2025 ni mwaka wa uchaguzi wa madiwani, wabunge na marais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar. Ni msimu ambao utashuhudia wimbi la wengi kuanzia watumishi wa umma, wanataaluma na wafanyabiashara, wakijitosa kwenye harakati hizo.
Baadhi ya watumishi wa umma, wateule wa Rais, wanaonekana hawaridhiki na nafasi walizokabidhiwa wanataka pia wakawanie ubunge, ambao unawaweka kwenye nafasi nyingine za uteuzi, hususan uwaziri au unaibu, ukuu wa mikoa na ujumbe wa bodi.
NI KIPI KIVUTIO?
Zipo sababu nyingi zinazowafanya watumishi wa umma na wanataaluma kukimbilia kwenye ubunge, ikiwamo kuporomoka hadhi ya utumishi wa umma, kazi za kitaaluma maslahi madogo na hata hofu ya kutumbuliwa.
Pia kuchukuliwa kama njia rahisi ya kufikia mafanikio, uwanja wa kutoa michango ya kisiasa, uhaba wa mifumo ya taasisi huru na kutafuta fursa za kuteuliwa.
Wanaotamani ubunge si watumishi wa umma pekee wakiwamo wateule wa Rais, bali hata wanataaluma, wafanyakazi wa sekta binafsi na wafanyabiashara wanakimbilia ubunge.
Maslahi yatokanayo na ubunge ni jambo linalovutia wengi, siasa ikichukuliwa kuwa ni eneo linalolipa zaidi au lenye maslahi manono mno.
Takwimu zinaonyesha kuwa mbunge analipwa mshahara mnono kila mwezi, anapata posho kubwa ya kila kikao, akiongezewa na posho ya kujikimu kila siku achilia mbali safari, vikao vya kamati na kazi nyingine nyingi.
Anakusanya malipo hayo kwenye vikao vyote na kikubwa zaidi ni cha bajeti kinachoanza Aprili hadi Julai.
Ni heri kwake maana baada ya miaka mitano ya ubunge anapokea pensheni nono.
Mtu akichaguliwa kuwa mbunge anapata bima ya afya daraja la kwanza na familia yake, pia wana safari za nje lakini pia hana makato.
Maprofesa wanalipwa takribani Sh. 6,000,000 kwa mwezi lakini hawawafikii pensheni hiyo.
Kazi hiyo wanaweza kuifanya kwa miaka 30 lakini kuambulia pensheni wanayopata wabunge si jambo rahisi.
Pili, ni suala la demokrasia kila raia ana haki sawa kushiriki michakato ya kidemokrasia wakilindwa na katiba ya nchi inayosema kila mwananchi anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa kwa mujibu wa ibara ya 21 (1) na (2).
Jambo la tatu, wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema, baadhi ya watiania wanapenda kuona mabadiliko ya kweli yanatokea nchini, ikitafsiriwa kukata tamaa pamoja na kuamua kushughulikia matatizo ya nchi kwa vitendo badala ya kusubiri wanasiasa pekee kila awamu.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema, ubunge ni ajira ya uhakika, ingawa ni kwa miaka mitano.
Nafasi za kuteuliwa si za kudumu na zinategemea mamlaka za uteuzi, kwani kuenguliwa ni kawaida, hivyo wengi wanaoteuliwa hawana uhakika na nafasi hizo kesho, ukiacha wale wanataaluma ambao wanatafuta maslahi.
Mbunge wa kuchaguliwa jimboni hawajibishwi na yeyote iwe amekaa kimya au kuzungumza bungeni, haiwezekani kutumbuliwa, labda baada ya miaka mitano mambo yamwendee kombo.
Mwalimu mkuu akipoboronga kwenye mitihani miaka miwili, anaweza kuhamishwa kwa adhabu kwenda vijijini.
Hakuna atakayemjali akihamishiwa mazingira mabaya, kadhalika halmashauri ikiboronga kwenye makusanyo ya maduhuli (mauzo na mapato), mhasibu au mkurugenzi anaweza kushushwa cheo hata kuhamishwa au kutimuliwa.
Mtu kama huyo anapopata nafasi ya kuwania ubunge anaona bora aende huko.
RUSHWA INAJIPENYEZA
Kwa kutambua 'vibunda vinono' kwenye ubunge, wengine huanza mapema kujisafishia njia wakitengeneza mazingira kwa wananchi, hususan wanachama wa vyama vya siasa.
Mathalani zipo taarifa kwamba, licha ya kwamba muda wa kampeni bado, wapo watu wanaoendelea na harakati za kujipenyeza majimboni.
Watiania wengi, kwa kutambua kwamba ubunge ni ajira na ina mapato makubwa, baadhi wako tayari kutumia fedha nyingi kwa kuwahonga wajumbe ili kupata nafasi hizo muhimu.
Kuna malalamiko kutoka mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara, aliyedai kuna kigogo anazurura jimboni akitumia gari la serikali na kugawa rushwa kwa baadhi ya walengwa hususan wahusika vikao vya maamuzi.
Waitara anamtuhumu kuwa amekimbia ofisi yake na kuhamia jimboni kuwarubuni wajumbe ili kumpigia kura za maoni akiwapa fulana, kofia na 10,000 au 20,000.
Mbunge huyo anayataja maeneo kigogo huyo anayodaiwa kugawa posho, akisema atawataja hadharani waliopokea rushwa na maeneo yaliyotumika.
Anamtuhumu kigogo huyo bila kumtaja kwamba ameacha ofisi ya umma na kukimbilia jimboni kugawa takrima ili kununua wajumbe.
Aidha, anamtishia kuwa hatamvumilia na kuwatuma washirika wake kumfikishia salamu.
"...Huu ndio mgawanyo wa madaraka, mwingine atakuwa mtumishi wa umma, mwingine mfanyabiashara, atakuwapo pia mwanasiasa. Mimi siasa ni kazi yangu. Kama kuna mtu ataacha nyumba yake na kugawa tisheti, kofia na elfu 10...”
"Desemba 27, 2024 walikuwa wanagawana hela Sirari. Najua. Wakatoka hapo wakaenda kugawa Nyang'ungu na Gogona pale Masanga, ishirini ishirini kwenye bahasha. Desemba 26, waliitwa watu wa Ganyange, Binagi, wakaitwa watu wa Nyakonga, walienda polisi wakagawana 30,000 thelathini."
Anaongeza: “Nataka niwaambie. Mimi siyo mjinga, siwezi kusafisha nyumba aje mtu arukeruke hapa, ama zako ama zangu. Tutagawana mbao, nawaambia. Wale wote ambao walipokea rushwa nitawataja hadharani. Na shughuli hii imeanza.”
Anasisitiza kuwa mtumishi huyo abake ofisini kwake ache kutangatanga, abaki njia kuu.
“Hivi una ofisi yako uiache, unakuja na gari ya serikali unazurura jimboni unagawa rushwa. Sasa nilitarajia asimame hapa wote awape hela, si anagawa hela? Kwa hiyo apate taarifa..."
TAKUKURU IINGIE
Kwa muktadha huo, wengi wanaishauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikaingia mitaani kuwashughulikia wanaomwaga fedha kusaka ubunge na udiwani.
Na kwa kuanzia iwe Jimbo la Tarime Vijijini ambalo tayari kumeshatajwa kuwapo kwa vitendo hivyo vya rushwa.
Suala hapa si tu kumfuatilia kigogo anayemwaga fedha, lakini hata wengine pia, akiwamo mbunge mwenyewe, kwani naye ni mmoja wa watu wanaowania jimbo hilo.
Malalamiko hayo siyo za kuomba 'huruma' kutoka kwa mamlaka lakini zinaweza pia kuwa ni za kuzidiwa kete katika kugawa mlungula.
Hili la Tarime Vijijini liwe mwanzo kwa TAKUKURU kufanya ufuatiliaji majimboni na kata kukomesha rushwa na kuepusha jamii kuchagua viongozi wasio waadilifu ambao hawawezi kuleta maendeleo kwani watakuwa wanatafuta fursa ya kurejesha fedha zao na kuchuma nyingine.
TAKUKURU ina ofisi kila kona kwa hiyo siyo kazi ngumu kufanya ufuatiliaji ikiwa tu maofisa wataacha ‘kukaa ofisini kula kiyoyozi'.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED