BAADA ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amekisifu kikosi chake, akisema sasa kimekuwa moto wa kuotea mbali, akikiri kuwa kimebadilika na kucheza lile soka ambalo amekuwa akilihitaji tangu alipofika nchini.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam juzi, kocha huyo alisema kama wataendelea kucheza kwenye kiwango hicho, basi ana uhakika wa kutimiza malengo yote yaliyosalia, kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la FA.
"Nichukue nafasi hii kwa kuwapongeza wachezaji wangu, wamecheza vizuri, tulianza mechi vema, tukaitawala, tungeweza kufunga mabao matatu kabla ya bao la kwanza, wapinzani wetu walibaki nyuma ya mpira na kujaribu kutushambulia kwa kushtukiza na mipira ya faulo, lakini tulicheza kwa nidhamu kubwa.
"Niseme tu kuwa kwa sasa tuko kwenye njia sahihi, naona wachezaji wangu sasa wameanza kucheza soka ninalotaka na kwa kasi ninayoihitaji, wamebadilika, najivunia hilo, na ikiendelea hivi basi malengo yote yaliyobaki tuliyojiweka yatatimia," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.
Ulikuwa ni ushindi wa sita mfululizo kwa kocha huyo kwenye michezo ya Ligi Kuu, tangu alipotua nchini na kukianza kukinoa, akichukua nafasi ya Miguel Gamondi, ambaye aliondolewa pale ilipopoteza kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Tabora United, Novemba 7, mwaka jana.
Kocha huyo aliiongoza Yanga kushinda mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC, Uwanja wa Ruangwa, Lindi, ikazichapa Mashujaa FC 3-2, Prisons 4-0, Fouintain Gate 5-0, na Kagera Sugar 4-0, mechi zote zikipigwa Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge, Dar es Salaam, na Dodoma Jiji ambao walilala 4-0, mechi iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Katika michezo hiyo sita, Yanga imefunga jumla ya mabao 22, ikiruhusu mawili tu.
Yalikuwa ni mabao ya Clement Mzize, Mudathir Yahaya, Pacome Zouzoua na Kenndy Musonda.
Ushindi huo umeifanya Yanga kuzoa pointi zote sita kutoka kwa Kagera Sugar msimu huu, kwani katika mchezo wa mzuguko wa kwanza, ilishinda mabao 2-0, mechi iliyopigwa, Agosti 29, mwaka jana Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera, ambayo yalifungwa na Maxi Nzengeli na Mzize, ambaye aliifunga tena Kagera Sugar juzi.
Kwa sasa Yanga imefikisha pointi 42, kwa michezo 16 iliyocheza, ikishinda mechi 14, ilipoteza miwili, haijatoka sare, ikifunga mabao 36 na kuruhusu sita wavuni mwake.
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Melis Medo, alisema bao la kwanza la kizembe waliloruhusu, ndilo lililowaondoa mchezoni.
"Goli la kwanza tuliruhusu kirahisi, baada ya hapo kila kitu kikaenda nje ya mipango, siwezi kusema sana, lakini nina uhakika kuwa penalti walizopata walizawadiwa, hazikuwa sahihi, hasa ile ya pili ambayo walifunga bao, lakini nawapongeza kwa ushindi," alisema Medo.
Yanga ilipata penalti mbili kwenye mchezo huo, moja ilikoswa na Stephane Aziz Ki, nyingine ikiwekwa wavuni na Pacome.
Kagera Sugar inasalia nafasi ya 15, ikiwa na pointi 11, ikicheza michezo 16, ikishinda miwili, sare tano na kupoteza michezo tisa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED