Tanzania kuanzisha vituo 2 vikuu vya tiba kinywa Afrika Mashariki

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 09:32 AM May 09 2024
Tiba ya kinywa.
Picha: Mtandaoni
Tiba ya kinywa.

WAKATI kuna juhudi za maboresho kitaalamu, miundombinu na vifaa vikiendelea kuboresha afya nchini, Waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu, anatambulisha wana hatua mpya kiserikali kwa Baraza la Mawaziri wa Kisekta ya Afya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika hilo, anasema kuna maombi ya Tanzania kuanzisha vituo viwili vya umahiri kwa Afrika Mashariki vitakavyohudumia afya ya kinywa na meno, pia upandikizaji uloto. 

Waziri Ummy ameyasema hayo, kwenye Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta wa Afya wa EAC, uliofanyika mjini Dar ss Salaam, pia ukiwakutanisha makatibu wakuu na manaibu wa wazira husika, kutoka nchi tano za Afrika Mashariki. 

“Chuo Kikuu cha Muhimbili kupitia Idara ya Kinywa na Meno, ina wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa. Kwa hiyo, tunataka wataalamu wote wa kinywa na meno wa Afrika Mashariki waje Tanzania kujifunza katika taasisi yetu ya MUHAS,” anafafanua.

Anasema, hadi sasa Tanzania inafanya vizuri katika masuala ya upandikizaji viungo, ikiwamo upandikizaji wa uloto hususan kwa watoto wenye changamoto za sikoseli.

Nchini kunatajwa  ni kati mataifa matano duniani, yenye idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na shida ya sikoseli. 

Anasema, Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH), jijini Dodoma, imeshafanya upandikizaji wa uloto kwa watoto 10 wenye tatizo hilo la sikoseli na kati yao, watoto sita wakathibitika kupona ugonjwa huo wa sikoseli. 

Waziri Ummy anasema, katika mkutano huo wakaujadili magonjwa ya kuambukiza, Afrika Mashariki kukikabiliwa na changamoto za magonjwa ya malaria, Ukimwi na kifua kikuu. 

“Tumeona ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza. Tumeona sasa ipo haja kama Mawaziri wa Afya wa Afrika Mashariki, tuweze kuweka mikakati ya kupambana na magonjwa hayo, ikiwamo kuhamasisha na kuelimisha umuhimu wa kufanya mazoezi,” anahitimisha Ummy.

Anasema, siri kubwa ya kuepuka magonjwa hayo ni kuzingatia ulaji wa vyakula, kupunguza unywaji wa pombe na ufanyaji wa mazoezi, kwa Tanzania kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi imetengwa kuwa ni muda wa mazoezi ambapo Waziri Mkuu alitoa agizo la kufungwa na Daraja la Tanzanite kwa muda huo ili kuwapa uhuru watu wanaofanya mazoezi. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Kenya,  Mary Muthoni, anasema jamii inapaswa kuelimisha juu ya afya kwa kuwa afya inaanzia nyumbani, “usipokata vichaka shida inaanzia nyumbani, usipokula vizuri shida inaanza nyumbani, usipoweka maji safi na salama shida inaanzia nyumbani.

Akizungumza madaktari 1,109 kunufaika na ufadhili wa Rais Samia Suluhu Hassan katika ufadhili wa masomo.

 Waziri Ummy anasema kuwa,Dk. Samia Super-Specialized scholarship Programme imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi ambapo kwa mwaka wa masomo 2023/2024, jumla ya Shilingi 10.9 bilioni zimetengwa na kuwawezesha wanafunzi 1,109 kwenye masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi. 

Waziri Ummy anayasema hayo,wakati akifungua mkutano wa Mwaka wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani Tanzania (APHYTA) uliofanyika katika ukumbi wa Kinataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam. 

“Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa madaktari bingwa katika kuwaendeleza kitaaluma kupitia programu ambayo imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa kwa mwaka wa masomo 2023/2024, kwa wanafunzi 1,109 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 582 ukilinganisha na mwaka wa masomo 2022/2023,” anasema.

 Anaongeza kuwa katika idadi ya wanafunzi wote ambao wamepata ufadhili kupitia programu hiyo, wanafunzi 79 watasomea udaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na kati yao madaktari 11 sawa na asilimia 33 wamekwenda kusoma ubingwa bobezi wa magonjwa ya ndani.

 Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa madaktari vijana kujitokeza kwa wingi kwenda kujiendeleza katika masomo ya ubingwa bobezi hususan kwenye magonjwa ya ndani na wakirudi wakubali kupangiwa sehemu yoyote kwa kuwa mikoa mingine pia inahitaji madaktari bingwa wabobezi. 

 “Kupitia muundo huu mpya wa Sekta ya Afya, tutaweza kuwatambua kwa kuwawekea mazingira mazuri madaktari wenye ubobezi katika maeneo mbalimbali ikiwemo wa masuala ya magonjwa ya ndani,” anasema.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewataka madaktari hao kujadiliana na kuja na mapendekezo ya jinsi ya kupunguza magonjwa Yasiyoambukiza kwa kuwa kwa sasa kumekuana ongezeko kubwa la magonjwa hayo. 

Pia, Waziri Ummy amewataka madaktari hao kujadiliana na kutoa maoni yao katika mwongozo wa kitaifa wa matibabu pamoja na orodha ya Taifa ya dawa ili  kama kuna mapungufu yaweze kurekebishwa. 

“Suala la kitita cha Bima ya Afya NHIF linatakiwa lijadiliwe kuanzia kwenye mwongozo wa kitaifa wa matibabu pamoja na orodha ya Taifa ya dawa, tukishakbaliana tunamwambia NHIF atambue na afuate mabadiliko hayo.” anasema.