MKAKATI KUUFUATA UMMA ULIKO; Anakokanyaga Samia kukabili shida afya akili

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:00 AM Jan 23 2025
Wataalamu wakiwa pamoja kwenye kliniki ya afya ya akili, Hospitali ya Rufani ya Mkoa Temeke, Dar es Salaam. Picha nyingine, Siku ya Afya ya Akili ilivyoadhimishwa kliniki hapo, kwa shughuli za usafi wa mazingira
Picha zote: Mtandao
Wataalamu wakiwa pamoja kwenye kliniki ya afya ya akili, Hospitali ya Rufani ya Mkoa Temeke, Dar es Salaam. Picha nyingine, Siku ya Afya ya Akili ilivyoadhimishwa kliniki hapo, kwa shughuli za usafi wa mazingira

UFANISI wa jambo lolote kimantiki, hutegemea mipango na utekelezaji wake; iwe ya kijamii, kiuchumi, hata kimaendeleo.

Ndani ya eneo la afya ya umma katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo sasa iko mbioni kuhitimisha mwaka wa nne, suala la afya ya akili linaanzia katika udhibiti. 

Msingi wake una mizizi kuanzia mipango afya, huku suala la kuimarisha afya ya akili kilishawekwa kipaumbele cha tisa, kama anavyosisitiza Meya wa Manispaa ya Songea, Michael Mbano mwezi uliopita.

Wakati kuna hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, akawataarifu wabunge kwamba serikali inatarajia kuanzisha Baraza la Afya ya Akili nchini.

Ni chombo kinakachosimamia muundo unaoratibu sekta za kitaaluma na kiutendaji kushughulikia ufanisi wa afya ya akili nchini.

Anarejea serikali chini ya utawala wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Afya, imekiweka kipaumbele cha tisa katika kuimarisha huduma za afya ya akili.

Ni tamko lake Majaliwa, akijibu swali la Mbunge wa Iringa, Jesca Msambatavangu, aliyedadisi uanzishaji wa baraza hilo, baada ya kukithiri matukio yasiyo ya kawaida yanayochangiwa na tatizo la afya ya akili.

Ndani yake, kuna yanayoongozwa na wizi, mauaji na mapenzi ya jinsia moja. Hapo anataja lengo ni kuhakikisha kila mwananchi, pasipo kujali mazingira yake, anapata huduma bora ya afya ya akili na kwamba huduma tembezi, ni moja ya mikakati inayolenga kufanikisha azma hiyo.

JUHUDI MIKOANI

Kati ya Desemba 16 hadi 20 mwaka huu, mjini Songea, kulikuwapo kambi ya matibabu ya kibingwa ya afya ya akili katika Hospitali ya Rufani Mkoa wa Ruvuma.

“Idadi ya wagonjwa wa nje na wale wa kulazwa mnaowahudumia inaonesha kuwa hitaji la huduma hizi ni kubwa, hasa kwa magonjwa yanayoongoza kama vile msongo wa mawazo na matatizo ya utumiaji wa dawa za kulevya,” anatamka Meya Mbano.

Meya huyo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa, kwenye tukio la ufunguzi wa wiki mbili wa kambi tiba afya ya akili mkoani Ruvuma.

Anasema serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu imeweka kipaumbele kuimarisha huduma za afya ya akili akitaja lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anpata huduma bora, pasipo kujali mazingira yake.

Anataja madaktari bingwa ya afya ya akili mkoani Ruvuma, pia wataongeza maarifa kwa watoa huduma kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu.

Katika hilo, Daktari Bingwa wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Dodoma, Dk. Sadiki Mandaru, akaitaja kuwa kambi ya pili kufanyika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. ya kwanza ilifanyika katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Iringa.

Mtaalamu huyo anataja maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi na kupatiwa ushauri wa kisaikolojia, pia tiba ni matibabu ya sonona; wasiwasi uliopitiliza, na matumizi ya dawa za kulevya.

Ikaelezwa kuwa, madaktari hao wakatarajiwa kufanya kipimo kikubwa cha umeme wa ubongo, ambacho ni maalum kwa wenye ugonjwa wa kifafa.

Kupitia huduma hizo, ambazo mzizi wake unatokana na juhudi zake Rais Dk. Samia, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufani ya Mkoa Songea, Dk. Magafu Majura, anawashukuru ugeni huo wa kitabibu, akiutaja unasaidia kuwafikia wenye changamoto za afya ya akili.

Mnamo Oktoba 10, duniani kukiadhimishwa Siku ya Afya ya Akili, jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Aga Khan kulikuwapo tukio la matembezi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Gunini Kamba, akihutubia, anasema tatizo la afya ya akili ni kubwa na la muda mrefu, linalochangia kwa kiasi kikubwa na changamoto za kimaisha.

“Serikali ya Rais Dk.Samia imehimiza sana ubia na sekta binafsi hivyo kushirikiana katika matembezi haya kwa wingi ni furaha na inasaidia kufikia malengo ya kukabiliana na afya ya akili,” anatamka Dk.Kamba.

Anaendelea: “Tunapoteza tukiwa kazini, tunakutana na watu tofauti tofauti na mazingira tofauti, ambayo yanaweza kupelekea tatizo la afya ya akili. 

“Hivyo, ni vyema kujitambua mapema na kuchukua hatua kama mwajiri kuwasikiliza wafanyakazi wako, ili kuepukana na changamoto ya afya ya akili.” 

Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya Aga Khan, Sisawo Konteh, anashukuru jitihada zinazofanywa na wadau kukabiliana na tatizo la afya ya akili, zikiwa na msaada mkubwa kwa jamii, kukabili changamoto ya afya ya akili.

Aidha, anasema kumewekwa malengo ya kujitumia, kushirikiana na kuwa na uwazi katika kuelezea changamoto ya Afya ya akili kutawezesha elimu kufikia jamii na kuchukua hatua kupambana tatizo la afya ya akili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Marcus Mwenezi Foundation, Belinda Nyapili, anasema katika kukabiliana na changamoto ya afya ya akili, wamekuwa wakitoa elimu kwa kinamama wajasiriamali.

Ni hatua inayotajwa kufanyika katika maeneo kama vile sokoni kukabiliana na viashiria vya afya ya akili yanayoweza kuwakumba wanapokopa na biashara kutoenda vizuri.