu ili kuifanya Tanzania kuwa na familia lakini pia nchi ikawe na watu wa kutosha. Wakumbuke kuwa watu au wananchi ni mtaji muhimu unaohitajika kwa maendeleo ya taifa , bila watu wa kutosha ni kujidanganya na kweli haimo ndani mwetu wakati taifa ni  kubwa na idadi ya watu ni ndogo.

 Ingawa maeneo mengine hayawezi kukaliwa na watu kama sehemu za ardhioevu, zenye maji na hifadhi za wanyama na misitu,  bado idadi ya watu ni ndogo. 

Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi  ya 2022 zinaonyesha kuwa idadi ya watu kwa kilometa moja ya mraba (km2) ina wastani wa wakazi  68 . Hata hivyo ipo mikoa ambayo watu ni kidogo kama Katavi wapo  25 kwa km2 au Lindi 18 wakati  Ruvuma ni watu 29 kwa  km2 moja.

Wakati huo Tanzania Bara inatarajiwa kufikia watu milioni  147 mwaka 2050, kutoka millioni  61 walioko sasa sawa na ongezeko la takribani asilimia 3.2 kwa mwaka. Kwa mwelekeo huo wa vijana kukataa ndoa na kuwa na familia na baadhi kujiingiza kwenye ushoga na usagaji, idadi hiyo itatoka wapi? Labda wahamiaji kutoka nje.

Pamoja na hayo, vijana wa kiume wamekuwa wepesi kukiuka misingi ua ubaba kupitia familia ya mume na mke kuishi pamoja na kuwa na watoto. Unajiuliza kijana mwenye afya njema anachangamkia ushoga na kuona fahari akitangazwa kuwa ni ‘shoga’ mtaani?

 Inawezekana akafanya hivyo kwa tamaa ya kupata fedha haraka kwa kurubuniwa na wenye nia mbaya na kwa kukosa maarifa ya Ki-Mungu anatumbukia kirahisi kwenye mtego wa aina hiyo, lakini mapato ya aina hiyo yana faida gani iwapo hutakuwa na familia?
 Vijana wamjue  Mungu ipasavyo bila shuruti maana kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa ambayo ndiyo hazina ya mafanikio  laa sivyo  wengi watajiangamiza kama neno la Mungu linavyoonya: “watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”.

Vijana kumbukeni kukumbatia ‘ushoga’ ni kutumbukia kwenye dimbwi lililo chukizo kwa muumba wako. Vilevile, ni kuwa na mioyo iliyosheheni mawazo mabaya na kujivika miguu iliyo miepesi kukimbilia dhambi.

Wafahamu kuwa  kutumbukia kwenye maovu kama ushoga na kwa kisingizio cha haki za binadamu ni sawa na kukosa maarifa hali inayopelekea maumivu makubwa kwa wazazi na jamii kwa ujumla.  Wazazi na walezi wanaposikia au kumshuhudia kijana waliompata akiwa zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ghafla anageuka kuwa mwovu au shoga ni hali tatanishi na isiyohimilika  kwao.

Vijana wa kiume na wa kike, jiulizeni ushoga na usagaji  una faida kwenu, wazazi, walezi ,jamii na taifa kwa ujumla? Je, mnavutiwa va vitu au vionjo gani mpaka kupagawa kiasi cha kutojali uhalisia wa maumbile yenu? Umezaliwa ni mwanamume iweje uwe na matamanio ya kumuoa mwanamume mwenzako? Kwa vipi uone fahari na kujisifu kuwa umeolewa na mwanamume mwenzako na kujiona ni mke wake? 

Binti naye anageuka kuwa mwanamume eti anamuoa binti mwenzake je uhalali huo unatokana na nini? Hakuna cha haki za binadanu wala chochote kile ni uovu uliokithiri mbele za Mungu na aibu kubwa kwenye jamii .

Kwa hili viongozi wa kiroho wa madhehebu mbalimbali simameni imara na kukemea kwa nguvu zote na dunia ielewe kuwa hatuko tayari kukumbatia uovu kwa minajili ya kutaka kufurahisha watu wengine. 

Vijana wengi wanalia kuwa hali ya uchumi na maisha ni magumu na ajira ni kidogo kulingana na mahitaji, kazi za kujituma hata kama ni kulima au kazi nyinginezo za kumpatia kijana kipato zinapuuzwa kwa kutaka kupata fedha kirahisi wakati kwa jasho letu; tunapaswa kupata riziki zetu za kila siku. 

Inapotokea uovu ukakithiri kwenye jamii milango ya baraka inafungwa. Hatuwezi kumlaumu Mungu kwa sababu tunajiangamiza kwa kukosa maarifa. Tunaivuruga misingi ya asili ya kutuwezasha kupata huruma ya Mungu na kuyafaidi mema ya nchi kwa kukumbatia maovu na kusababisha machukizo kwa Mungu  aliye na hatimiliki ya maisha yetu.