MKOA wa Mara uko kwenye kampeni ya kuhamasisha wananchi, ili wajiandae kuchanja mifugo yao, kuwaepusha na magonjwa kama sotoka, yanayowashambulia na kuwaua.
Kampeni hiyo ilianza Januari 22 na imetangazwa kuendelea hadi mwanzoni mwa Februari , kisha itafuatia chanjo itakayotolewa kwa awamu mbili, kulingana na makundi ya mifugo yaliyopo.
Katibu Tawala Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Musiba Nandiga, ameiambia Nipashe kwamba, ameshawasilisha hilo katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo hiyo mjini Musoma hivi karibuni.
"Mkoa wetu una mifugo 4,745,411, ng'ombe ni 1,451,484. Miongoni mwa mifugo hiyo, mbuzi ni 707,442, kondoo 569,536, kuku 1,742,557 na wanyama wengine tulionao," anasema Nandiga.
Anafafanua kuwa ng’ombe, mbuzi na kondoo watapatiwa chanjo kuanzia keshokutwa, Februari Mosi, hadi Machi 30 na kisha itafuata zamu ya kuku watakaochanjwa kuanzia Mei Mosi hadi 30 mwaka huu.
"Chanjo itakayotolewa kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo inahusisha magonjwa ya homa ya mapafu na sotoka, kwa upande wa kuku ni kwa ugonjwa mdondo," anasema.
Nandiga anasema, wananchi watatakiwa kuchangia fedha kidogo kwenye uchanjaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo, huku chanjo ya kuku itatolewa bure.
Anafafanua kuwa, ni wajibu wa wananchi pamoja na kujitokeza na kushiriki katika kampeni hiyo ili mifugo yao ipatiwe chanjo stahiki ya kuzuia mlipuko wa magonjwa yanayoweza kudhuru mifugo yao.
UMUHIMU WA CHANJO
Nandiga anataja faida za chanjo, zinasaidia kudhibiti magonjwa ya mifugo na kukuza soko la chanjo hizo zinazozalishwa nchini.
"Kwa sasa tunahamasisha kutumia chanjo zinazozalishwa ndani ya nchi yetu, zikiwamo za kutoka Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), inayomilikiwa na serikali na chanjo zinazozalishwa na viwanda vinavyomilikiwa na sekta binafsi," anasema.
Anasema, ni muhimu kutumia chanjo zinazozalishwa nchini, kwani zinasaidia bidhaa hizo kuwa na soko la uhakika, pia kukuza ajira katika jamii.
Hapo anahimiza kwamba, chanjo za mifugo zinazozalishwa nchini, zitengenezwe katika mazingira rafiki na rahisi kutumiwa na wafugaji.
Anataja kuwapo magonjwa mbalimbali ya mifugo, na mengi yanadhibitiwa kwa njia ya chanjo, mahsusi akiutaja ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo, akinena ni ya gharama nafuu kudhibiti magonjwa ya wanyama.
"Tiba ni bei ghali endapo mnyama akiugua kwa kuwa wafugaji wamekuwa wakiingia gharama kubwa kutibu wanyama wao, ndio maana tunasisitiza chanjo, ili kudhibiti magonjwa ya wanyama kwani ni njia isiyokuwa na gharama kubwa," anasema.
Anasema ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo ni moja ya magonjwa yaliyo katika mkakati wa kutokomezwa duniani ifikapo mwaka 2030 na kwamba Tanzania imo katika orodha ya nchi zenye ugonjwa huo.
FURSA KWA WANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, anawataka wananchi na wafugaji mkoani humo kuchangamkia fursa ya kampeni hiyo, kwa kujitokeza kwa wingi kuchanja mifugo yao.
Anasema serikali imewekeza katika kuwasaidia wananchi ili waweze kujiimarisha kiuchumi na kwamba, ni jukumu la kila mwananchi kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali katika kuboresha maisha.
“Wafugaji wote wa mkoani Mara kushiriki kampeni hii kwa kupokea elimu kutoka kwa wataalamu kuhusu chanjo ili mchanje mifugo yote kwa bei ya ruzuku," anasema Kanali Mtambi.
Anasema ni wajibu wa wakuu wa wilaya, viongozi wa halmashauri na wataalamu wa mifugo na wadau wa sekta ya mifugo kwenda kutoa elimu kwa wananchi na kuwahakikishia kuwa chanjo hizo ni salama na zote zimetengenezwa hapa nchini.
"Chanjo itakapoanza kutolewa, wataalamu na viongozi msimamie zoezi hilo ili zisitoroshwe kwenda nje ya nchi, tumejipanga kudhibiti hujuma hiyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa itakuwa makini kufuatilia utoaji wa chanjo hizo," anasema.
Rai yake anatamka, ni wataalamu wanaosimamia mifugo, kuona namna ya kuwatambua wafugaji nchini, ili ruzuku iliyotolewa na serikali iwanufaishe wafugaji Tanzania, ambao ndio walengwa wa kampeni hiyo.
CHAMA WAFUGAJI
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Mrida Mshota, anasema chama hicho kimefurahishwa na hatua ya serikali ya kuanzishwa utaratibu wa kutoa ruzuku ya chanjo ya mifugo.
"Hii ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kuwasaidia wafugaji kwa kuwapa chanjo za ruzuku. Kwa niaba ya wafugaji tunashukuru serikali kuwafikia wafugaji," anasema Mshota.
Anawaomba wakuu wa wilaya, viongozi wa halmashauri na wataalamu wa mifugo kushirikiana na vyama vya wafugaji kuwahamasisha wafugaji kushiriki kampeni ya utoaji wa chanjo hiyo ya ruzuku na kuwafafanulia wafugaji kuhusu madhara ya wao kutokuchanja mifugo yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED