ULAZIMA wa Tanzania kufanya mapinduzi ya elimu, sayansi na teknolojia ni hoja zinazotawala maoni ya makundi mbalimbali yanayosikika wakati wa kuhakiki rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Wadau wanataka iwepo mikakati madhubuti ya kusongesha mbele sekta hizo ili kufikia mabadiliko na maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2050.
Ni katika mkutano baina ya Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na makundi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, wafanyabiashara, wazee, vijana, wanasiasa, wenye ulemavu, wadau wa maendeleo, mabalozi na mashirika ya kimataifa, katika mchakato wa kukusanya maoni yatakayojumuishwa katika kuandaa dira hiyo.
Kwenye vikao vilivyofanyika kwa nyakati tofauti wajumbe wanasisitiza kuboresha mifumo ya kutoa elimu pamoja na kufanya jitihada za makusudi za kuwafanya Watanzania kuwa na uelewa wa kutosha wa matumizi ya teknolojia katika shughuli mbalimbali.
Mfanyabiashara Judith Mhina, akatia maoni yake , anashauri kwamba ni muhimu mwalimu kulipwa kiasi cha kutosha , pamoja na kuhakikishiwa maisha bora na kuwa na kipato cha kumudu gharama za maisha ili wawaandae vyema wanafunzi.
Judith anaishauri serikali kutathmini upya mishahara ya watumishi wa umma wakiwamo waalimu ili kuendana na mabadiliko ya gharama za maisha, akieleza kuwa ili kuwa na jamii bora ni muhimu waalimu wawezeshwe kikamilifu na kuishi maisha ya kufanana na hadhi zao.
Anashauri serikali kuanza kuweka kipaumbele katika mafunzo na malezi ya watoto, kuanzishwe utaratibu wa kujifunza kuhusu teknolojia ya akili mnemba (AI), pamoja na kufundishwa kujitegemea na kujilinda dhidi ya mashambulizi mbalimbali ya kimwili kwenye mitandao ya kijamii na kule wanakoishi.
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Shekhe Mohamed Khamis, anashauri kuboresha maslahi ya walimu ili kuwaongezea motisha na nguvu za kiuchumi, akieleza kuwa itajenga jamii iliyoelimika kuelekea miaka 25 ijayo.
Pia anahimiza umuhimu wa serikali kusimamia ratiba na mapumziko kwa wanafunzi wa shule za serikali na binafsi ili kuwa na ulinganifu wa masomo na mapumziko kwa wanafunzi, ili washiriki shughuli zingine.
Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa Tanzania (UNA-Tanzania) Lucas Kifyasi, anasema suala la elimu halijawekwa kama moja ya sekta za kimageuzi wakati dira 2050 itatakiwa kutekelezwa katika kipindi cha mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo teknolojia itahitajika zaidi.
Anashauri kuwa dhana ya teknolojia inaendelea kukua, hivyo ni muhimu kuheshimu elimu ambayo ndiyo nyenzo kuu katika kuhakikisha kwamba teknolojia inarithishwa vizazi na vizazi, huku akisisitiza elimu iwekwe kama sekta ya kimageuzi kwenye dira 2050.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni za GSM, Benson Mahenya, anashauri kwamba kuna haja ya kufundisha elimu ya biashara kuanzia chekechea hadi vyuoni ili vijana wakue na kuelewa kuhusiana na masuala ya kibiashara.
TEKNOLOJIA
Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Utetezi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Azgard Stephen, anasema ni muhimu pia kutolewa kipaumbele katika masuala ya sayansi, teknolojia, na diplomasia katika mapinduzi ya kiuchumi na kijamii.
“Sisi CCT tuliangalia suala la sayansi na teknolojia kwa kuzingatia jinsi dunia ilivyobadilika na mapinduzi yanayotokea. Tunapendekeza diplomasia iwe sehemu ya vichocheo vya maendeleo ili kuwezesha Tanzania kujihusisha vyema katika biashara za kimataifa na kujitengenezea nafasi bora kikanda na kimataifa,” anasema Azgard.
Stephen anaongeza kuwa mapinduzi ya kidijitali ni mojawapo ya vichocheo muhimu vya maendeleo vilivyotajwa katika rasimu ya dira hiyo, akibainisha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika teknolojia na sayansi ili kufanikisha malengo ya taifa.
“Mpango wetu umetaja umuhimu wa sayansi na teknolojia kama kichocheo cha maendeleo. Tunashauri diplomasia nayo izingatiwe kama kichocheo, hasa katika nguzo ya uchumi ambayo inazungumzia ushiriki wa Tanzania katika jumuiya za kikanda na kimataifa,” anasema.
Mtaalam wa Programu wa Takwimu za Kijinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Wanawake (UN Women) , Dk. Sadananda Mitra, anasema kiwango cha uelewa wa kusoma na kuandika kwa Watanzania ni kizuri, lakini hawapaswi kuishia hapo.
“Lazima tuangazie vipengele kama muunganisho wa intaneti na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba hasa vijijini. Hii itawahakikishia watu wa maeneo hayo ushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo,” anasema Dk. Mitra.
Anasisitiza umuhimu wa sera zinazoongozwa na ushahidi, akieleza kuwa upungufu wa data au upatikanaji wa data usio kamili umekuwa changamoto katika nyaraka nyingi za sera zilizopita, akishauri teknolojia kuhusishwa zaidi ili kuongeza ufanisi.
“Tunapaswa kuimarisha mifumo ya kukusanya data na kutumia takwimu sahihi na zilizogawanywa vizuri kufuatilia maendeleo yetu,” anasema.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Hanspaul, Satbir Hanspaul, anasisitiza kuwa kwenye elimu kuna umuhimu wa kuwa na mitaala yenye kujumuisha masomo ya uchumi na biashara kwa kiasi kikubwa kwani Watanzania wengi wamekuwa na changamoto ya kushughulika na masuala ya fedha jambo ambalo kwa mtazamo wake anaona linalirudisha nyuma taifa.
Anasema matumizi ya mifumo ya kidijitali na AI yameongezeka maradufu miongoni mwa kampuni, benki na wafanyabiashara hata ambao wapo mbali na miji kitu ambacho hakikuwepo kwa miaka 25 iliyopita.
“Kwenye rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 sijaona jambo hili likiangaliwa sana, kwamba sisi Watanzania tunatumiaje fursa ya AI ?” anahoji Hanspaul.
MALENGO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo anasema suala la elimu tangu mwaka 2000 serikali ilijiwekea lengo kwamba ifikapo 2025 angalau asilimia 90 ya watoto wanaomaliza shule za msingi waende sekondari, wakati huo ikiwa chini ya asilimia 20.
Anaeleza kuwa ilipofika 2022 walifanya tathmini walibaini kwamba takribani asilimia 70 ya vijana wanaomaliza shule za msingi wanakwenda sekondari na kwamba tathmini ya mwaka jana ilionesha ni asilimia 78. “Tunaamini hadi mwisho wa mwaka huu tutakuwa tumepiga hatua zaidi”.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED