NI miaka 25 tokea Tanzania lilipompoteza mwasisi wake Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Oktoba 14, 1999 akiwa kwenye matibabu kwenye Hospitali ya Mtakatifu Thomas huko Uingereza.
Alipotwaliwa wapo baadhi ya watu walisema huenda Tanzania inekumbwa na hali ya kutokuelewana na kuvutana katika baadhi ya mambo na hata wananchi kugawanyika.
Hilo halijawezekana kwani baada ya miongo miwili na nusu sasa hakujawa japo hata na ishara ya kutokea mpasuko wa kitaifa au mgawanyiko, badala yake Tanzania imezidi kuwa moja na kupata mafanikio makubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Pamoja na kwamba miaka 23 ya utawala wa Mwalimu Nyerere taifa lilikuwa likifuata mfumo wa chama kimoja, hata pale viliporuhusiwa vyama vingi, nchi imebaki katika mshikamano.
Kwanini basi hakujawa na mgawanyiko, mpasuko au utengano wowote? Hakuwezi kutokea na yote hayo kwa kuwa waasisi wa taifa hili, Mwalimu Nyerere na mwenzake Sheikh Abeid Amani Karume, waliweka misingi, miiko, uadilifu na kanuni za kudumisha mtangamano.
Ndiyo maana hata alipoingia madarakani Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, taifa limeendelea kubaki vilevile bila kutikisika au kushtushwa na lolote.
Licha ya waasisi hao kuondoka duniani wakiacha nchi ikiwa moja, yenye katiba zake, kanuni, taratibu, miiko na miongozo kama nguzo na kinga zinazolinda usalama wa taifa, watu na utamaduni mmoja.
Nyerere ambaye amekufa miaka 25 iliyopita ameiacha Tanzania ikishikamana bila ukabila, udini, ukanda wala ubaguzi wa ina yoyote.
Amewaacha Watanzaia wakiitana ndugu. Kila mmoja akiheshimu ubinadanu na utu wa mwenzake, kuthamini heshima ya kila mmoja, kusaidiana na kuhurumiana. Watanzania hawajivunii dini, kabila wala rangi zao.
Katika muda wote wa miaka ya uongozi wake, Mwalimu Nyerere alisimamia misingi ya uongozi na kuwataka viongozi katika nafasi zao kutambua kuwa binadamu wote ni sawa.
Alikuwa akisema mara kwa mara katika maisha ya uongozi wake wakati wa kupigania uhuru na hata baada ya kujitawala kuwa, kila mmoja anastahili kuheshimu wenzake na kuheshimiwa pia, akithamaniwa na kutambuliwa utu wake.
Nyerere hakuwa mtetezi wa haki za binadamu kwa Tanzania peke yake bali akipaza sauti yake kimataifa. Kila mahali duniani ambako binadamu walibaguliwa na kutengwa, Mwalimu hakusita kuwasemea.
Wakati Tanzania kila mwaka wamekuwa wakimkumbuka mwasisi wao, duniani kwenye midahalo na mijadala mbalimbali, kiongozi huyo hukumbukwa kwa uongozi wake bora uliosifika hasa usiothamani mali na utajiri.
Nyerere na mshirika mwenzake Karume ndio waliokuja na wazo la kuyaunganisha mataifa ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 na kuundwa kwa taifa ambalo halikuachwa na wakoloni liitwalo Tanzania.
Mwalimu Nyerere hakuishia hapo lakini pia alihakikisha mataifa yote ya kusini mwa Afrika yaliokuwa yakitawaliwa kibabe na wakoloni nayo yanajikomboa na kujitawala.
Akaweka mkazo mkubwa wa kuhifadhi vyama vya ukombozi kwenye ardhi ya Tanzania, wapigania uhuru wake hadi pale walipopata uhuru katika nchi zao.
Kiongozi huyo ndiye aliyeweka mkazo na kuhakikisha inaundwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967 kati ya Tanzania, Kenya na Uganda ingawa baadhi ya viongozi wenzake hawakutaka mpango huo.
Zikazuka fitna, mizengwe na kila aina ya hila zilizotaka jumuiya hiyo ife. Kweli ikafa miaka 1977 na mataifa wanachama wakarudi nyuma kimaendeleo baada ya mafanikio makubwa waliyoyapata kupitia mtangamano.
Hata hivyo baada ya kupuuza mawazo ya Nyerere, viongozi walikuja kuongoza madola baadaye mwaka 1999 wakaanzisha tena mchakato wa kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki kama alivyotaka Nyerere miaka mingi iliyopita safari hii ikiwa na mataifa mengi zaidi.
Mbali na Kenya, Uganda na Tanzania imezileta pamoja Rwanda, Burundi, Congo, Sudan Kusini na Somalia.
Nyerere ametwaliwa, hatunaye tena, hatarudi lakini fikra zake, maono na mawazo yake, yataendelezwa kwa bidii na kila rais au utawala utakaoshika madaraka kwakuwa taifa hili lina misingi, asili na miiko ambayo ilianzishwa na waasisi hasa yeye na Karume.
Mwalimu alichukia unyonyaji, uonevu, kukandamiza haki za wanyonge, unyanyasaji lakini pia hakuwa kiongozi aliyependa upendeleo.Akichukia rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na matumizi mabaya ya rasilimali za taifa.
Kiongozi huyo atakumbukwa kwa uongozi wake ambao hakuonyesha hata mara moja anahamanika na kutaka utajiri, hakuwa mkwapuzi wa mali za umma wala kujilimbikizia mali kama ilivyokuwa kwa baadhi ya viongozi.
Mwalimu Nyerere akiamini katika nadharia ya uongozi si ajira inayohitaji malipo lakini pia aliamini kila binadamu yuko huru kuchagua anachokiamini alimradi jambo hilo halivunji sheria za nchi wala katiba.
Taifa linapokikumbuka kifo chake, lazima viongozi wajipekue, Watanzania pia wajichunguze endapo bado wanaishi katika ndoto zake hizo au wameziacha kanuni hizo na sasa wanakwenda segemnege, shaghalabaghala au ndivyo sivyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED