WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, amesema Dira ya Maendeleo 2050, imeweka kipaumbele cha katiba imara yenye mwafaka wa kitaifa, demokrasia na mfumo madhubuti wa vyama vya siasa.
Aidha, amesema inataka pato la Mtanzania lifikie Dola za Marekani 4,700 (takribani Sh. milioni 10), kutoka dola 1,210 (Sh. milioni 2.8) la sasa; na la nchi lifikie Dola za Marekani bilioni 700 (Sh. trilioni 1.5).
Aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati wa kikao cha Tume ya Mipango cha maoni ya uhakiki, kilichowakutanisha viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa na kusema kuwa lengo ni kujenga taifa la kidemokrasia na haki sawa kwa wote.
Alisema Dira 2050 imeyaweka mambo hayo kwa kuzingatia maoni ya wananchi hususani ya wawakilishi wa vyama vya siasa, waliyoyatoa Agosti 27, 2024.
“Tunataka Tanzania kuwa taifa la kidemokrasia, likiongozwa na katiba imara, inayoakisi muafaka wa kitaifa, taasisi madhubuti za umma na mfumo thabiti wa vyama vya siasa,” alisema Prof. Mkumbo.
“Tunachokipendekeza kwenye dira ni kujenga picha kubwa ya tunataka taifa liweje. Tunataka tujenge taifa ambalo ni jumuishi, lenye ustawi, haki na linalojitegemea.”
Kuhusu pato la nchi, alisema limekua mara nne kutoka Sh. trilioni 32 mwaka 2000 hadi Sh. trilioni 150, mwaka huu na kwamba makadirio ya sasa ya wachumi yanaonesha ukiwekwa msukumo mahsusi kwenye sekta 10, litafikia Sh. Trilioni 1.5 mwaka 2050.
Alisema wachumi wameeleza kuwa ikiwa makadirio yatakuwa ni kukua mara nne kama ilivyokuwa 2000/2025, Pato la Taifa litafikia Dola za Marekani bilioni 400 (karibu Sh. trilioni moja).
Alisema dira mpya inalenga kuondoa umasikini kwa kuhakikisha Tanzania inakuwa mzalishaji mkubwa wa chakula barani Afrika na kuwa miongoni mwa wazalishaji 10 duniani.
Prof. Mkumbo alisema tayari wameshakubaliana ndani ya serikali kwamba mipango yote ya nchi ya muda mfupi, wa kati na mrefu, ijadiliwe na kuidhinishwa na Bunge.
“Kwa kuzingatia hilo, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ameelekeza kwamba dira hii tofauti na dira iliyopita, lazima ikaidhinishwe bungeni. Inamaanisha kwamba itatungiwa sheria kwa hivyo kwa sababu hiyo, kutakuwa na legal protection (ulinzi wa kisheria), kwa maana ya kwamba yeyote atakayekuja huko mbele hawezi akasema atakuwa na dira yake nyingine, itakuwa ni hii hii itabidi aisimamie,” alisema.
Mbali ya hilo, alisema rasimu ya Dira 2050 ina maeneo makubwa matano ambayo ni Msingi Mkuu uliojikita kwenye utawala, amani, usalama na utulivu.
Prof. Mkumbo alisema itasimamiwa na nguzo tatu ambazo ni uchumi imara na jumuishi, uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, uhifadhi wa mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema Dira 2050 imetaja pia miundombinu fungamanishi ambayo itahusisha barabara, reli na usafiri wa majini, sayansi na teknolojia, utafiti na maendeleo, mageuzi ya kidijitali na nishati.
Alisema imeweka sekta 10 za kimageuzi ambazo ni kilimo, huduma za watumiaji, utalii, madini, uzalishaji viwandani, huduma za fedha, ujenzi, uchumi wa buluu, michezo na sanaa za ubunifu, zitakazowekewa mkazo mahsusi.
Alisema huduma za kijamii kama elimu, afya, hifadhi ya jamii, umiliki wa ardhi, maji na ustahamilivu wa mabadiliko ya tabia nchi, nazo zitapewa uzito mkubwa.
“Ardhi yote ya Tanzania kupangwa na kupimwa kwa matumizi mbalimbali. Ardhi kwa ajili ya makazi bora, kilimo, mifugo na uwekezaji,” alifafanua.
Wakitoa maoni, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, alisema rasimu hiyo inahitaji maboresho kwenye muundo wa uchumi kwa kuweka mkakati wa kuongeza thamani mazao ya kilimo na malighafi zote zinazopatikana nchini.
Pia alitaka Watanzania wote wenye umri wa miaka 18 waingizwe kwenye hifadhi ya jamii.
Naye mwakilishi wa TADEA, Ali Makame Issa, alishauri ardhi yote ipangiwe matumizi, ili kulinda inayotengwa kwa shughuli za kilimo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, aliishauri tume isifunge milango ya kupokea maoni yakiwamo ya maandishi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED