Wenye ulemavu waomba kutibiwa bure

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:43 PM Dec 15 2024
 Francis Daula, kutoka Chama cha Wasiiona Tanzania (TLB).
Picha: Mpigapicha Wetu
Francis Daula, kutoka Chama cha Wasiiona Tanzania (TLB).

MMOJA wa watu wenye ulemavu Francis Daula, kutoka Chama cha Wasiiona Tanzania (TLB), ameshauri kwamba kufikia mwaka 2050, mtu mwenye ulemavu awe na uhakika wa kupokea matibabu ya bure kwa asilimia 100, hasa kwa magonjwa makubwa.

Ametoa ushauri huo leo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) wa kuhakiki rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Daula amesisitiza umuhimu wa dira hiyo ya maendeleo kuweka kipaumbele kwenye afya ya watu wenye ulemavu, akieleza kwamba ni vyema kuhakikisha kundi hilo wanapata matibabu ya uhakika bila vikwazo kufikia 2050.

"Sasa hivi tunaona madaktari bure, lakini dawa bado ni changamoto katika hospitali za serikali, hasa kwa magonjwa makubwa," amesema Daula, akieleza kuwa gharama za matibabu bado ni mzigo kwa watu wenye ulemavu, jambo ambalo linahitaji suluhisho la kudumu kupitia sera na mikakati madhubuti.

Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo
Wakati huo huo, ameshauri kushushwa kwa bei ya nishati safi na kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata matibabu ya uhakika bila vikwazo kufikia mwaka 2050.

Daula ameeleza kuwa ingawa kuainishwa kwa nishati safi kama sehemu ya masuala ya mazingira ni hatua nzuri, lakini changamoto ya bei bado inakwamisha upatikanaji wake kwa watu wa vijijini na wenye kipato cha chini.

"Kama nishati safi tunataka tuitumie, basi kwenye Dira iwekwe kipengele cha kushusha bei, tuhamasishe matumizi yake, lakini pia bei ishushwe zaidi kwasababu nishati hiyo ipo nchini kwetu," amesema Daula.