Mbegu za migomba kwenye paketi zaja, huandaliwa kutoka kwenye ndizi mbivu

By Beatrice Philemon , Nipashe
Published at 05:45 PM Jul 16 2024
Gerald  Mabuto, akielezea teknolojia ya  mbegu za migomba kwa washiriki wanaotembelea banda la  Mzumbe.
PICHA: BEATRICE PHILEMON
Gerald Mabuto, akielezea teknolojia ya mbegu za migomba kwa washiriki wanaotembelea banda la Mzumbe.

KWA wakulima wa migomba, hii ni habari njema kwao. Kwa sababu juhudi zinafanyika kuandaa mbegu za migomba ili zipatikane kwa wepesi na urahisi kama ilivyo kwa mbegu za mchicha au mahindi.

Ni kazi ya utafiti inayofanywa na Gerald Mabuto, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya menejimenti ya rasilimali, katika Chuo Kikuu cha Mzumbe-kampasi ya Mbeya.

Anasema utafiti aliofanya sasa umewezesha kupata mbegu za migomba kutoka kwenye ndizi zilizoiva na kuzalisha miche, lakini juhudi zinaendelea kuandaa mbegu ambazo zitakaushwa na kufungashwa kwenye paketi, japo anasema hatua hiyo haijafikiwa.

Akizungumzia lengo la utafiti anasema ni kuinua biashara ya ndizi na kuongeza kipato kwa kutumia miche ya migomba inayozalishwa kwa kutumia ndizi mbivu asilia kama malindi, mkono wa tembo, mshare na kisukari.

Mabuto, anasema ni teknolojia mpya inayotumia njia za asili kuzalisha mbegu ya mgomba tofauti na mbinu nyingine zilizotumiwa katika kilimo hicho ambazo ni pamoja na kung’oa chipukizi kwenye shina.

Anataja sifa za mbegu hizo kuwa zinatumia muda mfupi kukua na kutoa matunda, kuanzia miezi nane hadi 11 tofauti na mbegu nyingine za mgomba zinazotumia miezi 15 hadi 18.

Anasema zinavumilia magonjwa kama mnyauko, hazishambuliwi na maradhi lakini pia zikishapandwa zinatoa mbegu kwa wingi.

Akizungumza na Nipashe kwenye Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba jijini Dar es Salaam, Mabuto anasema amefanya utafiti na kuibua mbegu mpya za mgomba ili kumwezesha mkulima kupata mahitaji yake kwa wingi.

Anafafanua kuwa mkoani Kagera na Mbeya wakulima wanalalamika kuhusu upatikanaji wa mbegu bora za migomba.

Anasema mbegu hizo wamezipa virutubisho na madini maalumu ya kutosha yanayofanya ziwe bora zaidi na ukinzani dhidi ya magonjwa yanayoshambulia mgomba.

Mabuto anataja madini hayo kuwa ni pamoja na kalsham na zink ambayo hukuza mmea kwa haraka na kuupa afya bora.

Amezalisha mbegu nne mpya za mgomba za mshare, malindi, kisukari na mkono wa tembo ambazo wakulima wanaweza kuzilima kibiashara na kuongeza kipato.

“Kwa kuanza, tumezisambaza kwa wakulima 15 wa mikoa ya Songwe na Mbeya kwa sababu ndiyo sehemu niliyofanya utafiti. Wamezipenda na ndiyo wateja wetu wakuu hivi sasa kwa ajili ya kilimo cha biashara,” anasema.

Anaongeza kuwa chuo kinamsaidia kupata wadau mbalimbali wa kilimo na tayari Wizara ya Kilimo imetambua uzalishaji wa mbegu hizo.

Anakumbusha kuwa Kagera, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga, Morogoro, Kigoma, Mara na Pwani ni mikoa inayolima ndizi kwa wingi na bado zao hili linaendelea kuenea katika mikoa mingine ya Ruvuma, Shinyanga, Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam.

Akizungumzia matumizi ya mbegu hizo anasema yanaanza na kuandaa eneo kwa kuchimba mashimo yenye urefu wa futi mbili kwenda chini na upana wa futi mbili pia na kuyajaza mbolea na kumwagia maji yenye kalshamu inayopatikana kwenye mimea ya aloivera.

“Ili kuyapata madini ya kalsham kutoka kwenye aloivera, mkulima anashauriwa kutafuta aloivera kuisaga kwenye blenda au kuiponda kwenye kinu kulingana na mahitaji ya shamba, kisha kutumia juisi iliyosangwa au kuihifadhi sehemu salama.”

Baada ya hapo achukue mililita 20 za juisi au maji ya aloivera na kuchanganya kwenye lita 20 za maji kwa ajili ya kumwagilia angalau kwa kila shimo lipate lita moja kwa kila mmea.

UCHAVUSHAJI

Mabuto anamshauri mkulima aweke mililita 50 kwenye lita 20 za maji kwa ajili ya kupulizia maua ya mgomba kwa sababu ya kupunguza uharibifu wa bakteria wanaoharibu maua ya ndizi au mgomba.

Anasema utafiti wa mbegu mpya za mgomba ulianza mwaka 2021 hadi 2024 kwa ufadhili wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na wakati wa utafiti alikuwa anaangalia uwezekano wa kupata mbegu kwa kutumia muda mfupi na zinazozaa matunda mengi na bora na zenye ukinzani kwa magonjwa.

Anaeleza kuwa bei ya kila mche ni Shilingi 2,000 na zinapatikana chuoni Mzumbe-kampasi ya Mbeya lakini pia mkulima anaweza kupata popote alipo kama akihitaji.

CHANGAMOTO

Mabuto anataja uwezeshwaji wa uzalishaji ili kufikia wakulima wengi zaidi pia wengi kutokuelewa na kutambua mbegu hizo.

Kilimo cha migomba ni maarufu hapa nchini kwa sababu ndizi zinatumika kwa chakula kwa baadhi ya mikoa mfano, Kagera, Kilimanjaro, Mbeya na  Kigoma hivyo ni zao muhimu kwa wananchi na wafanyabiashara pia.

Anasema ndizi ni moja kati ya mazao ya biashara iwapo wakulima watapata mbegu bora na kufuata kanuni endelevu za kilimo kama kupanda aina bora ya migomba inayozaa mazao na kukubalika katika masoko ya kimataifa.

Migomba inayolimwa Tanzania kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, asili yake ni India na Malaysia, iliyofika Afrika Mashariki katika karne ya tano.

Baadhi ya faida nyingi za ndizi ni chakula zikiliwa mbivu, ni matunda, ni mlo kamili zikipikwa na nyama, samaki na maharage. 

Kadhalika ni maarufu kwenye vitafunwa hukaangwa, kuchomwa, kutengenezwa viwanda ambao ni mkate wa ndizi na pia hutengenezwa krips.

Ni malighafi kuzalisha bidhaa nyingine kama pombe, juisi, chakula cha mifugo, hutengenezwa unga, mbolea (mboji), majani na maganda yake ni matandazo shambani (mulch), majani yake huezekea, migomba hutoa kivuli na kuleta ubaridi nyumbani.

Aidha, hutoa nyuzi za  kutengenezea bidhaa za sanaa, majani ni miamvuli wakati wa mvua  vijijini na sahani za kulia hasa Kagera, pia hutengenezwa kama vikombe kunywea vitu mbalimbali.

Ni kata ya kubebea mizigo kichwani, ni maganda yake ni bomba za kusafirisha maji mtoni au kisimani kuyasambaza vijijini.