Acheni matumizi holela ya dawa mnayaweka maisha yenu rehani

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 05:49 PM Aug 15 2024
Mteja wa akihudumiwa kwenye duka la dawa.
PICHA: BEATRICE MOSES
Mteja wa akihudumiwa kwenye duka la dawa.

NI mazoea kununua dawa kiholela kuanzia ‘flajili’ unaposikia tumbo linauma au kuhara na ‘antibayotiki’ kubwa kama ‘amoksilini na azuma’ hata bila kumwona daktari.

Mtindo uliozoeleka, ni kwenda kwenye duka la dawa, kununua au kueleza shida yako. Na bila kujali, mwingine humeza vidonge vichache na baadhi hutumia nusu dozi na kuachana na  dawa baada ya kupona. 

Wataalamu wa afya wanathibitisha kwamba, mazoea ya kumeza dawa pasipo maelekezo wala vipimo sahihi, ni kujimaliza, wapo watu kadhaa imewagharimu maisha baada ya kuwasababishia maradhi ya ini na figo.  

Hapa wataalamu hao wanaonya kuwa, kununua dawa na kujitibu kiholela ni hatari, kwa kuwa  dawa za tiba sio sawa na bidhaa nyingine, umewekwa utaratibu maalum wa kufuatwa, ili kusimamia matumizi sahihi na kudhibiti hatari na athari za kiafya zinazoweza kujitokeza. 

Baraza la Famasi lililopo chini ya Wizara ya Afya, kupitia kipeperushi chake linaelimisha matumizi sahihi ya dawa kuwa ni sumu na huleta madhara iwapo hazitatumiwa ipasavyo.

Linasema ni muhimu mgonjwa kufanyiwa uchunguzi na kupata ushauri wa mtaalam wa afya kabla ya kutumia dawa. 

         MAANA YA DAWA

Ni  kemikali au kitu chochote kinachotumika kutibu au kuzuia ama kutambua magonjwa ya binadamu au wanyama. Zinaweza kuwa vidonge, za maji na mafuta, gesi, hewa ya kuvuta na mionzi. 

Baraza linasema zinaweza kutumiwa kwa njia mbalimbali kama kumeza vidonge, kunywa  dawa za maji, kupaka, kuchoma sindano na kuvuta kwa njia ya hewa.  

Matumizi sahihi ya dawa, kwa mujibu wa Baraza la Wafamasia, yanahusisha mgonjwa kufanyiwa uchunguzi wa kina, kuandikiwa na kupewa dawa anayostahili kulingana na hali ya ugonjwa wake.

Anaelekezwa  kutumia dawa kwa kipimo, njia na muda sahihi kulingana na maelekezo aliyopewa na mtaalam wa afya. 

Pia matumizi sahihi ya dawa yanazingatia uhifadhi wa dawa katika kipindi chote cha matibabu anayopokea. 

Kwa mujibu wa baraza hilo, ni kujinunulia na kutumia dawa pasipo maelekezo ya mtalaam wa afya, kutokumaliza dozi au dozi kamili na kuchangia dawa na mtu mwingine.  

ATHARI  ZAKE 

Madhara ya matumizi yasiyo sahihi ya dawa, ni pamoja na kuongezeka ugonjwa, kutopata nafuu, kutopona hatimaye kufa.   

Mengine yanatajwa kuwa ni pamoja na  kuongezeka kwa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa na kusababisha maradhi ya figo na ini kuwa na jamii isiyo na imani na mfumo wa kutoa huduma za afya.   

Baraza la Famasi linatahadharisha watu kuepuka kununua dawa kwenye maduka yasiyosajiliwa kisheria, kwa kuwa ubora wake ni wa mashaka, pia maelezo ya matumizi yanaweza kutolewa bila usahihi au na mtu asiye sahihi, kitendo kinachoweza kusababisha madhara kwa mtumiaji. 

Matumizi sahihi ya dawa, yanapunguza usugu wa vimelea vya ugonjwa na kiasi cha madhara na maudhi ya dawa inayotumika. Kwa upande mwingine huipunguzia serikali au gonjwa gharama za matibabu.  

 Hupunguza uwezekano wa kupata magonjwa yanayoweza kusababishwa na matumizi holela ya dawa, huboresha afya ya mgonjwa kwa kupona kwa wakati na kujenga imani kwenye  mfumo wa kutoa huduma wa afya na wataalamu wake, linasema Baraza la Famasi. 

Ikumbukwe, awali  huduma za dawa katika maduka ya dawa muhimu  ilitolewa kwa mujibu wa Sheria ya Dawa na Sumu ya mwaka 1978, ambayo baada ya utafiti ilifutwa.  

Wakati huu huduma inatolewa kwa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003. Maduka ya dawa muhimu yaliyoanzishwa na kusajiliwa na mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), ndio yaliyoruhusiwa kutunza na kuuza dawa, kabla ya mabadiliko kufanywa. 

Baada ya  kutungwa kwa Sheria ya Famasi  ya mwaka 2011,  TFDA inabaki na mamlaka ya kusimamia na kudhiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa. 

Mkuu wa Kitengo cha Sheria Baraza la Famasi Paulo Makanja, anasema, kwa mujibu wa Sheria ya Famasi, baraza hilo ndilo lenye wajibu wa usimamizi na udhibiti wa maduka ya dawa muhimu.  

Anabainisha kuwa vifungu vya 45 na 48 vinatoa wigo wa utendaji kazi, kulingana na vigezo na inaeleza adhabu zinazotolewa iwapo  mtoa huduma za dawa atakwenda kinyume.

 “Kwenye duka la dawa inapaswa kuwekwa cheti cha muuzaji ili iwe rahisi kutambua kiwango chake cha elimu na dawa anazouza. Hii ni muhimu ndio maana wakaguzi hukagua ili kujiridhisha,” anasema Makanja.   

 Anasema, muuza dawa au mgawaji anapaswa kuwa na mafunzo ambayo yanatambulika, hivyo kwenye kila duka la dawa muhimu na famasi kunapaswa kubandikwa vyeti vya muuzaji ili kuonyesha uhalali wa uuzaji au utoaji wa dawa hizo katika utaratibu uliowekwa.  

Mfamasia Irene Massawe kwenye duka la dawa Nakiete liliko Dar es Salaam, anasema wamekuwa wakipata changamoto kubwa kutoka kwa wateja wanaofika na kutaka kuuziwa dawa bila kuwa na cheti chenye maelekezo ya dawa wanazohitaji.

 “Anafika dukani anakwambia nipe dawa ya malaria maana ninavyojisikia hii ni malaria tu, naujua mwili wangu hata unapomwambia kuwa anapaswa kupimwa  ili kuwa na uhakika haelewi inawezekana akapewa dawa hizo, kisha kusisitizwa kuwa dalili zikiendelea aende hospitali,” anasema.  

Irene anaongeza kuwa kuna baadhi ya dawa za maumiivu, ambazo wanaruhusiwa kuuza bila cheti, lakini za magonjwa kama presha au  kisukari, ambayo ni endelevu kwa mgonjwa huuzwa kwa tu kwa vyeti au maelekezo ya daktari.

 Mratibu wa Kanda ya Mashariki wa Baraza la Famasi Arapha Nshau, anasema wafamasia watalam waliosajiliwa  ni 3,789 na kwamba ni wale wenye elimu ya kiwango cha kuanzia shahada ya famasi. 

Wengine ni  fundi dawa sanifu wako 8,466 (stashahada ya famasia) pia kuna fundi dawa wasaidizi 1,042  wenye  elimu ya awali ya famasi.  

Nshau anasema, maduka makubwa ya dawa  yanayoruhusiwa kuuza dawa na vifaa tiba mbalimbali yaliyosajiliwa ni 3,187, maduka ya dawa muhimu ni 22,536 ambayo kuna baadhi ya dawa hayaruhusiwi kuziuza. 

 “Maduka haya ya dawa muhimu hupaswa kusajiliwa pembezoni mwa maeneo ambayo hakuna zahanati au kituo cha afya, lengo likiwa likiwa ni kurahisisha kupatikana kwa dawa muhimu za matibabu. Wanaruhusiwa kuuza aina 37 tu za dawa,” anasema.  

Vilevile, anakumbusha kuwa kuanzishwa kwa maduka haya ni kuimarisha kupatikana huduma bora za afya kwa wananchi, ikizingatiwa kuwa yanapaswa yasimamiwe na kuendeshwa na mtu aliyepata mafunzo ya msingi ya kutoa dawa. 

Anasisitiza kuwa, yanapaswa kuanzishwa vijijini au miji midogo, ambako upatikanaji wa dawa ni tatizo, na kwamba ni sharti yaanzishwe katika umbali usiopungua mita 150 kutoka duka moja hadi jingine.