SIGARA NI KITANZI: Watafiti wanakupakulia mapya, ukivuta 3 umekata saa 1 ya umri wako

By Restuta James , Nipashe
Published at 08:06 AM Jan 14 2025

Kuvuta sigara kunatajwa kuwa ni kama  kujinyonga kwa sababu muda wote inapunguza maisha.
PICHA: MTANDAO
Kuvuta sigara kunatajwa kuwa ni kama kujinyonga kwa sababu muda wote inapunguza maisha.

WAKATI madaktari bingwa wa magonjwa yasiyoambukizwa wakionya kuhusu athari za matumizi ya tumbaku, utafiti mpya umebaini kwamba sigara moja inayovutwa, inapunguza dakika 20 za maisha ya anayevuta.

Aidha, wanawake wanapoteza dakika 22 za kuishi kwa kila sigara moja wanayovuta, wakati wanaume wanapoteza umri huo kwa dakika 17.

Maradhi yasiyoambukiza ni pamoja na saratani, mfumo wa hewa, kisukari na shinikizo la juu la damu na figo. 

Utafiti huo umechapishwa kwenye jarida la Addiction hivi karibuni unaonesha kwamba kama mtu anavuta pakiti ya sigara 20 kwa siku, anapoteza karibu saa saba za maisha kwa kila pakiti.

Mtafiti Mkuu na Mwandishi Mkuu wa Utafiti huo, Dk. Sarah Jackson, anasema uamuzi wa kuacha sigara na aina yoyote ya tumbaku ni muafaka ili kuokoa uhai na kupunguza mzigo wa magonjwa yanayozuilika.

Dk. Sarah anasema kwenye utafiti huo kwamba wakati watumiaji wa tumbaku wanapoteza umri wa kuishi, wanaongeza mzigo kwa wapendwa wao ambao watalazimika kuwauguza wanapopata maradhi ya saratani, kisukari, shinikizo la damu na athari za mfumo wa hewa.

"Hii ni kwa sababu katika kipindi cha baadaye cha maisha yako watumiaji wa tumbaku huelekea kuishi katika afya mbaya zaidi,” anaonya.

Utafiti huo, ambao umeidhinishwa na Idara ya Afya ya Jamii ya Uingereza, unajumuisha takwimu za vifo zilizotolewa na utafiti wa madaktari wa Uingereza ambao ulionyesha kuwa kwa wastani, watu waliovuta sigara katika maisha yao yote wanapoteza karibu miaka 10 ya maisha ikilinganishwa na watu ambao hawakuvuta sigara.

Wakati takwimu zikiwa hivyo Uingereza,  huko Marekani hali ni hiyo hiyo kwani watumiaji wa tumbaku wanapunguza umri wa kuishi kwa miaka 10 ikilinganishwa na wasioitumia, kwa mujibu wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.

Kwa ujumla, utafiti huo wa Uingereza unaonyesha kuwa madhara yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku ni mengi na mabaya.

Hata hivyo, Dk. Sarah anasema pamoja na kwamba ni vigumu kurejesha umri ambao umeshapotea, anashauri watumiaji waache.

"Tafiti zimeonyesha kuwa watu ambao waliacha wakiwa na umri mdogo kwenye miaka 20-30, wana kuwa umri wa kuishi sawa na watu ambao hawajawahi kuvuta sigara. 

Lakini kadiri unavyozeeka, hatua kwa hatua unapoteza zaidi umri wako, lakini hata uwe na umri gani unapoacha, sikuzote utakuwa na muda mrefu wa kuishi kuliko kama ungeendelea kuvuta sigara. 

Kwa hiyo, kwa kweli, ingawa hubadili maisha yaliyopotea tayari, unazuia upotevu zaidi wa muda wa kuishi.”

Katika utafiti huo, Dk. Sarah na wenzake, wanaeleza kuwa kwa mtu aliyekuwa anavuta sigara 10 kwa siku ambaye ameacha kutumia kwa siku nane, anaweza kurejesha siku moja ya maisha yake iliyokuwa imepotea.

“Kama umeacha tangu Januari Mosi, kufikia Februari 08, mwaka huu, unaweza kurejesha umri wa kuishi kwa wiki nzima na mwezi mzima kufikia Agosti 05, mwaka huu kama utaacha kwa mwaka huu wote, utajirejeshea siku 50,” anasema.

"Kuacha kuvuta sigara na matumizi yote ya tumbaku ni jambo bora zaidi unaweza kulifanya kwa ajili ya afya yako. Mara tu unapoacha kuvuta sigara utaishi muda mrefu," anasema Dk. Sarah.

Aidha, ingawa viwango vya uvutaji sigara vimekuwa vikipungua tangu miaka ya 1960, matumizi ya tumbaku yanatajwa kuwa sababu kuu ya magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika. Mathalani, nchini Marekani matumizi ya tumbaku huua zaidi ya Wamarekani 480,000 kila mwaka. 

Utafiti tofauti, uliochapishwa mwaka jana katika jarida la Nature, uligundua kuwa uvutaji sigara unaweza kuwa na athari za muda mfupi na za muda mrefu kwenye mfumo wa kinga ya mtu, na kuwaacha katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa kama saratani. 

Mwandishi mwenza wa utafiti huo, Dk. Darragh Duffy, anasema wavuta sigara walioacha walionesha hatua moja ya mabadiliko katika mfumo wa kinga.

"Habari njema ni kwamba, walau kuna mabadiliko kwenye kinga. Si wakati mzuri wa kuanza kuvuta sigara, lakini ikiwa wewe ni mvutaji sigara, wakati mzuri wa kuacha ni sasa," anasema.

Wakati utafiti ukibaini namna matumizi ya tumbaku yanavyopunguza umri wa kuishi, watengenezaji wa bidhaa hizo wameongeza vionjo vya ladha za matunda ili kuwapumbaza watumiaji hasa vijana ili wafurahie kutumia bila kupima madhara makubwa ya kiafya.

Mara kadhaa, wanaharakati na madaktari bingwa nchini wameonya kwamba kwa hali ya matumizi ya shisha, sigara za kielektroniki na aina nyingine za tumbaku, miaka michache ijayo Tanzania itakuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa moyo na saratani wenye umri mdogo.

Bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Mwanaada Kilima, mara kadhaa anasema asilimia 90 ya saratani ya mapafu na koo inatokana na matumizi ya tumbaku wakati bidhaa hizo zikichangia asilimia 40 ya aina nyingine ya saratani.

 “Nimeona madhara mengi na makubwa sana…matumizi ya tumbaku ya aina yoyote ile iwe ya kusokota, kumung’unya, sigara au za kielektroniki ni majanga,” anasema.

Mbali ya saratani, madaktari wanaeleza kuwa mtu anapovuta sigara, ndani ya saa moja presha yake na mapigo ya moyo yanapanda kwa kasi na athari ya hali hiyo ni shinikizo la juu la damu, mishipa ya fahamu, ubongo na hata kupata kiharusi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chama cha Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Tanzania (TTCF), Lutgard Kagaruki, anasema athari za matumizi ya tumbaku zinajulikana kutokana na kusababisha maradhi ya saratani, moyo, kisukari na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa huku watumiaji wakifariki mapema kabla ya umri wao.

“Tunajua tumbaku inaua kuanzia ya msokoto ya shambani, kufunga kwenye karatasi, ya kiwandani, sigara kielektroniki na shisha. Zote hizi ni tumbaku na zinapunguza umri wa kuishi na kusababisha mzigo kwa familia na jamii kutokana na maradhi yanayowapata watumiaji,” anasema Kagaruki.

Anasema viungo vinavyowekwa kwenye tumbaku vimesababisha madhara ya muda mfupi na mrefu, ikiwamo kifua kubana na mwisho kupata saratani ya mapafu na mishipa ya damu kuvimba.

Anaonya kwamba wakati matumizi ya tumbaku yakipungua katika baadhi ya nchi, hali ni tofauti nchini kwani yanaongezeka yakiwaathiri zaidi vijana kutokana na watengenezaji kuongeza vionjo vya ladha hasa kwenye shisha.

“Kama hakuna hatua madhubuti zitakazochukuliwa, miaka mitano au 10 ijayo, kwa kiwango ambacho vijana wanavuta shisha na sigara za kielektroniki, Ocean Road, Muhimbili na hospitali nyingine kwenye kliniki za kisukari hakutatosha. Tuna vijana ambao wanaelekea kupata uraibu kutokana na matumizi holela ya shisha,” anasema.

Anaongeza: “Ukikaa karibu na wanaovuta shisha ndani ya saa moja hata kama hutumii, ni sawa na umevuta vipisi 100 vya sigara. Anayetumia shisha ni sawa na amevuta sigara 200.”

Anasema imethibitika kwamba tumbaku inasababisha magonjwa mengi yanayozuilika ikiwamo afya ya akili na uraibu wa dawa za kulevya.

“Kuna ongezeko la vifo vya vijana kutokana na magonjwa ya figo, mapafu, shinikizo la damu, saratani, kisukari, magonjwa ya fahamu na afya ya akili. Kama nchi tunaelekea sehemu mbaya sana kwa sababu nguvu kazi ya taifa inapotea. Vijana wanavuta sigara na wanatumia pombe kali,” anasema Kagaruki.

Anaishauri serikali itunge sheria kali kudhibiti matumizi ya tumbaku na kupiga marufuku kuvutaa shisha.