Udanganyifu, utoro, matusi katika mitihani vimezidi, ufumbuzi uje!

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:20 AM Jan 31 2025
Katuni
Mchoro: Muhidin Msamba
Katuni

HIVI karibuni, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) lilitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne. Tukaambiwa , huku matokeo ya wanafunzi 67 wakiwamo watano walioandika matusi yakifutwa.

Matokeo hayo ni ya mtihani uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, kukiwapo idadi hiyo ya wanafunzi waliofutiwa matokeo yao kwa vitendo hivyo, ambavyo ni kinyume na utaratibu.
 
 Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Said Mohammed, anasema wanafunzi hao walioandika matusi ni tatizo la maadili na kwamba matusi hayakubaliki katika chumba cha mtihani na kila mahali.
 
 Udanganyifu na kuandika matusi, ni kama vinatakiwa kuwa vya kawaida, kwani matokeo ya mtihani wa kidato hicho ya mwaka 2023, wanafunzi 102 walifutiwa kwa udanganyifu, watano kwa matusi.
 
 Inatia mashaka kwamba nchi inaandaa wasomi wa aina gani kama wapo wanaotafuta kufaulu kwa udanganyifu huku wengine wakipoteza muda shuleni kujiandaa kuandika matusi kwenye karatasi za mitihani.
 
 Yaani mwanafunzi anagharimiwa na wazazi au walezi ili apate elimu, lakini mwisho wa siku anaandika matusi katika katarasi za mitihani! Kama hapendi shule kwanini asikae tu nyumbani?
 
 Mwanafunzi akishaingia sekondari anatarajiwa kuwa ni mtu ambaye ameanza kujitambua na kujua kile anachokifanya shuleni, lakini inasikitisha kuona bado wapo ambao hawajitambui hadi kupoteza muda wa miaka minne shuleni kwa maandalizi ya kuandika matusi.
 
 Kama anavyosema Katibu Mkuu wa NECTA, hilo ni tatizo la maadili ambalo binafsi ninaamini linaanzia nyumbani, hasa kutokana na ukweli kwamba shule ya kwanza ya mwanafunzi ni wazazi au walezi.
 
 Inawezekana hao wanaoandika matusi katika mitihani, ni wale ambao wazazi hawafuatilii maendeleo yao shuleni na hivyo wanakuwa huru kuhudhuria masomo shuleni au kushinda vijiweni.
 
 Iwapo hakuna ufuatiliaji, ni rahisi wanafunzi kujiingiza katika makundi yasiyofaa na kujikuta wakiacha shule. Kwa mtindo huo, wanaweza kufika shuleni kuripoti kisha wakatoroka kwenda vijiweni.
 
 Ninaamini mwanafunzi anayejitambua na anayejua kwa nini yupo shule, hawezi kusubiri kuandika matusi katika mitihani, badala yake anaelekeza nguvu katika masomo ili kwenye mitihani afanye vizuri.
 
 Pamoja na hayo ya wanafunzi wanaoandika matusi, wale ambao wamekuwa wakisubiri kufanya udanganyifu ili wafaulu, wanajiandaa kuwa wasomi wasio na faida kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla.
 
 Ingefaa, kila mwanafunzi atumie maarifa aliyopewa shuleni kwa muda wote wa miaka minne au sita kufanya mtihani badala ya kusubiri kufanya udanganyifu kwa lengo la kufaulu.
 
 Sidhani kama ufaulu wa aina hiyo unaweza kuwa manufaa, kwani huku mbele anakokwenda anaweza kukosa msaada kwa udanganyifu na kujikuta akikwama kuendelea na elimu ya juu.
 
 Hivyo, njia nzuri ya mwanafunzi kufaulu, ni kutumia maarifa ambayo amepewa na walimu wake ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufaulu. Kufaulu kwa njia ya mkato, daima haina matokeo mazuri mbele.
 
 Wakati kukiwapo changamoto hizo mbili za udanganyifu na kuandika matusi, ipo nyingine ya tatu katika elimu ambayo ni utoro unaofanywa na wanafunzi wa kidato cha kwanza kila mwaka.
 
 Imekuwa ni kawaida kila mwaka wa masomo unapoanza, huwa kuna utoro mkubwa wa wanafunzi hao maeneo mbalimbali nchini, kitendo ambacho ni hatari kwa maendeleo ya elimu.
 
 Kama ilivyo kwenye mitihani ya taifa kwa kuandika matusi au kufanya udanganyifu kila mwaka, ndivyo ilivyo kila mwaka kwa kidato cha kwanza kufanya utoro hadi serikali kuwasaka majumbani.
 
 Mfano mmojawapo ni wa hivi karibuni ilipoelezwa kuwa wanafunzi zaidi ya 5,000 wa kidato cha kwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini mkoani Mara, walikuwa hawajaripoti katika shule walizopangiwa tangu zifunguliwe Januari 13 mwaka huu.
 
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Simion Langoi, anasema hayo katika kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Madiwani, kilichojadili bajeti ya halmashauri kwa mwaka wa  fedha 2025/2026.
 
 Inaelezwa kuwa wanafunzi 6,313 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika halmashauri hiyo, ni 1,233 pekee walioripoti shule walizopangiwa, huku wengine 5,080 wakiwa hawajulikani walipo.
 
 Hiyo ni halmashauri moja tu, ukifanyika uchunguzi, ninaamini watoro wanaweza kuwa wengi zaidi, kwani imekuwa ni kawaida viongozi wa serikali sehemu mbalimbali nchini kufanya msako wa wanafunzi watoro kila mwaka na kuwarejesha shuleni.
 
 Kwa kuwa matatizo hayo hujirudia kila mwaka, ninadhani ni wakati sasa umefika kwa serikali na wadau wake wa elimu kukaa pamoja na kuweka mikakati ya kuyamaliza ili kusaidia kuandaa vizuri taifa la kesho.
 
 Ni kweli kuna jitihada mbalimbali ambazo serikali imekuwa ikifanya ikiwamo kufanya msako na kuwakamata wanafunzi watoro au wazazi wao, lakini tatizo linajirudia kila mwaka, hali ambayo inaonesha kuna haja ya kuja na mbinu nyingine zaidi zitakazokuwa na matokeo chanya.