Usiyoyajua timu kundi moja na Taifa Stars AFCON 2025

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:15 AM Feb 03 2025
The Super Eagles
Picha: Mtandao
The Super Eagles

TANZANIA imepangwa kwenye Kundi C, katika droo ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, iliyochezeshwa hivi majuzi nchini Morocco. Iko na timu za Nigeria, Uganda na Tunisia.

Baada ya upangwaji, kumezuka mijadala mikali kutoka kwa baadhi ya wadau na mashabiki wa soka juu ya ugumu wa kundi ambalo Taifa Stars imepangwa.

Wengi hawasemi kuwa si kundi la kifo, ila ni kundi gumu ambalo Stars inatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kusonga mbele.

Sababu kubwa ni timu ambazo imepangwa nazo. Nigeria ni moja kati ya majina makubwa si barani Afrika tu, bali duniani pale linapokuja suala la mpira wa miguu.

Tunisia nayo ni hivyo hivyo, ni moja kati ya timu kubwa ya kutisha linapokuwa suala la soka barani Afrika na hata duniani.

Uganda si timu ngumu au yenye jina sana kwenye soka barani Afrika, lakini ni moja kati ya timu inayoipa ugumu na changamoto kubwa Tanzania linapokuja suala la soka, iwe timu za wakubwa, wanawake mpaka vijana wa umri wote.

Katika makala haya tumekusanya historia, rekodi na takwimu za timu zilizo kwenye Kundi la Stars na kukuletea mengi juu ya timu hizo, twende sasa...

1# Nigeria  ( The Super Eagles)

Ni moja kati ya timu za kuogopwa, si barani Afrika, bali hata inapofuzu kwenda kucheza Kombe la Dunia.

Hii ni moja ya timu ambazo zikiingia kwenye hatua hii, lengo si kufuzu kwenye kundi, bali kutwaa ubingwa wenyewe.

Ndiyo timu iliyochukuwa ubingwa wa AFCON mara nyingi kwenye kundi hilo. Imelitwaa mara tatu, 1980, 1994, na 2013. Mara ya kwanza ilikuwa ni 1980, ilipotwaa kwa kuifunga Algeria mabao 3-0, mechi iliyochezwa, Machi 22, Uwanja wa Surulere, nchini Nigeria ambapo michuano hiyo ilifanyika.

Taifa Stars ilishiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, baada ya kufuzu 1979, na awali ilikuwa kundi moja na mabingwa hao, zikiwa Kundi A, pamoja na timu za Misri na Ivory Coast.

Ilitwaa tena mwaka 1994 kwenye fainali zilizofanyika nchini Tunisia, ambapo iliichapa Zambia 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa, Uwanja wa El Menzah, Aprili 10, mabao yakifungwa na Emmanuel Amunike la Zambia likifungwa na Elija Litana. Ikumbukwe Zambia ilikuwa na kikosi kipya, baada ya kile cha kwanza kufariki kwenye ajali ndege iliyotokea mwaka mmoja nyuma, Aprili 27, 1993 nchini Gabon.

Mara ya tatu na mwisho, iliuchukua nchini Afrika Kusini, ilipoifunga Burkina Faso kwenye mchezo wa fainali, uliopigwa, Uwanja wa FNB, Johannesburg.

Timu ya Taifa ya Nigeria, imefanikiwa kuingia AFCON za 2025 kwa kuongoza Kundi D, ikimaliza na pointi 11.

2# Tunisia (The Eagles of Carthage)

Kama Nigeria, ni timu ambazo zinaanza AFCON zikiwa na nia moja tu ya kwenda kulibeba kombe, na haijalishi michuano hiyo inafanyika nje ya ardhi yao.

Tunisia ni moja kati ya timu tishio si kwenye kundi, bali kwa timu zote zinazoshiriki michuano hiyo.

Rekodi zinaonesha kuwa imelitwaa kombe hilo mara moja, 2004, kwenye fainali zilizopigwa nchini kwao.

Katika mchezo wa fainali uliochezwa, Februari 14, 2004  iliifunga Morocco mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Novemba 7 Stadium, jijini Tunis.

Imefanikiwa kutinga fainali za AFCON zinatazopigwa baadaye mwaka huu nchini Morocco, kwa kumaliza nafasi ya pili Kundi A, ikiwa na pointi 10, lililoongozwa na Comoro iliyomaliza na pointi 12.

3# Uganda (The Cranes)

Uganda ni timu yenye mzani kama Tanzania, ikiwa ni timu ambayo haijafanya maajabu yoyote kwenye michuano hiyo tangu ianzishwe 1957.

Si tu kwamba haijawahi kutwaa ubingwa, lakini kama ilivyo Stars, mafanikio yao makubwa mara nyingi ni kuvuka tu hatua ya makundi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa rekodi, inaipa sana changamoto Tanzania kila zinapokutana kwenye michuano yoyote ile, iwe AFCON, au CECAFA na kuwa kama watani wa jadi hivi, kwani zikikutana huwa 'panachimbika.'

Uganda imefuzu kutoka Kundi K, ikimaliza nafasi ya pili nyuma ya Afrika Kusini. Wakati Sauzi hao wakimaliza na pointi 14, Uganda ilihitimisha na alama 13.