Kamwe tusikubali mazingaombwe kwenye uchaguzi

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 08:08 AM Jan 10 2025
Kamwe tusikubali mazingaombwe kwenye uchaguzi.
Mchoraji: Msamba
Kamwe tusikubali mazingaombwe kwenye uchaguzi.

ENZI hizo tukiwa shule za msingi, kila Alhamisi ya mwisho wa mwezi, mwalimu wa zamu alikuwa akitutangazia kuwa kesho Ijumaa, atakuja mtu kuonesha mazingaombwe, hivyo kila mmoja aje na kiingilio.

ENZI hizo tukiwa shule za msingi, kila Alhamisi ya mwisho wa mwezi, mwalimu wa zamu alikuwa akitutangazia kuwa kesho Ijumaa, atakuja mtu kuonesha mazingaombwe, hivyo kila mmoja aje na kiingilio. 

Nakumbuka alikuwa akija mchezesha mazingaombwe huyo aliyekuwa na asili ya bara Asia na kutuonesha mambo ya ajabu ajabu, ikiwa ni pamoja na kutafuna nyembe na kutapika sindano nyingi! 

Tukiendelea kushangaashangaa, alikuwa akichukua karata na kuziunganisha kimaajabu na kuwa kama mkanda mrefu, nasi tukishangilia kuhalalisha kiingilio chetu. 

Kana kwamba haitoshi, alikuwa akichanachana karatasi na kuzifikicha na ghafla kutoa leso nyingi na kuzigawa kwa baadhi yetu watazamaji, waliopata wakawa wamefidia viingilio vyao. 

Siku moja katika maonesho hayo, tuliyoyaona kama ya kichawi, mwanamazingaombwe huyo, akaniteua mimi nishiriki onyesho la kupasua tumbo na kutoa chakula na kuniponya papo hapo.

Nashangaa sikuwa na woga, wala hofu, nilikubali na akanikalisha kwenye meza na kunilisha ndizi kibao na kuwaambia watazamaji kuwa punde atanipasua na kuzitoa ndizi nilizokula.

 Watu walinyamaza katika chumba hicho cha darasa kwa hofu, wakiamini kuwa ulikuwa mwisho wa maisha yangu. Hakika nilibugizwa ndizi mpaka kitumbo ndi! 

Baadaye akanilaza kwenye meza na kunifunika uso nisione kilichokuwa kikiendelea, huku akionya kuwa nikipiga kelele na hata watazamaji wakipiga kelele, basi safari ya mwisho ni kwa Muumba wangu. 

Kwa hofu ya kiuanafunzi na hasa kitoto, nilitii amri na kulala nakuhakikisha hata sikohoi wala kupiga chafya, nikihofia maisha yangu kutoweka, huku wazazi nyumbani wakiwa hawajui nini kinaendelea. 

Basi ‘upasuaji’ ulipoanza, nikahisi kama nafinywafinywa tumboni na mjanja aliyeteka akili zetu na mara akanibandika pamba nyingi tumboni, eti kuonesha kuwa kweli alinipasua na kutoa ndizi, ambazo kweli nilipoamka nikaziona pembeni zikiwa zimesagwasagwa mithili ya zilizotafunwa na kumezwa. 

Nilipoamka, wanafunzi wakashangilia kwa nguvu huku wengine wakinipongeza na kutaka kujua nilikuwa najisikiaje, lakini nami nikawa nawashangaa ingawa kwa hofu, lakini sikuthubutu kugusa tumbo nikihofia kufumua ‘mshono’!

 Na siku hiyo ndiyo lilikuwa onyesho la mwisho na kabla hajaondoka akanifuata na kunitaka nifuatane naye mpaka nyumba ya kulala wageni alikofikia, kwani hakuwa mkazi wa mji tulipokuwa tukiishi. 

Walimu waliniruhusu, kwani muda wa kutawanyika ulishawadia, nikafuatana naye kwa kutembea kwa miguu mpaka alikokuwa amefikia, tukaingia chumbani mwake akanizolea sarafu nyingi alizokuwa nazo akanipa. Sikuamini!

 Hata nilipofika nyumbani, nikamsimulia mama na kumwonesha zile pesa akashangaa na kunihoji nilikozipata, akafurahi sana, ingawa alinionya nisiwe najitia kimbelembele kufanyiwa majaribio kama hayo, kwani kuna siku wakikosea nami ndiyo basi. 

Hata Jumatatu shuleni, wenzangu wakawa hawaamini kama ni mimi niliyepasuliwa. 

Basi ndugu zanguni, mwaka huu ni mwaka mwingine wa mazingaombwe, mwaka wa watu kutafuta kura za kula. Ni mwaka ambao tutaoneshwa na kusimuliwa mengi mazuri ya kusadikika. 

Watu wema wataongezeka ghafla, ‘watoto’ wataongezeka wa kutoa shikamoo za bwerere bila hata kujali umri, ili kubembeleza kono liende kinywani. Ni wakati wa mavuno kwa wapiga ‘kula’. 

Kama kawaida zile ahadi za mkinichagua nitaleta hiki na kufuta hiki na kile, na nitapambana na changamoto hizi na zile na mtaishi maisha mazuri ambayo hamjapata kuyaishi. 

Zile kauli za tangu mwaka 1961 tulipopata uhuru mpaka leo zitatamalaki.Bila shaka mmeanza kusikia wenyeviti wa kamati za usalama za mikoa 

wameanza kupaza sauti dhidi ya wanaojipitisha majimboni kuomba kutambuliwa kama watia nia. 

Marufuku zimeanza kupigwa huko, kwamba wabunge waliopo wasibughudhiwe, waachwe wamalize ngwe yao kwa usalama na watu wavute subira, ili muda ukifika wafanye yao. 

Baadhi ya wabunge wanaolindwa na kauli hizo, ni ambao tangu wachaguliwe hawajatia mguu majimboni na kama wamekwenda ni bababisha bwege tu, ili kuuza sura. 

Kuna wabunge na madiwani ambao wamediriki hata kuhama maeneo yao na kuishi kwingine, wakiwekeza miradi yao wakisubiri mwisho wa ngwe wavune kiinua mgongo watanue miradi.

 Watia nia msirudi nyuma, mbele kwa mbele tu mpaka kieleweke, safari hii tunataka wabunge imara wanaojua shida za wananchi na si chawa wanaoshangilia na kusifu kila kitu, wakikodolea hisani za mamlaka ya uteuzi.

 Wananchi tusikubali mazingaombwe tena, tusiwe tayari kulishwa ndizi na kupasuliwa feki, ili kudanganywa kuwa tunaletewa maendeleo, kumbe babaisha bwege! Tukipata wabunge wazuri ndipo tutapata serikali nzuri. Inshallah!