MIGONGANO WANYAMA NA WANADAMU… Wajerumani na wana - Namtumbo walipoingia ubia kumaliza kasoro

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 08:53 AM Nov 01 2024
Wanakijiji Kitanda, wakisafisha mahindi yaliyouzwa na wakulima katika Kituo cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, kijijini hapo.
PICHA ZOTE: JENIFER GILLA.
Wanakijiji Kitanda, wakisafisha mahindi yaliyouzwa na wakulima katika Kituo cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, kijijini hapo.

LICHA ya utalii wa wanyamapori kuwa sekta iliyo juu kuingizia taifa mapato, kutokana na fedha za kigeni, inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Sasa imefika hatua inaleta madhara kwa binadamu, ikiwamo kuharibiwa vyanzo vya mapato kama vile mashamba na vyakula na kuwaacha wakiwa katika hali ya umasikini kwa muda mrefu.  

Kwa upande wa pili, wanyamapori pia huathirika, kwa sababu binadamu hulipiza kisasi kwa kuwadhuru kutokana na uharibifu wanaofanyiwa.

 Kitakwimu, Sekta ya Maliasili na Utalii, inachangia pato la taifa kwa asilimia 17.5 na fedha za kigeni asilimia 25, pamoja na kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja Mil. 1.5. 

 Hata hivyo, Sekta ya Utalii na Wanyamapori inakabiliwa na changamoto mbalimbali, kubwa ikiwa migogoro na binadamu inayosababisha madhara kwa pande zote mbili.

 Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2012 hadi 2019, watu 642 wamejeruhiwa, pia 1069 wamepoteza maisha na mifugo 792 iliuawa; vilevile kuna ekari 41,041 za mazao zimeharibiwa, kutokana na migongano hiyo baina ya binadamu na wanyamapori. 

KUTOKA NAMTUMBO

Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, ni moja ya maeneo yanayotajwa kukabiliwa na changamoto ya migongano kati ya binadamu na wanyamapori. 

Hiyo ikasababisha uharibifu mkubwa wa mazao na kuwaacha wanakijiji katika umaskini, huku wakilipa kisasi kwa kuwawinda na kuwaua wanyama hao.

 Kwa kutambua umuhimu wa binadamu na wanyamapori kuishi pamoja na kutegemeana, Halmashauri ya Namtumbo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), wamebuni mikakati ya kupunguza kuelekea kabisa migogoro hiyo.

 Taasisi hizo zilikaa pamoja na kuibua miradi ya miradi ya kibunifu, inayohakikisha kuwa makundi hayo yanakaa pamoja kufurahia rasilimali zinazowazunguka. 

Mbinu hizo ni kama vile elimu kwa jamii namna ya kukabiliana na wanayamapori waharibifu na kuwafundisha fursa zinazopatikana kutokana na uwapo wa wanyama hao, ili wawaone sehemu ya maendeleo na si maadui.

 Mshauri wa Kiufundi wa GIZ - Namtumbo, Chrian Zimbai, anawaambia waandishi wa habari, Chama cha Wanahabari wa Mazingira Tanzania (JET), anasema GIZ inaiongezea nguvu halmashauri hiyo kupunguza migogoro ya watu na wanyama.

 Chrian anasema, katika wilaya hiyo wanatekeleza mradi wa miaka mitatu ulioanza 2022 ukilenga kumaliza migongano kati ya binadamu na wanyamapori, wakishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika vijiji vya Mtelawamwahi, Ligunga, Kilimasera, Mtonya na Kitanda.

 Anasema kupitia mradi huo wanaijengea uwezo Halmashauri ya Namtumbo, namna ya kukabiliana na wanyama waharibifu, wanaipa ruzuku iwasaidie kuweka mafuta kwenye magari na kuwapa posho askari wa wanyamapori wa vijiji ili kuwarahisishia wanapokwenda kutekeleza majukumu ya uhifadhi.

 Ofisa huyo anaeleza kwamba, pia wanawapa vitenda kazi vya utekelezaji shughuli hizo ikiwamo pikipiki, kompyuta na vinavyohitajika kufukuza tembo kama vile dawa zenye harufu kali.

 Anasema kutokana na bajeti ndogo ya wilaya iliyotengwa kwa ajili ya kupunguza HWC, taasisi hiyo ya GIZ iliamua kutoa ruzuku ya shilingi milioni 120 kusaidia mafuta, sare, posho na hema. Vilevile wanatoa mafunzo ya kuweka vizuizi. 

Hiyo ni kama vile fensi yenye pilipili ili kuzuia wanyamapori waharibifu kama vile tembo kuingia katika makazi ya au maeneo ya kilimo, na hivyo kupunguza matukio ya migogoro.

 “Ama kwa kuhamasisha matumizi endelevu ya ardhi au kwa kuhimiza mbinu za matumizi ya ardhi zinazooana na makazi ya wanyamapori, tunaweza kusaidia kupunguza migogoro kwa kuunda maeneo ya ‘buffer’ au korridoni za wanyamapori,” anasema.

 Anasema, pia wanatoa mafunzo kwa jamii juu ya tabia za wanyamapori watambue namna ya kuishi nao na kujiepusha na uharibifu ikiwa ni mbinu mojawapo kuboresha uwezo wao wa kupunguza migogoro kwa amani.

 Lingine anasema, wanasaidia kwa zana za mafunzo ya Askari wa Wanyamapori wa Vijiji (VGS) katika Kituo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Jamii, kilichoko Likuyu Sekamaganga, kuwafundisha jinsi ya kushughulikia wanyamapori wakorofi na waharibifu.

Chrian Zimbaiya, Mshauri wa Kiufundi wa Taasisi ya GIZ, Namtumbo, Ruvuma.
 “GIZ inafanya kazi kwa karibu na mamlaka za eneo hilo, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na wadau wengine kuendeleza suluhisho za pamoja zinazoshughulikia mizizi ya migogoro ya binadamu na wanyamapori katika Wilaya ya Namtumbo,” anasema.

 Mradi huo anasema wanautekeleza katika Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi na wilaya za Tunduru mkoani Ruvuma.

Mhifadhi wa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Issa Ndomondo, anasema, wamekuwa wakiwashauri wanakijiji kutumia mbinu zilizotolewa na wataalamu kufukuza wanyamapori, mbinu sasa zinajulikana, hazina zenye ufanisi mkubwa.

 “Changamoto ilikuwa kubwa zaidi kabla ya GIZ kufika wilayani kwetu,” anasema, akibainisha kuwa watu wanashukuru kwamba matukio ya tembo kuvamia mashamba yamepungua katika vijiji vingi. 

 “Changamoto za HWC zimepungua katika vijiji vitano vilivyohusika kwenye mradi. Ni vijiji vitatu pekee bado vilikabiliwa na tatizo,” anasema kama GIZ isingechukua hatua hiyo, uharibifu wa mazao katika vijiji hivyo, hasa Likuyu Sekamaganga, ungekuwa mkubwa zaidi. 

SABABU MIGOGORO  

Ndomondo anataja sababu zinazochochea migogoro hiyo, ni ongezeko la makazi na idadi kubwa ya watu, zinazosababisha ardhi kuwa finyu na kushawishi wanakijiji kwenda kufanya shughuli za kiuchumi, kama vile kilimo kwenye mapito ya shoroba.

 Anataja sababu nyingine, ni uingizaji mifugo katika maeneo ya hifadhi, mabadiliko ya hali ya hewa yanayoleta ukame na njaa kwa wanyama, hivyo wanavamia maboma kusaka mahitaji yao.

 Katibu wa Kimbanda, Jumuiya ya Wanyamapori ya Kimbanda (WMA), Juma Kihindo, kwa kushirikiana na GIZ, wakaanzisha miradi ya usimamizi endelevu wa misitu, ikiwamo ya kuuza hewa ya safi inayosaidia kunyonya hewa chafu ya kaboni.

Hiyo, ndio ikawawezesha wakazi wa maeneo yanayozunguka kama vile Lusewa, Milonji, Ligunga, Matepwende, Msisima, Mnalawi na Malalawima kunufaika kiuchumi.

Anasema kabla ya miradi huo - Kimbanda WMA, ilikabiliwa na mwingiliano na wanyamapori, ikawafanya binadamu kuwawinda na kuwadhuru wanyama hao, kwa dhana “si rafiki kwa maisha yao.”

 “Kimbanda WMA tayari imeingia makubaliano na Carbon Tanzania (kampuni). Ushirikiano huu ni hatua kubwa kuelekea jitihada za uhifadhi endelevu na uangalizi wa mazingira katika eneo hili,” anasema.