RIPOTI ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kukabili Dawa za Kulevya na Uhalifu, (UNODC), inataja idadi ya waraibu wa dawa za kulevya duniani kuwa ni milioni 292.
Kiwango kikiongezeka zaidi ya idadi ya mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia ishirini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Akizindua ripoti ya mwaka huu, mwezi uliopita huko Vienna Austria, Mkurugenzi Mkuu wa UNODC, Ghada Waly anaeleza kuwa, kuzalisha dawa za kulevya na kuzitumia kunazidisha hali ya kukosa utulivu, usawa, amani na madhara makubwa ya kiafya, usalama pamoja na ustawi duniani.
“Tunahitaji kutoa matibabu yaliyofanyiwa uchunguzi na kuwa na ushahidi wa kusaidia waathirika huku tukilenga kuondoa soko haramu la dawa hizo na kuwekeza zaidi kuzuia matumizi yake.” Anasema Ghada.
UNODC inasema, bangi inatumika zaidi duniani kote ambako kuna watumiaji milioni 228, lakini pia uzalishaji wa cocaine umeweka rekodi mpya ya juu ukifikia tani 2,757 mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 zaidi tangu mwaka 2021.
Ingawa wastani wa watu milioni 64 duniani kote wanakabiliwa na matatizo yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya, ni mtu mmoja kati ya 11 anayetibiwa. Anasema, Mkurugenzi Mkuu wa UNODC.
Ripoti ya UNODC inaigusa Tanzania na dunia nzima kwa ujumla, ndiyo maana inaanza kufanyiwa kazi Bagamoyo mkoani Pwani, wadau wakitoa elimu kwa waraibu waziache dawa hizo, wajue haki zao, kupunguza unyanyapaa na jamii ifahamu madhara yake na kuzikataa.
Aidha, waraibu, wanafunzi, walimu, wazazi, viongozi wa dini, serikali, polisi, madaktari, wanasheria na maofisa wa ustawi wa jamii wilayani Bagamoyo wanahusishwa.
Shirika la kiraia la Life LHRO linalowezeshwa na Taasisi za Kimataifa za AFHR Grant na PEPFAR za Marekani ndilo linalofanya kampeni hizo.
Mwalimu mlezi wa Shule ya Msingi Kizuiani Bagamoyo, Raphia Azza, ambaye mradi huo upo shuleni kwake, anasema wana vipindi maalumu vya kuelimisha wanafunzi kuhusiana na madhara ya dawa za kulevya, na ujio wa LHRO umewaongezea ujuzi na nguvu zaidi.
"Tunatenga muda kuwafundisha kujiepusha na dawa hizo, shirika la LHRO limetuongezea elimu hii, kwani ni wabobezi kwa mbinu mbalimbali za kutambua vyanzo vya vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya," anasema Raphia. LHRO wamewafundisha umuhimu wa kuzingatia malezi, kujua tabia za wanafunzi na kufuatilia mienendo yao na kuwaepusha na makundi hatarishi na ya kihalifu.
Aliyekuwa mraibu Zaka Nchimbi, anayeishi kata ya Kisutu wilayani Bagamoyo, ambaye ni dereva wa bodaboda, anasema elimu hiyo imemtoa kwenye dawa hizo."Nilishtuka mapema baada ya kuelimishwa na sasa ninatumia dawa ya methadone huku nikiendelea kufanya kazi yangu," anasema Nchimbi.
Kiongozi wa Msikiti wa Wazee Magomeni, Ustadhi Haji Mwinyi, amefikiwa na LHRO anasema, elimu hiyo imekuja wakati sahihi na kwamba wamekuwa wakitoa nafasi kwa waelimishaji wa shirika hilo wakati wa mawaidha kuzungumza na waumini.
"Dawa hizi zimeharibu vijana wengi. Baada ya kupata elimu hii, tumekuwa tukitumia kipindi cha mawaidha, kukumbusha waumini kuzingatia malezi mema ya watoto wao," anasema Ustadhi Mwinyi.
Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Sayuni Mathayo Mwanjisi, anasema, elimu hiyo inatolewa kanisani kwake, na kwamba kilichobaki ni kuendelea kuliombea taifa ili vijana waache dawa hizo na umma ubadilike.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Bagamoyo, Mushana Mujema anasema, hatua ya shirika hilo kuihusisha polisi katika mradi huo ni nia halisi ya kutaka kusaidia vijana kuacha dawa hizo. Anasema, wanazuia vitendo vyote vya uhalifu, kwa kuwa baadhi ya vijana wanaotumia dawa hizo ni wahalifu na kwamba wataendelea kushiriki katika kutoa elimu ili kusaidia vijana kuacha maisha ya uraibu wawe msaada kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo, Dk. Kandi Lussingu, anapongeza viongozi wa LHRO kwa kuanzisha mradi huo na kufafanua kuwa umeibua waraibu wengi zaidi wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya kutibiwa na methadone. Anaongeza kuwa, miaka ya nyuma kulikuwa na idadi ndogo ya waraibu wanaofika kunywa dawa, na kuongeza kuwa sasa wamefikia zaidi ya 700, na kwamba hatua hiyo inaonyesha ni jinsi gani elimu imewasaidia.
"Niwashukuru viongozi wa idara ya maendeleo ya jamii, polisi kata, dawati la jinsia na wadau wengine kwa kushirikiana na LHRO kuwatoa vijana katika uraibu wa dawa za kulevya,"anasema Dk. Kandi. Anaeleza kuwa, ni muhimu vijana waelimishwe, watambue madhara ya dawa za kulevya ili waachane nazo, pia wapewe elimu ya ujasiriamali pamoja na mtaji ili waweze kujishughulisha na shughuli za kuwaingizia kipato.
LHRO KAZINI Mkurugenzi Mtendaji wa LHRO, Al-Karim Bhanji, anasema, mradi wa kutoa elimu hiyo, ulianza Desemba mwaka jana na kwamba wameingia awamu ya pili ambayo inaelekea ukingoni na karibuni wataendelea na awamu ya tatu hadi Desemba mwaka huu.
"Wafadhili wetu AFHR na PEPFAR walitupatia Sh. milioni 50. Tunaendesha mradi huu katika kata tano za Magomeni, Kiromo, Kisutu, Nianjema na Dunda, tayari kuna makundi mbalimbali tumeyafikia," anassema. Bhanji anaongeza kuwa tangu waanze kutoa elimu, wamefika katika shule za Msingi Kiromo na Jitegemee, Kizuiani na Nianjema na sekondari za Mwambao na Asanary.
Aidha, wamekifikia kituo kidogo cha polisi Magomeni, hospitali ya wilaya, zahanati za Kiromo, Buma na maskani ya Buma na vijiwe vya bodaboda.
Mbali na hapo anasema, wameyafikia makanisa ya Katoliki Parokia ya Mtakatifu Elizabeth, Kanisa la Mlima wa Sayuni lililoko Dunda, Kanisa la Mungu Baba lililoko Nianjema na la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na vijiwe mbalimbali vya waraibu wa dawa hizo.
Bhanji anasema, wametinga misikiti ya Masjid Rahman, Msikiti wa Wazee Kata ya Magomeni, Masjid Noor na Masjid Rahman ulioko Kata ya Dunda. Anafafanua kuwa, njia wanayotumia kutoa elimu ni mikutano ya hadhara vijijini, kwenda shuleni kuzungumza na walimu na wanafunzi na kwenye nyumba za ibada.
Anasema wanatamani kuona jamii ikibadilika, waraibu wakitambua athari na kuacha dawa hizo , pia wakifahamu haki zao akisema kumekuwa na unyanyapaa, unaofanywa na wanafamilia na jamii wakiwachukulia kama wasiofaa.
Kundi hilo anasema linatakiwa kusaidiwa, ndio maana wanatoa elimu, wasinyanyapaliwe, watambue haki za kupata tiba na kuachana na dawa hizo tena wanufaike na huduma nyingine za kijamii kama fursa za kiuchumi, miradi ya maendeleo na ujasiriamali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED