"MARA ya kwanza tulipoonana alinisalimia. Aliambia ananitambua kutokana na mapicha yangu. Mwanamke mzuri kama malaika, anavyotembea ni kama nguva ndani ya bahari. Tafadhali nielezee kwenu wapi.
Akasema anatoka Afrika ya Mashariki, nyumbani kwao Tanga. Usiumize Kabibi. Anania wangu yuko Dar. Sikia tabu niliyopata. Kamanga wangu Manzese."
Ni baadhi ya mashairi yaliyomo kwenye wimbo wa mwanamuziki maarufu barani Afrika, Sam Mangwana, uliotoka mwanzoni mwa miaka ya 1980, uitwao 'Kabibi.'
Katika wimbo huo anawata Mwanamuziki ambaye pamoja na kuwa ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, aliuimba kwa kiswahili kizuri sana.
Hapo kuna maneno anasema Anania wake yupo Dar, na Kamanga wake Manzese.
Kuna mashabiki wengi wa muziki wanapata tabu sana wakisikia maneno hayo na hawajui kwa nini Mangwana aliimba hivyo. Hao ni marafiki zake, washkaji au wafadhili wake, ambao humpa kampani kila anapokuja nchini Tanzania.
Ambalo mashabiki wengi wa Bongo hawajui ni kwamba huyu jamaa aliishi kwa muda fulani Tanzania, hasa jijini Dar es Salaam mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1980.
Akiwa nchini alikuwa anaishi maeneo ya Manzese Midizini kwa rafiki yake huyo Kamanga. Na hata kila alipokuwa akija nchini alifikia hapo hata akirudi leo, Mangwana humpotezi mitaa ya Manzese, anaijua vilivyo. Labda tu anaweza kushangaa kwa jinsi ilivyojengeka tofauti na alivyoondoka.
Hebu tuwafahamu marafiki hao wa Mangwana aliowaimba kwenye wimbo wa 'Kabibi' ni kina nani Kamanga alikuwa mmoja wa wafanyabiashara maarufu nchini, na mwingine alikuwa ni Anania Sangula aliyewahi kuwa mcheza soka kwenye klabu ya Simba miaka ya 1970, kabla ya kuwa mfanyakazi kwenye kiwanda cha bia wakati huo.
Kutokana na urafiki wao mkubwa na ukarimu wa hali ya juu waliokuwa wakimfanyia kila alipokuwa akija mchini, akawatunuku kwa kuwataja kwenye wimbo wa 'Kabibi.'
Pia si wengi wanaojua kuwa alishawahi kupigia bendi za Maquiz du Zaire na Vijana Jazz Band.
Nyimbo za 'Mary Maria', 'Tambiko la Pambamoto', na 'Bujumbura' ambazo zilitungwa na hayati Hemed Maneti, kwa kiasi kikubwa zilichangiwa na Mangwana kwenye utengenezaji wake hadi zikakaa sawa.
Ndiyo maana ukichunguza nyimbo hizo, uimbaji wake na upigaji, ni tofauti na nyimbo za Vijana Jazz zilizopita kabla ya albamu hiyo.
Umaarufu wa Mangwana ulianza tangu mwanzoni mwa 1970, na ukitaka kujua kuwa ni mwanamuziki mkubwa amezipigia bendi zote kubwa nchini DR Congo, za TP OK Jazz chini ya hayati Luambo Luanzo Makiadi Franco, na Afrisa International, chini ya hayati Tabu Ley Rochereau. Hadi leo yupo hai na anaendelea na muziki.
Huyu jamaa ni Mkongomani aliyezaliwa jijini Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ingawa wazazi wake hawakuwa Wakongomani. Baba yake alikuwa ni Mzimbabwe na mama yake alikuwa raia wa Angola.
Ni mmoja wa wanamuziki wachache wanaojua lugha nyingi mno. Akiimba Kiswahili unaweza ukadhani amezaliwa Dar.
Tatizo la Mangwana ni mwanamuziki asiyetulia. Huwa hakai bendi moja. Alikaa muda mfupi kwenye bendi zote mbili kama mwanamuziki mualikwa na akaondoka zake nchini Kenya, akakaa kidogo, akaenda zake Ulaya na kwa sasa anafanya shughuli zake kwenye nchi za Ufaransa na Ubelgiji.
Tuma meseji 0716 350534
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED