Bibi miaka 80, wajane, hadi vijana waishi kwa kugonga mawe kokoto

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 08:54 AM Jan 10 2025
Mariamu Shija (80), bibi anayetegemea ujira wake kwa kugonga mawe ya kokoto, mwenye miakia 30 kazini.
Picha: Pilly Kigome
Mariamu Shija (80), bibi anayetegemea ujira wake kwa kugonga mawe ya kokoto, mwenye miakia 30 kazini.

KAZI inatajwa kuwa jibu kuu la hatima au kipato cha watu. Hapo ndipo katika dodoso wanapatikana kinamama wanaojishughulisha na ugongaji mawe makubwa.

Ujira wao ni shilingi 250 kwa ndoo, eneo la Kunduchi Mtongani, mkoani Dar es Salaaam wanakiri ni ‘kazi ngumu’, kukiwapo kundi la wenye umri mkubwa, shida na majukumu kifamilia, zimewaelemea. 

Yupo Mariamu Shija (80), bibi anayetegemea ujira huo kugonga mawe ajilishe yeye na mume wake, asiyeweza kufanya chochote kutokana na umri mkubwa. 

Anatamka kishatumikia kazi hiyo ya ugongaji kokoto kwa zaidi ya miaka 30, wakiwajibika bila kinga ya misimu yote; juani na kwenye mvua. 

“Mjukuu wangu, mimi Mungu hajanijalia uzazi, sijazaa! Sina mtoto hata wa dawa wa kusema labda angenihurumia, nisifanye kazi hii ngumu nateseka sana.

 “Lakini, nashukuru nanunua unga na mchicha nakula japo nguvu zimeshaniishia,” anasimulia katika eneo la Kunduchi, Mtongani, Dar es Salaam.

 Bibi Mariam, anasimulia alikuja jijini Dar es Salaam kutafuta maisha akitoka kwao mkoani Tabora, baada ya kuachika na mume wake wa kwanza, anayedai kisa ni baada ya kukosa uzazi wakiwa kwenye ndoa muda mrefu.

 Hapo analalamika mateso, dharau na kebehi kutoka familia yake yakachukua nafasi, akisema ndiyo ikawa ‘kisa na mkasa’ kuachika.

 Anataja ilikuwa zama za miaka ya 1970, ndipo akaamua kuingia katika tafsiri mpya ya maisha, kusaka mwelekeo ndani ya Dar es Salaam. Hata hivyo, hakumbuki mwaka mahsusi aliyoiacha Tabora, hadi kufika jijini.

 Pia, akadokeza kaka yake aliyeenda Tabora akamshawishi wafunge wote safari kujaribu Maisha, Dar es Salaam, akaridhia.

 MAISHA MAPYA

Anasimulia alifikia eneo la Tegeta kwa Masista kwa kaka yake, akaanza kujishughulisha na biashara ndogo kipindi hicho na kubahatika kuhifadhi fedha, akaweza kununua eneo la kipimo cha ‘mti wa mkorosho’ kwa shilingi 100, akajenga nyumba ya udongo, akaweza kuishi eneo hilo.

 Miaka mingi baadaye, anasema akatokea mnunuzi kutaka eneo hilo, naye akapauza na hata kumuwezesha kujenga nyumba ya tofali na pakampatia makazi bora ya kudumu.

 Anasema, miaka ya baadaye akaona ajiunge na shughuli ya ugongaji mawe kwa kushauriwa na mmoja wa jirani zake ili aweze kupata fedha ya kujikimu kimaisha.

 Hata hivyo, anakiri amechoka sana kiafya, lakini hana mbadala wa kumpatia chakula kumsitiri, huku mume wake hajimudu kimaisha ‘hata kiduchu’.

 “Kwa sasa naweza kugonga ndoo nne tu napata shilingi 1000 kwa siku, narudi nyumbani,” anasimulia.

 WAGONGAJI WENGINE

 Pia, mahali hapo pana mgonga mawe Batuli Masayanyika (60), mjane ambaye ni mkongwe katika shughuli hiyo, kwa miaka 20 sasa.

 Amekutana na Nipashe hivi karibuni, naye akarudisha kumbukumbu zake mwaka 1994, alipoanza shughuli hizo eneo la Kunduchi Mtongani.

 Mwasiti anasimulia kwamba wakati anaanza shughuli hiyo, alikuwa na mume ambaye kipato chake kilikuwa hakitoshelezi kuleta ustawi katika familia, ndipo alipoamua kujiunga na wanawake wengine kituoni hapo.

 Mwasiti anasema, maisha yakasonga na miaka mingi baadaye, mume wake akafariki umri ukiwa umeshasonga na ili kuweza kujikimu kula na watoto, pia wajukuu na ndugu wa karibu wanaomtegemea, akajikita katika kazi hiyo

 Anaielezea Nipashe kuwa, sasa anategemewa na watu zaidi ya wanne ambao wote wanamuangalia yeye kwa kipato hicho kisichozidi shilingi 3000 kwa siku.

 Katika orodha hiyo, anawataja watoto wawili, pia wajukuu wawili, huku kukiwapo mtoto wa kaka yake alitokea mkoani Tanga na kuja nyumbani kwake, baada ya kushindwa maisha kijijini.

 Anasimulia kipindi anaanza kazi hiyo mwaka 1994, walikuwa wanalipwa ujira wa shilingi 150 kwa ndoo, yenye vipande vya kokoto zitokanazo na jiwe lililogongwa.

 Mwasiti anataja kiwango anacholipwa sasa kwa kila ndoo ni shilingi 250 na kwa siku huwa anamudu ndoo 10 ikimapatia shilingi 2,500.

 Naye kama alivyonena mtangulizi wake Bibi Mariamu, Mwasiti analalamika ameshachoshwa na kazi hiyo, ila anashindwa kuacha kwa sababu ndio nguzo ya kipato chake na familia.

 “Sina jinsi mwanangu, sina wa kunisaidia, kwani nikiacha hapa, wajukuu zangu watakufa njaa na wanaonitegemea hivyo nitafia kwenye hii kazi,” anasema

 Mwasiti anaeleza manufaa pekee anayoiona katika kazi hiyo ni ujira unaomlisha, tena akinena chakula cha gharama nafuu anachokitaja “kununua mboga za majani na unga hakuna faida nyingine!”

 Anaendelea: “Mwanangu wa kiume kaachana na mkewe, watoto wake wawili kaniletea mimi. Nina mtoto wa kaka yangu wa kiume katokea Tanga... nae yupo siwezi kumfukuza kaka amefariki

 “Sisi tunakula, yeye anatuangalia haitawezekana na hata ukiweka ugali...mtoto wangu wa kike naye sio wa kumtegemea sana kwani na yeye hana mume na hana kazi.”

 Sasa anawaomba wamiliki wa mradi wanaotumukia, kuwaongezea ujira kutoka shilingi 250 za sasa, akisema awali alikuwa anagonga hadi ndoo 15 kwa siku. Lakini, akakwama kutokana na umri kumuacha.

 Sharifa Bakari (55), anataja kuanza kazi hiyo mwaka 2014, akidumu na miaka 10 ya kupambania kula yake mahali hapo, kupitia ugongaji mawe ya kokoto.

 Anaiambia Nipashe kuwa kazi hiyo ni ngumu, naye hana jinsi kutokana hali mapungufu ya kifedha na uhalisia wa udhaifu aliyo nayo.

 “Mume ninaye, baba wa watoto wangu niliyezaa nae watoto watano, ila kwa sasa ni mtu mzima sana na mbaya zaidi hafanyi kazi yoyote ni mlemavu wa macho kwa hiyo hawezi kufanya kazi yoyote, ninalazimika kufanya kazi hii ili tule,” anasema Sharifa.

 Anasema, ana mnyororo wa watu watano wanaomtegemea akiwamo mume, pia mdogo wake wa kike, binti na mjukuuu mmoja, wote wanamtegemea yeye.

 Nipashe ilipotaka kujua kulikoni hali hiyo kutegemwewa na kundi, akafafanua mbali na mume mlemavu, mdogo wake ni mlemavu asiyetembea na binti yake bado hajapata kibarua anachokitaja ‘cha kueleweka.’

 Anafafanua kuwa bintiye ‘anahangaika Kariakoo’ kusaidia Mamalishe kwa ujira duni, unaoishia kwenye usafiri, kutokana na umbali mrefu kutoka makazi yao.

 Pia, ananena kuwa binti huyo kazalishwa na mwanaume aliyekataa mtoto huyo, akiitaja ni hali inayowaongezea uzito wa kimaisha.

 Anasema mumewe awali alikuwa na shughuli zake za ulinzi, pia kiongozi wa kisiasa Kunduchi, lakini baadaye akapata ugonjwa na macho yakafa, huku umri umeshakuwa mkubwa.

 “Sasa hapo ndipo nilipovurugwa zaidi, kwa kuwa awali tulikuwa tunasaidiana, lakini sasa hata yeye ananiangalia mimi, iwe jua iwe mvua, ni lazima nije nigonge kokoto, ili mradi tununue kilo ya unga na mchicha tule” anasema

 Kamera ya Nipashe, katika dodoso hiyo, ihakahamia kwa Mariam Julius (36), anayejitambulisha yu mama wa watoto watatu, mumewe amefariki.

 Anaitaja kuwa mazingira yaliyomfanya kujiunga na kazi hiyo kujikimu na wanawe, akisema “wanakula” pia, “wanaenda shule na matumizi madogo madogo ya kila siku anayapata kutokana na kazi hiyo.”

 Mgonga kokoto huyo mama kijana, anasimulia safari yake yua kijiunga na kundi hilo, ilianza baada ya kujikuta anasumbuliwa na maendeleo ya biashara yake, hasa kimasoko.

 Anaeleza mitaji yake ‘ilikatika’ kila mara, huku wa kumasaidia amefariki, akaona aingie mbadala wa vibarua vya kuchekecha kokoto (kuzitofauatisha na udongo), akijaza ndoo moja analipwa ujira wa shilingi 200.

 “Kutokana na kazi hiyo kwa siku nina uwezo wa kuchekecha ndoo 40 hadi 30 najipatia hela (Sh. 6,000 hadi Sh. 8,000) ya kwenda kula na wanangu,” anasema Mariam.

 Anataja changamoto kubwa anayokutana nayo kazini ni kipindi cha mvua kazi haifanyiki, kwa kuwa eneo hilo lote kunakuwapo tope na kokoto hata kukwamkisha uchekechaji mchanga kuwa mgumu. 

WADAU WAINGILIA 

Baada ya kubaini madhila wanayopata kinamama hao, taasisi isiyo ya kiserikali ya HIMA, ililiona kundi hilo la wanawake wagonga kokoto wa Kata ya Mtongani mkoani Dar es Salaam, wakawapa elimu ya ukatili wanawake hao wapatao 50.  

Kaimu Mkurugenzi ambaye ni Ofisa Miradi, Hilda Msangi, anasema wakaona wawafikie wanawake hao kuwapatia elimu hiyo, waweze kujitambua wanapokuwa katika shughuli zao hizo 

Hilda anasema, hiyo ni kutokana na ongezeko la vitendo vya ukatili majumbani, makazini na maeneo ya utafutaji riziki wa kila siku. 

“Tumeona kundi hili kama limesahaulika, mashirika mengi hawawafikii, sisi tumeona tuwe mfano kulifikia kundi hili na mwandishi umeona ni jinsi gani wanawake hawa hawana uelewa mkubwa kuhusiana na ukatili,” anafafanua Hilda. 

Soviana Martin (30), mgonga kokoto katika eneo la Mbuyuni, anasema wanakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwamo kukosa vifaa kazi kama vile 

barakoa, mabuti, glovu, miamvuli ya kujikinga na jua na ukosefu wa vyoo Jirani yanayayowazunguka. 

Nipashe ilipomfuata Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mtongani Stanslaus Thomas, kufafanua baadhi ya changamoto zinazomhusu, akakiri madai lao ya wagonga kokoto, ikiwamo kuwa katika wakati mgumu kwa hitaji kama vyoo. 

Akataja changamoto hiyo ni kubwa na yeye hana ufumbuzi wa moja kwa moja, kulingana na ngazi yake ya utendaji kikazi, ikizingatiwa shughuli hizo zinaendeshwa kando ya hifadhi ya barabara.