WANANCHI katika Vijiji vya Miyuguyu na Mguda wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, wanatarajiwa kutekelezewa Mradi wa uvunaji Maji ya Mvua na kuyahifadhi kwenye matangi katika Kaya zao msimu wa masika, ili wanawake waondokane na adha ya kufuata maji umbali mrefu kipindi cha kiangazi, pamoja na kutopoteza muda wa kufanya shughuli za kiuchumi.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Jamii Economic and Social Research Foundation (ESRF) Prof. Fortunata Makene, wakati wa uzinduzi wa mradi huo, ambao utatekelezwa ndani ya miaka mitatu (2024 hadi 2027).
Alisema wanatekeleza mradi huo baada ya kufanya utafiti wilayani Kishapu,na kubaini wanawake wengi wilayani humo wamekuwa wakipata shida kipindi cha kiangazi kutafuta maji umbali mrefu, na wengine kutembea kilomita 10 hadi 20 na hivyo kupoteza muda mwingi wa kufanya shughuli za kiuchumi.
“Mradi huu wa uvunaji maji ya mvua kipindi cha msimu wa masika na kuyahifadhi kwenye matangi, lengo ni kupunguza na kugawanya kazi zisizo na malipo kwa wanawake katika kuwawezesha kujikwamua kiuchumi,ili wasipoteze tena muda sababu ya kufuata maji umbali mrefu,” amesema Prof. Makene.
Mkurugenzi wa Shirika la Relief to Development Society (REDESO) Abeid Kasaizi ambao ndiyo watekelezaji wa Teknolojia ya uvunaji Maji ya Mvua, alisema wananchi watawezeshwa kuvuna maji hayo kwa kutumia paa za kwenye nyumba zao, na kisha kuyahifadhi kwenye matangi chini ya ardhi ambayo watawajengea.
Alisema katika Mradi huo watajenga Matangi ya Maji 20 sawa na kuziwezesha Kaya 240 kupata Maji safi na salama kipindi cha Kiangazi, na kubainisha kwamba Mradi kama huo tayari walishawahi kuutekeleza mwaka 2021 katika vijiji vitatu wilayani humo vya Inolelo,Ngofila na Kiloleli.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, alisema mradi huo upo wakati muafaka kutokana na wananchi wengi wa wilaya humo kukabiliwa na shida kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama.
Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Utafiti kutoka Wizara ya Maji, Alex Tarimo, alisema mradi huo ni miongoni mwa mikakati ya wizara, kwa kuhakikisha wananchi wanakuwa na tabia ya kuvuna maji ya mvua,huku akitoa wito kwa wananchi wilayani Kishapu ambao bado wana nyumba za Tembe wabadilike na kujenga za Bati.
Nao baadhi ya wanawake wilayani Kishapu akiwamo Hellena Emmanuel, alisema kutokana na ukosefu wa maji kipindi cha kiangazi hua wanashindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi, sababu ya kupoteza muda mwingi kufuata maji umbali mrefu, ambapo yeye shughuli zake ni ushonaji wa nguo na kuwafanya kudumaa kimaendeleo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED