Washtakiwa walalamikia barua kutojibiwa

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 05:14 PM Apr 03 2024
Washtakiwa walalamika barua kutojibiwa.
PICHA: MAKTABA
Washtakiwa walalamika barua kutojibiwa.

UPANDE wa utetezi katika kesi inayomkabili Respicius Magesa na wenzake wanaodaiwa kujipatia Sh. milioni 159.5 kutoka akaunti binafsi ya benki ya CRDB ya Dola za Marekani na kuziingiza katika akaunti ya Shule ya Sekondari Maxmillan umedai kuwa umeandika barua mbili lakini haujapata majibu hadi sasa.

Aidha, umedai kuwa barua hizo moja iliandikwa kwenda Ofisi ya Mashitaka ya Taifa na nyingine Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, hivyo wanataka majibu ya barua hizo.

Madai hayo yalitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya wa mahakama hiyo na Wakili wa Serikali Frank Rimoy wakati  kesi hiyo ilipofikishwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upelelezi umekamilika au la.

Wakili Rimoy alidai kuwa bado wanaendelea na upelelezi, hivyo aliiomba mahakama iwapangie tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya Rimoy kudai hivyo, Wakili Joseph Msengesi, anayewatetea washtakiwa hao, alidai kuwa kuna barua waliiandika Februari 12,2024 kwa upande wa mashtaka wakitaka kuondolewa kwa kosa la utakatishaji fedha linalowakabili lakini hadi sasa hawajapata majibu.

"Barua nyingine ililetwa na ilipokelewa mahakamani hapa. Tunaomba  upande wa mashtaka ulete majibu ya barua hizo kwa sababu ukiyapitia mashtaka yote  hayana uwiano na mashtaka waliyoshitakiwa nayo," alidai Msengesi.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Rimoy alidai kuwa hawajapata barua yoyote kutoka upande wa utetezi, hivyo aliwaomba kulifuatilia barua hizo.

Hakimu Lyamuya alisema kutokana na kesi hiyo kushindwa kusikilizwa mara mbili mfululizo kutokana na shida ya mtandao, ndiyo maana wamefikishwa mahakamani, hivyo tarehe itakayopangwa kesi hiyo itasikilizwa kwa njia ya mtandao.

Kesi hiyo iliahirishwa  hadi Aprili 9, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa. Washtakiwa wote wamerudishwa rumande kwa sababu shitaka la utakatishaji fedha halina dhamana kisheria.

Mbali na Magesa, washtakiwa wengine ni Dereva wa CRDB, Michael Owiti, wafanyakazi wa benki, Sia Meta na Ray Nittu, mfanyabiashara Aisha Bagasha, Deogratius Rulangalanga, Andrew Kamugisha na  Ezekiel Salakana.

Katika kesi ya msingi , washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu, kuingilia mfumo wa kompyuta, kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo, kujitambulisha na kutakatisha fedha.

Ilidaiwa kuwa kati ya Julai 20 na  Oktoba 29, 2023 washtakiwa wakiwa maeneo tofauti ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ovu, waliongoza mtandao wa kihalifu kwa kufanya vitendo vya udanganyifu na kujipatia Sh milioni 159.5.

Ilidaiwa kuwa Nittu, akiwa Ofisa Mauzo wa CRDB Tawi la Mwenge, Julai 20, 2023  aliingilia mfumo wa kompyuta na kugushi akionyesha Kepha Mwiti amebadilisha taarifa zake za benki kwenye akaunti yake binafsi ili zifanyiwe kazi wakati akijua taarifa hizo ni za uongo.

Shtaka  la sita la utakatishaji fedha, linawakabili washitakiwa wote wanaodaiwa kuwa Julai 25 na Septemba 29, 2023 wakiwa ndani ya mkoa wa Dar es Salaam walijipatia kiasi hicho cha fedha wakati wakijua ni mazalia ya kosa tangulizi la kugushi nyaraka.