BWAWA la kufua umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) zamani Stigler’s Gorge, ndani ya Mto Rufiji tangu mwanzo ni kazi iliyokuwa itekelezwe kati ya 1975 na 1985.
Itakumbukwa ni wakati wa awamu ya Mwalimu Julius Nyerere, lakini matarajio yalififia taifa lilipoingia kwenye vita vya Uganda kati ya miaka 1978 na 1980.
Baada ya vita na nchi kujihakikishia usalama rasilimali nyingi zilitumika kuwaondoa wavamizi, Tanzania ikajikuta kwenye changamoto lukuki kiuchumi.
Kutokana na hali hiyo mradi wa bwawa la Stigler’s Gorge au sasa JNHPP kwa kutumia maporomoko ya Mto Rufiji, likawekwa kiporo.
Ili kukidhi mahitaji makubwa ya umeme wa gharama nafuu kuliko unaotokana na mafuta, serikali ilijenga mabwawa ya Kidatu mkoani Morogoro na Mtera mpakani mwa Iringa na Dodoma kufua umeme wa maji ya Mto Ruaha-Mkuu.
Vilevile, iliendelea kutumia umeme wa bwawa la Nyumba ya Mungu mkoani Kilimanjaro na jingine eneo la Hale la Pangani , mkoani Tanga yaliyokuwa yamejengwa kabla ya uhuru 1961 na TANESCO ikiendelea kuyapanua baada ya uhuru na leo yanachangia umeme kwenye gridi ya taifa.
Pamoja na juhudi hizo, bado kuna dosari za upatikanaji umeme wa uhakika.
Upo usemi kuwa ‘hayawi hayawi huwa’ ikimaanisha kilichoshindikana awali sasa kinawezekana kama ilivyokuwa mradi wa mkakati kujenga bwawa kubwa kutumia maji Mto Rufiji ili taifa liwe na umeme kamilifu.
Naipongeza serikali awamu ya tano ambayo Rais Samia Suluhu Hassan wa awamu ya sita, alikuwa Makamu wa Rais wakati juhudi za kuanza utekelezaji mradi zilipoanza.
Kama siyo uthubutu, umakini wa aliyekuwa Rais wakati huo, John Magufuli, alipodhamiria kujenga JNHPP huenda leo shida ya umeme ingekuwa kubwa.
Kama siyo uthubutu huo, sipati picha hali ingekuwaje kuhusu kuwapo nishati hiyo ya uhakika nchini. Kadhalika, serikali ya awamu ya tano imekuwa chimbuko la miradi ya kimkakati kadhaa ambayo awamu ya sita inaimaliza na kusongambele.
Pia, inatekeleza miradi mingine kadri inavyoona inafaa. Kupitia juhudi hizo wengi sasa wana ufahamu wa kutosha kuwa tukidhamiria kwa dhati na kukawepo nidhamu,maadili kwa viongozi hakika Afrika inaweza kujikwamua kiuchumi bila kutegema sana misaada kutoka nje.
JNHPP inalenga kulipatia taifa megawati zaidi ya 2,100 sasa upo ukingoni, ni jambo la kujivunia. Taarifa kutoka TANESCO kwenye vyombo vya habari zinaeleza kuwa bwawa limefikia hatua ya mitambo ya kufua umeme kuwashwa na kutoa megawati 1,410 karibu asilia 70 ya kiwango cha megawati zinazotarajiwa.
Kadhalika, imethibitishwa kuwa njia za kusafirisha umeme kutoka Mto Rufiji hadi Chalinze zimekamilika kwa asilimia 99. Aidha, kituo cha kupoza umeme kinachojengwa Chalinze kimekamilika kwa asilimia zaidi ya 97 yakiwa ni mafanikio makubwa.
Mafanikio na miradi mingine ya kufua umeme na megawati kwenye mabano ni Rusumo (80) na Kinyerezi 1 (185) yameipa nguvu serikali ambayo kupitia wakala wa kusambaza umeme vijijini (REA), mwisho wa mwaka 2024 imesambaza umeme kwenye vijiji zaidi ya 12,000.
Vilevile, kufika mwisho wa 2024 vitongoji zaidi ya 32,000 vimefikishiwa umeme kati ya vitongoji 64,359. Kwa takwimu hizi tunajivunia uwepo wa JNHPP kama kiini cha kuchochea maendeleo nchini pamoja na mataifa mengine yatakayonunua nishati hiyo.
Kuwepo bwawa la JNHPP ni suala moja lakini kuwepo matumizi endelevu bila kuathirika mifumo ufuaji umeme ni jambo jingine.
UHAI JNHPP
Hoja ya msingi ni kuhusu bwawa JNHPP kubaki katika uzima na kuzalisha umeme kwa miaka mingi ijayo.
Maji ya mto Rufiji yanatokana na vyanzo vya mito na vijito kutoka mikoa mingine nje ya mkoa wa Pwani bwawa lilipo yanahitaji kulindwa.
Mto huo ni muunganiko wa maji ya mito Ruaha Mkuu, Kilombero na Kihansi na kwamba Ruaha Mkuu vyanzo vyake vikuu ni vijito mbalimbali katika mikoa ya Iringa na Mbeya ikiwemo pia Mto Ruaha Mdogo wenye vyanzo vyake katika wilaya ya Mufindi hapa kuna eneo muhimu la shamba la miti la Saohill.
Mito Kilombero na Kihansi hupata maji kutoka sehemu mbalimbali mkoani Morogoro.
Ukifuatilia mito na vijito hutoka mlimani, kuelekea ziliko shughuli za binadamu; unakuta maji yamesheni taka, udongo, tope, mchanga na takangumu.
Mito mingi nchini vyanzo vyake ni kwenye maeneo kadhaa yenye shughuli kemkemu za mfano, Ruaha Mkuu unatokea juu milimani na kuteremkia wilayani Mbarali kuelekea kwenye ukanda wa wakulima ya mpunga ikiwamo mashirika makubwa na wakulima wadogo ambao tegemeo kubwa ni maji ya Ruaha Mkuu.
Mto unapoelekea Hifadhi ya Taifa Ruaha, unapita eneo oevu la Ihefu ambayo ni sehemu ya kuhifadhi maji yanayoendelea kutiririka Ruaha Mkuu.
Eneo hilo muhimu mara kwa mara hughubikwa na changamoto za kuingiza makundi makubwa ya mifugo nyakati za ukame na kusababisha madhara makubwa kwenye ikolojia na uoto asili unaofanya maji yatuame au kuhifadhiwa muda mrefu.
Matokeo hasi husababisha maji kwenye Ruaha Mkuu kuwa hafifu na kupelekea mahangaiko makubwa kwa wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Ruaha pia kuathiri kufua umeme kwa kiasi kikubwa.
KULINDA JNHPP
Kama kweli tumedhamiria kuhakikisha JNHPP inastawi kwa miaka mingi, na kutokana na ukweli kuwa mito inayopeleka maji hadi mto Rufiji, imo kwenye sehemu zenye shughuli nyingi za binadamu zisizoendelevu hasa kilimo na ufugaji ni dhahiri hatua kali lazima zichukuliwe kuhakikisha maji yanaendelea kutiririka katika mito hiyo.
Ni lazima yalindwe yawe safi kwa kuzingatia yafuatayo : Mosi ni usimamizi, utekelezaji endelevu wa sera, sheria na kanuni za kulinda na kutunza mazingira zikiwemo sheria za mazingira, misitu na nyuki na nyingine za kisekta na kuimarishwa kwa ngazi zote za uongozi,utawala nchini.
Uzoefu unaonyesha kuwa sera, sheria, kanuni na miongozo vipo isipokuwa utekelezaji ni changamoto ainayake.
Tunahitaji nidhamu na kudhamiria na usimamizi makini kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa mifumo ikolojia ya kuchuja maji ya mvua yaweze kuingia kwenye mito ili udongo na tope pamoja na taka nyinginezo vibaki juu ya ardhi.
Pili, kulima, makazi na mifugo kandokando ya mito na vijito tangu mwanzo hadi mwisho baharini au kwenye maziwa na mabwawa, zidhibitiwe bila kuoneana haya ili kulinda mifumo ikolojia.
Kifungu 57 (1) cha sheria ya usimamizi wa mazingira (2004), kinazuia shughuli za binadamu ambazo kwa asili yake, zinahatarisha sana ‘uhai’ wa eneo la hifadhi ya mita 60 linalotakiwa kulinda mazingira yasiharibike husasani ni ardhioevu ikiwamo bahari, mito, mabwawa na maziwa;
La tatu tuhakikishe wakati wote ukanda wa mita zilizoainishwa kwenye mwongozo uliotolewa Disemba mosi, 2020 na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, unatekelezwa ipasavyo.
Kupitia waraka huo shughuli za kibinadamu zisizotakiwa kufanyika ili kulinda mifumo ikolojia kwa nia njema ya kuiweka salama na kuhakikisha mito muhimu inayoingiza maji JNHPP na mabwawa mengine, inatunzwa kwa manufaa ya wengi.
Lengo kuu likiwa ni kuhakikisha mito inatiririsha maji safi badala la kusheheni taka na tope na kusababisha vina vya mabwawa kupungua hivyo na kuathiri ufuaji umeme.
Matokeo chanya ya kuhifadhi na kulinda mifumo ikolojia ni pamoja na ukanda wa mita 60 kutoka mtoni au ziwani kuachwa na kuhakikishiwa kuwa unafunikwa na uotoasilia unaotosheleza.
Misitu, nyasi na mimea mbalimbali na kina cha maji JNHPP kitaweza kubaki kilivyo 2025 mpaka miaka mingi ijayo iwapo:
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi, pia kwa kutambua kuwa shughuli za kibinadamu zinazosababisha uharibifu kwenye mifumo ikolojia zinadhibitiwa kwa kusimamia sheria na kanuni ikiwemo kuwajibika ipasavyo.
Vilevile, mwongozo uliotolewa 2020 unafafanuliwa na kueleweka kwa wadau wote, ikiwemo jamii zilizopo karibu na mito, mabwawa na maziwa ili kutimiza wajibu kwa kuzingatia matakwa kisheria.
Jingine ni kuondokana na mawazo na mitazamo kama vile kuwalinda na kuwatetea wanaokiuka sheria, kanuni na miongozo rasmi kwa kutanguliza maslahi binafsi wakati athari za vitendo vyao ni hatarishi kwa uchumi.
Kuhifadhi kingo za mito na mabwawa ni muhimu sana ili mifumo ikilojia ndani ya mita 60 inabaki ilivyo na salama wakati wote. Kwa kufanya hivyo, kutalihakikishia taifa kwanza, kupata maji-safi yatakayosambazwa na Mamlaka za Maji Mijini na Vijini kwa gharama nafuu bila kutumia fedha nyingi kuyasafisha kabla ya kuyasambaza pili, ‘uhai’ wa mabwawa ya kufua umeme utadumu miaka mingi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED