WILAYA ya Musoma ni moja ya wilaya za mkoa wa Mara, hasa jimbo la Musoma Vijijini, wana habari njema katika mikakati ya elimu 2025, ambayo ni kuinua masomo ya sayansi kwa kila kata.
Wananchi wamedhamiria kutenga sekondari mbili za kata za kidato cha tano na sita kwa ajili ya mchepuo wa masomo ya fizikia, kemia, hisabati, bailojia na jografia.
Ndivyo anavyosema Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Majidu Karugendo.
Anazitaja kuwa ni Sekondari ya Suguti itakayokuwa na mchepuo wa fizikia, kemia na hisabati (PCM), fizikia, kemia na bailojia (PCB), kemia, bailojia na jiografia (CBG) na uchumi, jiografia na hisabati (EGM).
Nyingine ni Sekondari ya Mugango ikitarajiwa kuwa na mchepuo wa kemia, bailojia na jografia (CBG) na EGM.
Ofisa elimu anasema hayo wiki iliyopita, wakati akizungumzia mikakati ya kuinua masomo ya sayansi kwenye sekondari za halmashauri yake, ili kuandaa wataalam wengi zaidi wa baadaye wa fani mbalimbali watakaolifikisha taifa kwenye dunia ya sayansi na teknolojia.
"Lengo letu ni kutaka kuinua masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa Musoma Vijijini na halmashauri yetu ili kuandaa wataalamu wa fani mbalimbali wa baadaye," anasema Karugendo.
Anafafanua kuwa sekondari hizo kila moja ina maabara tatu za masomo ya sayansi, bweni moja au mawili, maji na umeme, na kwamba hatua hiyo itasaidia wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo.
"Mwaka huu sekondari hizo zitakuwa na 'high school' kwa masomo ya sayansi, hivyo tunatamani kuona hilo linatimia ili kuwa na vijana wengi wabunifu kupitia masomo hayo kutoka huku kwetu," anasema.
Aidha, anasema wakati kukiwa na mkakati huo wa kuzifanya baadhi ya sekondari za kata kuwa za kidato cha tano na sita, huenda pia baadhi ya sekondari za vijiji zinazoendelea kujengwa zikafunguliwa mwaka huu.
"Mfano kuna sekondari za Muhoji, Rukuba Island, Nyasaungu, Butata, Nyamrandirira Technical na David Massamba Memorial, zitakazokidhi vigezo ikiwamo kuwa madarasa ya kutosha kuchukua wanafunzi, zitafunguliwa kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza," anasema.
Anafafanua kuwa kila sekondari imepokea Sh. milioni 584, kutoka serikalini za kuanza ujenzi, na kwamba kuna vijiji vingine sita ambavyo navyo vimepata vibali vya kujenga sekondari.
Ofisa elimu huyo anavitaja vijiji hivyo kuwa ni Chitare, Katakkryo, Kiriba, Mmahare, Musanja na Nyambono, huku akiongeza kuwa itafika wakati kila kijiji kitakuwa na sekondari yake.
Musoma Vijijini ipo ndani ya halmashauri yetu ina vijiji 68, kata 21 na sekondari 24 za serikali na mbili za binafsi, kwa mwamko wananchi wa kuinua elimu, ninaami kila kijiji kitakuwa na sekondari yake," anasema.
JICHO LA MBUNGE
Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, anasema vijana wa Kitanzania wakiwamo wa jimboni mwake, wanapaswa kujiandaa kuingia katika ushindani wa dunia ya sasa na ijayo wa ajira, taaluma, ubunifu na uchumi.
"Maoteo au global forecast, ifikapo mwaka 2030, utakuwapo upungufu wa wataalamu milioni 80 ifikapo mwishoni mwa mwaka huo, kampuni kubwa duniani zitatumia takribani Dola za Kimarekani trilioni 3.2, kila mwaka kuwekeza kwenye akili bandia au akili mnemba (Artificial Inteligence -AI)," anasema Prof. Muhongo.
Anaeleza kuwa, kampuni zitafanya hivyo, ili kutatua tatizo la ukosefu wa wafanyakazi duniani, na kwamba roboti zitatumika kwa wingi, na kwamba ni muhimu kuwekeza katika masomo ya sayansi.
"Tunaanza na sekondari chache, lakini zinahitajika nyingi zaidi. Kwa mfano sekondari za Bugwema, Nyakatende, Kiriba na Etaro ambayo ina chumba cha kompyuta, zote zina maabara tatu," anasema.
Mbali na hizo, mbunge huyo anazitaja nyingine zinazolengwa kuwa na kidato cha tano na sita kuwa ni Rusoli, Makojo na Nyambono, ambazo anasema kila moja ina maabara mbili.
"Wanavijiji wanaowamba wadau elimu wakiwamo wazaliwa wa Musoma Vijijini waishio maeneo mbalimbali, waendelee ushirikiana na serikali kuchangia ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi katika sekondari za jimboni humu ili kuboresha masomo ya sayansi.
MFUKO WA JIMBO
Mbunge huyo anasema fedha za mfuko wa jimbo ni Sh. milioni 75.7 na kwamba zimetumika kwa ajili ya vifaa vya ujenzi katika sekondari mbalimbali za kata na vijiji jimboni humo.
"Wiki iliyopita, Kamati ya Mfuko wa Jimbo ilitembelea ofisi za halmashauri yetu zilizopo Kijiji cha Suguti kwa ajili ya kuweka mikakati ya kununua vifaa vya ujenzi kwa ajili ya shule mbalimbali," anasema.
Prof. Muhongo anavitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni mifuko 1,970 ya saruji, mabati ya rangi 322 na nondo 430 za milimita nane, huku baadhi ya shule zitakazofaidika zikiwa ni Muhoji na Nyasaungu.
Mbali na hizo, nyingine ni Rukuba na zile zinazokamilisha ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi zikiwamo za Mtiro, Makojo, Nyambono, Bwai, Mkirira, Etaro na zinazoanza ujenzi wa maabara za masomo hayo za Bukwaya na Nyanja.
"Katika mgawo huo zimo pia sekondari za Chitare, Mwigombe, Mmahare, Musanja, Kataryo, na Nyabakangara ambazo wananchi wa maeneo hayo wapo kwenye harakati wa ujenzi," anasema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED