NI muda mrefu kumekuwapo kilio kinachoendana na walakini katika hali ya kinamama na mchakato mzima wa uzazi, hadi kupatikana mtoto.
Sura kuu ilijificha katika elimu au uelewa duni kuhusu suala hilo, kukosekana mahitaji muhimu katika nyumba za tiba, ngazi ya ujuzi na ushirikiano kijamii.
Kuna wakati katika Serikali ya Awamu ya Nne, kulikuwapo taasisi isiyo ya kiserikali chini ya Mama Salma Kikwete, ikajivisha sehemu ya wajibu huo, ikisambaza vitanda vya kusaidia huduma za uzazi.
Pia, ni katika awamu hiyo mapema, zikabuniwa mambo makuu mawili; Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) na sera yake mwaka 2007, ambazo maudhui yake yamekuwa na maana kubwa katika afya ya mama na mtoto hadi leo.
Mfumo wa kiserikali nchini, ikiwa na itifaiki ya kupokezana kijiti katika utendaji, ilipoingia madarakani Serikali ya Awamu ya Sita, nayo ikajikita kwa itifaki kuu mbili.
Mosi, kuendeleza ya MMAM na sera iliyoyakuta, pia kufanya ubunifu wake. Hapo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akawa na lake maalumu akiweka itikadi yake ya ‘Mama Kashika Usukani’ akizamia mapya yanayokomboa afua ya mwanamke kwa upekee.
Hapo akaanza na hatua kwamba, katika zaidi ya miaka mitatu ya uongozi wake, akaogeza bajeti maradufu, kwa sekta afya, mwanamama anufaike kwa kiasi kikubwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, akidokeza Septemba mwaka huu kuwapo jumla ya hospitali za wilaya 129 zimejengwa nchini kote.
Takwimu za afya kitaifa, sasa zinaonyesha uwekezaji wa miundombinu ya afya; vituo vya huduma za afya kuongezeka kutoka 8,549 alipokuwa anaingia madarakani mwaka 2021 hadi 9,610 Machi mwaka jana; sawa na ongezeko la vituo 1,061.
Hapo ikivaliwa miwani, anaonekana mhitaji mwanamama, anapewa unafuu wa aiona yake.
MANUFAA YAKE
Hatua za manufaa yake inatajwa kwa mfano na Wizara ya Afya, Machi mwaka jana, kwamba kuna ongezeko la wajawazito waliojifungua kwenye vituo vya huduma za afya kutoka asilimia 63 mwaka 2021 hadi asilimia 85 mwaka mwaka 2023.
‘Lengo la nchi ni kufikia asilimia 95 ya wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ifikapo mwaka 2030,” anatamka wizara hiyo katika taarifa yake.
Pia, taarifa hiyo inadokeza kupunguzwa vifo vya wajawazito kwa asilimia 80, huku kukiimarshwa huduma za uzazi, mama na mtoto.
Mavuno yake hadi sasa ni kupunguzwa vifo vya wajawazito vitokanavyo na uzazi kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104.
Pia, inatajwa mageuzi hayo ya Rais Dk. Samia, ni kwamba vifo vya watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja, vimepungua kutoka 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi 33 mwaka jana.
“Vifo vya watoto wachanga (wenye umri wa chini ya siku 28) vimepungua kutoka 25 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi vifo 24 kwa vizazi hai 1,000 hadi sasa, “ inaeleza taarifa hiyo ya Wizara ya Afya.
Eneo lingine la ufafanuzi wa wizara, ni kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano vifo vyao vimepungua kutoka 67 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 na kufika 43 mwaka 2022.
Hapo ndipo inapozaliwa swali la msingi, kuna hatua na mikakati ipi inayofanyika kufikisha mahali hapo?
UMIRAISHAJI HUDUMA
Wizara ya Afya katika taarifa yake in ufafanuzi kwamba, kati ya mwaka 2021 hadi Machi jana, Serikali ya Awamu ya Sita ikaendelea kuwekeza katika huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, katika maendeleo kadhaa;
Hapo kuna rekodi ya kukamilishwa ujenzi wa jengo kongwe la huduma za afya ya mama na mtoto, katika hospitali kongwe ya Meta, jijini Mbeya ikigharimu shilingi bilioni 13.2.
Pia, kuna uendelezaji wa majengo ya Mama na Mtoto, kwenye hospitali za rufani za mikoa ambazo ni; Sekou oure (Mwanza), Geita, Simiyu, Mawenzi, Njombe na Songwe ambazo zimegharimu jumla ya shilingi bilioni 71.1.
Kuna kuimarishwa huduma za upasuaji wa wajawazito kwa kuongeza, vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji wa dharura wa kwa mjamzito (CEMoNC) kutoka vituo 340 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 523 mwaka 2023. Ni ziada ya 183.
Kuanzisha wodi maalum kwa ajili ya huduma za watoto wachanga wagonjwa (Neonatal Care Units - NCU); hadi kufikia Desemba 2023, kuna jumla ya hospitali 189 zinatoa huduma za NCU ikilinganishwa na hyospitali 165 mwaka 2022 na Hospitali 14 tu mwaka 2018.
Kumekuwapo uimarishaji, upatikanaji wa bidhaa za afya na uzazi, mama na mtoto, katika vituo vinavyomilikiwa na serikali, ukiongezeka kutoka asilimia 82.5 mwaka 2021 hadi asilimia 88.2 Za mwaka 2023.
Kuimarishwa huduma za Saratani ya Mlango wa Kizazi; kukiwapo jumla ya mashine 140 za uchunguzi wa saratani zimenunuliwa na kusambazwa kwenye vituo 140 vya kutoa huduma za afya katika halmashauri 104, katika mikoa 26. Vifaa vyote vina thamani ya shilingi bilioni 1.1.
Mfumo wa M-mama; Serikali ya Rais Dk. Samia, imeanzisha mfumo wa kieletroniki unaoratibu rufani, kwa kusafirisha wajawazito na watoto wachanga wanaohitaji huduma za dharura.
Hiyo ni safari kutoka ngazi ya jamii hadi vituo vya kutoa huduma za afya au kutoka kituo cha ngazi ya chini, kwenda ngazi ya juu.
Kati ya mwaka 2022 hadi 2023, mfumo huo umeendelea kufanya kazi katika mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar, kukiwapo wahusika 46,941 wamenufaika na huduma za dharura za rufani.
Wizara ya Afya kupitia ripoti yake mwaka jana, inatamka uwekezaji uliofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hasssan, katika kuimarisha ubora wa huduma za afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, viashiria vya nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ikang’ara kufanya vizuri kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED