Shida yaibuliwa ujenzi Daraja la Nyerere

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:26 AM Apr 17 2024
Daraja la Nyerere.
PICHA: NSSF
Daraja la Nyerere.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini malimbikizo ya riba ya Sh. bilioni 103.22 yaliyotokana na kushindwa kulipa madai ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ya ujenzi wa daraja la Nyerere (Kigamboni).

Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2022/23 iliyowasilishwa bungeni, CAG Charles Kichere anabainisha kuwa Novemba 20, 2014, Wizara ya Ujenzi iliingia mkataba na Bodi ya Wadhamini ya Mfuko huo kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa daraja hilo na barabara zake mkoani Dar es Salaam.

Gharama zote za mradi zilikuwa Dola za Marekani milioni 143.50 sawa na Sh. bilioni 238.71 (zilizorekebishwa mwaka 2016 hadi kufikia Sh. bilioni 328.9).

Kwa mujibu wa ibara za 2, 4, na 5 za mkataba, NSSF ilitakiwa kuchangia asilimia 60 ya gharama za mradi huku serikali ikitakiwa kuchangia asilimia 40.

CAG anasema michango kutoka kwa kila upande ilipaswa kutolewa kwa kuzingatia madai ya kazi zilizokamilika, huku riba ikitozwa kwa ucheleweshaji malipo baada ya siku 90 kulingana na kiwango cha riba cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Pia NSSF ilipewa haki za usimamizi wa daraja hilo kwa miaka 30 baada ya ujenzi, ikijumuisha ukusanyaji ushuru wa magari na pikipiki zinazovuka daraja hilo ili kurejesha uwekezaji wake.

CAG anasema kuwa kutokana na upungufu wa fedha serikalini, NSSF ilitoa gharama zote za mradi na serikali ilikubali kurejeshea mfuko huo Sh. bilioni 215.03, ikijumuisha gharama za ulipaji fidia wa eneo la ujenzi Sh. bilioni 14.14; asilimia 40 sawa na Sh. bilioni 124.54 ya mchango wa serikali katika mradi pamoja na riba ya Sh. bilioni 76.34 hadi Juni 30, 2021.

Hata hivyo, anasema hadi kufikia Juni 30, 2023, serikali haikuulipa mfuko huo gharama za mradi wa Sh. bilioni 215.03, hivyo kusababisha riba iliyotokana na ucheleweshaji huo wa malipo kuongezeka kutoka Sh. bilioni 76.34 Juni 30, 2021 hadi Sh. bilioni 103.22 Juni 30, 2023.

CAG anasema aliambiwa sababu kubwa ya kuchelewa kulipa madeni ya mfuko huo ni kutotolewa kwa fedha na Wizara ya Fedha.

“Hivyo, ucheleweshaji huo wa malipo kwa mfuko unaweza kuhatarisha hali ya kifedha ya mfuko na kusababisha ucheleweshaji malipo ya pensheni kwa wastaafu.

"Ucheleweshaji huu wa malipo ya pensheni unaweza kuathiri vibaya ustawi na ubora wa maisha ya wastaafu na wategemezi wao," CAG anahadharisha.

Mdhibiti anapendekeza serikali kuhakikisha malipo ya fidia ya madai ya NSSF kwa mradi wa Daraja la Nyerere yanafanyika ili kulinda utulivu wa mfuko wa pensheni.

MIKOPO CHECHEFU

CAG pia ameonesha hasara inayotarajiwa ya Sh. bilioni 20.43 kwenye mikopo chechefu kutokana na kushindwa kufanya marejesho ya mikopo.

Katika ukaguzi wake kwenye Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), CAG amebaini mfuko ulikuwa na mikopo ambayo ilikuwa haijarejeshwa yenye thamani ya Sh. bilioni 25.42 hadi Juni 30, 2023.

Kati ya mikopo hiyo, mfuko ulitenga kiasi cha hasara tarajiwa kutokana na wakopaji kushindwa kurejesha mikopo jumla ya Sh. bilioni 20.43, ikiashiria matarajio ya kupata hasara ya takribani asilimia 80 ya mikopo iliyotolewa.

CAG anasema mfuko ulitarajia hasara ya asilimia 100 kwenye mikopo ambayo ilikuwa haijarejeshwa kwa muda wa siku 721, ambayo ni jumla ya Sh. bilioni 19.83.  Kwa mikopo iliyobaki ya Sh. milioni 600, mfuko ulitarajia hasara ya kati ya asilimia moja hadi 50.
 Vilevile, CAG anabainisha kuwa kati ya mikopo ambayo haikurejeshwa, Sh. bilioni 1.71 ni mikopo ambayo haikurejeshwa kuanzia mwaka 1995 hadi 1997, ikionesha ucheleweshaji wa kati ya miaka 26 na 28.

Pia inajumuisha mikopo ya jumla ya Sh. milioni 801.38 iliyotolewa kwa benki nne zilizofungwa na BoT kati ya mwaka 2017 na 2018.