Waziri Ummy: Utafiti muhimu kubaini matatizo ya wenye ulemavu

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:48 PM Dec 15 2024
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga, ameshauri kutolewa kipaumbele kwenye maeneo ya utafiti ili kubaini changamoto mbalimbali za watu wenye ulemavu.

Pia ameeleza kuwa rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, imetoa msisitizo wa kuwekeza kwenye tafiti na kutumia matukio ya tafiti katika kuandaa sera na kufanya maamuzi katika sekta na ngazi mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Waziri Ummy ameyaeleza hayo leo mkoani Dar es Salaam wakati akihutubia katika mkutano uliowakutanisha Tume ya Mipango na watu wenye ulemavu, huku akisisitiza kufanyika kwa maabuzi katika kutengeneza sera, sheria na miongozo ambayo itasaidia kupeleka mbele kundi ya wenye ulemavu.

“Maeneo yote muhimu ambayo mmeendelea kutuzingatia, mimi nikiwa mmoja wa walemavu na wenzangu tunaendelea kuwashukuru sana, lakini kama nilivogusia awali leo tumekuja kwa pamoja tusikilize, wenzangu muwe huru katika kutoa maoni ili mambo yetu yaende vizuri,” amesema Ummy.

Washiriki wa mkutano huo
Pia amesema “Tunaona uandishi wa dira hii umezingatia masuala ya watu wenye ulemavu katika kiwango chake. Nakala hii, miaka 25 ijayo, inatupa matumaini kwamba mambo ya watu wenye ulemavu hayatakuwa ya kutafuta tena bali yatakuwa wazi na yaliyowekwa moja kwa moja,” amesema Ummy.

Katika hotuba yake, Naibu Waziri ameishukuru Timu ya Uandaaji wa Dira ya 2050 kwa kuzingatia maoni ya watu wenye ulemavu na kuahidi kuwa kundi hilo litaendelea kushirikiana kikamilifu kuhakikisha dira hiyo inakamilika kwa mafanikio.