MBOWE ALIPOSTAAFISHWA...

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 10:24 AM Jan 29 2025
Sura za Freeman Mbowe na Tundu Lissu, katika uchaguzi wa CHADEMA.
PIicha: HALFAN CHUSI
Sura za Freeman Mbowe na Tundu Lissu, katika uchaguzi wa CHADEMA.

MBIO za uchaguzi CHADEMA, zimefikia ukingoni Tundu Lissu ndiye Mwenyekiti Taifa na sasa anapanda daraja kutoka makamu na kuwa mwenyekiti, ni baada ya kumbwaga Freeman Mbowe.

Kilichokonga hisia za wafuasi na wajumbe waliopiga kura, ni namna Lissu alivyopangua hoja ya Mbowe anayesisitiza ‘hakuna sababu ya kubadilisha jenerali mzoefu, katikati ya mapambano.’

Ukumbini wakati wa kunadi sera wajumbe walielekea kumkubali Mbowe na hata kumpigia makofi japo haikuruhusiwa kushangilia huku wengine wakiamini Lissu, aliyezungumza wa mwisho asingekuwa na jipya.

Katika sera zake kwa wajumbe Mbowe anajinadi akiwataka wasibadilishe jenerali anayeongoza mapambano vitani wakati chama kipo katikati ya vita, na kwamba kufanya hivyo ni hatari kwa ustawi wa CHADEMA.

Anawaambia wanahitaji jenerali mzoefu akiwataka wasidanganyike kwa kuwa uzoefu ni muhimu kukuza taasisi.

"Tusifanye mchezo wa kupima ukali wa sumu kwa kuionja, kutokana na kazi kubwa niliyoifanya na wote mnatambua hilo. Nimebuni mikakati, ninapolifuatilia jambo nalifuatilia kwa kina kwa sababu nakipenda chama. 

“Ninakiona kama lulu ya taifa. Nendeni na mtu aliyepimika, kuzoeleka kwa mikakati na utayari wa kumsaidia mwingine. Ninaomba mniamini sitawaangusha kama ambavyo sijawahi kwa kujenga chama hiki kwa miaka 20,” anasema akioomba kura.

Shangwe zikaibuka, mjumbe akahoji iwapo ni kosa kubadili jenerali wakati wa vita, si sahihi kuibadili CCM wakati huu?

Mbowe akajibu, kisha akawaamsha wajumbe wakisema ‘anatosha kuendelea na nafasi hiyo’.”

LISU ULINGONI

Anaanza kukosoa hoja ya kutokimbilia kubadili jenerali katikati ya vita, akiwakumbusha madhila ambayo chama hicho kimepitia katika uchaguzi wa 2019, 2020 na 2024.

Lissu mwanasheria mbobezi anasema: “Mwaka 2020, CHADEMA iliambulia mbunge mmoja wa jimbo wa kuchaguliwa na wananchi, katika uchaguzi mkuu na miezi miwili iliyopita imeambulia asilimia 0.8 ya mitaa na vijiji kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, lakini jenerali yupo na hajafanya lolote kunusuru chama chake". 

Ni kauli iliwafanya wajumbe kushindwa kuficha hisia zao, baadhi wakicheka, wengine wakimshangilia Lissu na baadhi wakilaumu wasimamizi wa uchaguzi kwa kufumbia macho 'mashambulizi' ya Lissu kwa Mbowe.

Lissu anahitimisha kwa kuwapa tahadhari wajumbe kwamba kwa kuzingatia mifano hiyo, walipaswa kuamua wamwongeze muda Mbowe aongoze kwa miaka 26 waendelee na madhila yaliyopo au wafanye mabadiliko kwa kumpa kura zao.

Kabla ya kupigakura, unafanyika uhakiki mkali wa wajumbe na kwa kipindi chote cha uchaguzi, wasimamizi wakihakikisha unakuwa wazi, wajumbe wakiitwa kwa majina (wasiozidi sita) kwenda kupiga kura kwa kupeana nafasi na kutolewa fursa kwa yeyote mwenye dukuduku au kuwa na taarifa yenye shaka, kuieleza na utatuzi na ufafanuzi kutolewa.

Ni hatua inayoibua wajumbe wachache ambao kikatiba hawakutakiwa kupiga kura hiyo taarifa ikatolewa na wakaondolewa ukumbini.

WAFURAHISHWA

Baadhi ya wajumbe wa uchaguzi huo, wanapongeza utaratibu hasa uwazi na kushuhudiwa na kila mtu aliyekuwa ndani na nje ya ukumbi.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, anampongeza Lissu kwa ushindi na kumwahidi ushirikiano wa dhati katika harakati za kuimarisha demokrasia.

Ni katika mtandao wa X zamani (tweeter), Dorothy, anaandika: "Ninakupongeza Tundu Lissu kwa kushinda uchaguzi na kuwa mwenyekiti wa chama chako cha CHADEMA.

Kuchaguliwa kwako kunakufanya pia uwe Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Nikiwa makamu wako, ninakukaribisha sana katika uongozi wa TCD.

"Ninakuhakikishia ushirikiano wa dhati katika kupigania demokrasia ya nchi yetu. Pia ninampongeza Mbowe kwa kukamilisha muda wake wa uongozi na kuonesha mfano wa ukomavu wa kisiasa."

Kiongozi mstaafu ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, anamkaribisha Mbowe katika maisha mapya ya kustaafu huku akimpongeza kwa mchango wake alioutoa kwenye siasa za mageuzi.

"Ninakukaribisha mwenyekiti mstaafu katika ustaafu na kukuhakikishia kuwa kuna mengi ya kufanya nje ya siasa za uongozi katika kazi kubwa iliyo mbele yetu ya kujenga na kustawisha demokrasia inatuhitaji wanamageuzi walio ndani na nje ya uongozi."

HALI ILIVYOKUWA

Ulinzi kuhakikisha hakuna hujuma katika uchaguzi huo uliimarika kila kona ya ukumbi hadi vyooni. Vyooni na ukumbini walinzi walitanda wakizuia wanachama kuzungumza kwa makundi au kuteta jambo lolote.

Walifanya hivyo kudhibiti uwezekano wa kutoa na kupokea rushwa kutokana na tuhuma zilizokikumba chama hicho siku za hivi karibuni zikidai kuna baadhi ya wanachama walipeana mlungula katika mazingira kama hayo.

Baada ya Lissu, kutangazwa mshindi shangwe ikaibuka nje na ndani ya ukumbi huku wafuasi wake wakimuimba kwa kulitaja jina lake kumpongeza kwa ushindi.

Wenye mahaba na Mbowe wakapoa japo baada ya muda baada ya matokeo kutangazwa wakaanza kurejea katika hali ya kawaida na kwamba wako tayari kumuunga mkono mshindi. 

Nje ya ukumbi wafuasi wa chama hicho, wakaikejeli timu Mbowe wakidai wamekula rushwa lakini wamemsaliti kwenye boksi wakimchagua Lissu.

Mmoja kati ya wafuasi hao akarusha kijembe, “wajumbe mmekula mpaka pilau na kuku lakini mmemchinja bosi wenu.”

Nyimbo mbalimbali za chama hicho zikatawala ukumbi Mlimani City, vifijo na nderemo, ikawa burudani eneo nzima na kuvuta macho ya watazamaji kuanzia abiria wa daladala, wateja wa maduka ya Mlimani City na majirani.

Itakumbukwa ni uchaguzi uliofanyika usiku kucha ambapo wajumbe ndani ya ukumbi hawakupata hata dakika moja ya kulala kutokana na msuguano ulivyokuwa. Nje ya ukumbi wafuasi wa chama hicho wakifurika na wengine kulala pembezoni ya kuta za ukumbi hata sakafuni kwenye vibaraza.

Wapo wengine wakikesha kwa kupiga soga zinazoambatana na ubishi wa nani aneyeibuka mshindi na kwanini.

SURA ZA USHINDI

Punde baada ya kumaliza  kuhesabu kura, wakala wa Lissu, Godbles Lema, akasambaza tabasamu na uso wenye  bashasha, ikawa ishara kwa wafuasi kuwa  matokeo ni mazuri, hivyo kulipuka kwa shangwe.

Aidha, wakala wa Mbowe, Boniface Jacob maarufu Boni Yai, akapoa baada ya kuhesabu kura, kabla ya matokeo kutangazwa, ndiyo ishara kwa timu Mbowe kwamba wameanguka.  

NJE YA UKUMBI 

Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Kwamba Mkoa wa Mwanza, Samason Matobogolo, anasema uongozi mpya utaleta tija kwa sababu siasa za Mbowe zilizoeleka.

"Ninaona kuanzia kwenye matawi mpaka juu tutakuwa pamoja. Tutafanikiwa kuongeza wafuasi na chama chetu kitasonga zaidi," anasema Matobogolo.

Chama kimepata viongozi watakaowapeleka kupata mabadiliko, na ni uchaguzi wenye matokeo chanya kwa maslahi ya taifa, anaeleza.

Anasema wanachohitaji wanachama ni amani, umoja na upendo pamoja na kusimamia kile wanachokiamini ili kukuza imani kwa wanachama.

Mjumbe wa chama hicho, Husan Ally anatangaza kuupokea ushindi huo kwa shangwe akiamini kuwa viongozi wamekuja na mawazo mapya kuleta mabadiliko.

Anamsifu Mbowe akisema amefanya vitu vingi vizuri lakini ni wakati sahihi kupumzika, akiamini CHADEMA inaweza kushika dola, kwa kuwa kila kitu kinawezekana chini ya uongozi mpya na anaamini hilo litafanikiwa.

Sharifa Suleiman, Mwenyekiti Baraza la Wanawake CHADEMA Taifa (BAWACHA), anashauri chama kiendelee kushikamana ili kisijigawe na kwamba umoja haujavunjika kutokana na matokeo ya uchaguzi akiahidi wataendelea kuwa imara.