WAATHIRIKA wa mafuriko yaliyotokea katika msimu wa masika mwaka huu wilayani Rufiji, mkoani Pwani wamekabidhiwa msaada wa mbegu za mahindi na Benki ya CRDB.
Msaada huo ni kilo 7,148.857 za mbegu za kisasa za mahindi zitakazosambazwa kwa wananchi ili wazitumie katika msimu ujao wa kilimo kuhakikisha wanakuwa na chakula cha uhakika. Zina thamani ya Sh. milioni 50.
Akikabidhi msaada huo uliopokewa na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa benki hiyo, Tully Esther Mwambapa, alisema taarifa za athari zilizosababishwa na mafuriko yaliyotokea zimewasikitisha watu wengi ndio maana imekuwa rahisi kwao kutoa msaada huo utakaosaidia kurudisha shughuli za kilimo kwa uhakika.
"Majanga yana athari kubwa zinazorudisha nyuma uchumi wa watu na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Mara zote, hutokea na kutukuta tukiwa hatujajipanga kukabiliana nayo au hatuna uwezo wa kuyazuia yasitokee.
"Hii ndio sababu iliyoishawishi benki yetu pamoja na kampuni zake tanzu kushirikiana bega kwa bega na serikali kukabiliana na majanga pindi tu yanapotokea ili kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika," alisema.
Tully ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation, alisema walipopata maombi ya uhitaji wa mbegu hizo kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mohammed Mchengerwa, na Mbunge wa Rufiji, kwa ajili ya waathirika wa mafuriko, hawakufikiria mara mbili kwa kuwa waliona ni jambo jema litakalowasaidia waathirika kupunguza athari walizopitia na kurejesha hali zao kiuchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele alishukuru benki hiyo, akisema kitendo ilichokifanya cha kukumbuka na kukimbilia waathirika wa mafuriko yaliyotokea ni cha kizalendo na kinachopaswa kuigwa na wengine.
“Moyo wangu na kichwa changu kama ilivyo kwa wana Rufiji wengi leo, vimejaa shukrani nyingi. Tunawashukuru sana kwa kutukimbilia kipindi hiki kigumu.
"Msaada huu wa mbegu za mahindi mnaotukabidhi leo umekuja kwa wakati mwafaka kwani utatusaidia kujikwamua kutoka katika athari za mafuriko kwa kupunguza gharama za kilimo, hivyo kutuhakikishia mavuno msimu ujao,” alisema Meja Gowele.
Alisema mvua kubwa iliyonyesha mwaka huu imesababisha mafuriko yaliyoharibu mazao yaliyopandwa shambani na hata baadhi ya biashara, hivyo kurudisha wananchi wengi kwenye lindi la umasikini.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED