RAIS Samia Suluhu Hassan ameonesha kuchoshwa na matamko ya mara kwa mara ya viongozi katika ngazi mbalimbali serikalini, badala yake amewataka kuwa na ubunifu katika kutatua kero na kuwa na majawabu ya changamoto zinazowakabili wananchi.
Rais Samia alisema hayo jana wakati akizindua kampeni ya Tutunzane katika Uwanja wa Sokoine, Mvomero mkoani Morogoro iliyoasisiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Judith Ngulil, ikiwa na kaulimbiu 'Mkulima Mtunze Mfugaji na Mfugaji Mtunze Mkulima Ili Kulinda Mazingira Yetu".
Kampeni hiyo inalenga pamoja na mambo mengine, kuwaelimisha wananchi hususani wafugaji kumiliki ardhi kwa lengo la kupanda malisho na kufuga mifugo michache kwa tija katika ardhi wanayomiliki na kutambua kila mmoja anamtegemea mwenzake kwa kile anachozalisha.
Samia alizitaka mamlaka za mikoa na wilaya kuhakikisha zinawasimamia vyema wenyeviti wa vijiji ili waache kupokea rushwa na kusaidia kuleta suluhu ya migogoro ya ardhi kwenye jamii na viongozi kutumia kampeni mbalimbali za suluhisho la amani badala ya kutoa matamko.
Rais alisema kilio kilichopo ni baadhi ya viongozi kushindwa kusimamia serikali za vijiji badala yake watu wakishaumizana huwa kichocheo rahisi kunyosha mkono kupokea badala ya kuleta suluhu. Aliwataka viongozi kuwasimamia wenyeviti wa vijiji ili walete suluhu za kweli za matatizo ya wananchi kwa kuzingatia sheria.
"Lakini kila mwananchi aheshimu uhuru wa mwenzake kwa kila shughuli anayoifanya ikiwamo kilimo na ufugaji kwani wote mnategemeana katika maisha ya kila siku. Mkulima amheshimu mfugaji na mfugaji amheshimu mkulima. Wote mnazalisha na wote mnahitaji chakula kinachozalishwa," alisema.
Rais pia aliwataka wakuu wa wilaya na mikoa kuwachukulia hatua wale wote watakaoingilia uhuru wa watu kwa manufaa yao binafsi.
"Kama unataka kulisha mifugo, kalishe kwenye malisho siyo kwenye mashamba. Na nyie wakulima muache kukata mifugo ya wenzenu," alisisitiza.
Rais alionesha kuridhishwa na kampeni ya kimkakati ya Tutunzane wilayani Mvomero na kuahidi serikali kusimamia vyema na kuagiza uongozi wa mkoa, wilaya ya Mvomero, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Kilimo kuusimamia vyema mradi huo wa mfano kwa kutenga bajeti na kuwashirikisha wananchi kikamilifu.
Rais Samia alitumia mkutano huo kuwapatanisha wakulima na wafugaji kwa kuwataka wapeane mikono kama ishara ya kumaliza migogoro baina yao.
"Sasa wote mnakwenda kubadilika na kuingia kwenye mradi. Mkabadilike mlime mnaolima na mnaofuga mkafuge. Hakuna haja ya kugombana bali mtumie mradi huu kwani wote mnatupa uhai na mnatupa vitoweo na vyakula," alisema.
Aidha, alisema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakisababisha migogoro mingi ya wakulima na wafugaji hasa wakati wa ukame na kwamba kampeni hiyo inatarajiwa kuwa suluhisho kubwa katika suala hilo.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Nguli, alisema kampeni hiyo ya miaka mitano iliyoanza mwaka 2023, imeshawafikia zaidi ya wakulima na wafugaji 1,200 na kuwezesha uanzishaji wa zaidi ya mashamba ya malisho 40 sambamba yakiwamo ya ufuta.
Nguli alisema kampeni hiyo inakusudia kumaliza migogoro ya ardhi baina ya jamii hizo kwa kuhamasisha upandaji wa malisho ya mifugo, uchimbaji wa visima na malambo kwenye mashamba binafsi ya wafugaji, hamasa ya kilimo biashara na wananchi kuwa rafiki wa mazingira.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema katika kipindi cha miaka mitatu, wamejenga mnada wa kisasa uliogharimu Sh. milioni 500 eneo la Mkongeni wilayani Mvomero na kwa nchi nzima, imejengwa minada ya kisasa 51 iliyogharimu zaidi ya Sh. bilioni 17.5.
Pia alisema serikali imejenga majosho mawili ya mifugo yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 36 wilayani Mvomero wakati nchi nzima majosho 742 yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 17 yamejengwa.
"Tumesambaza dawa za kuogesha mifugo lita 230 za thamani ya Sh. milioni 10.5 kwa Mvomero wakati nchi nzima lita 180,000 zimesambazwa za thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 8.3, sambamba na madume bora ya mifugo 366 ya thamani zaidi ya Sh. milioni 100 nchi nzima," alisema.
Naye Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema wanakusudia kutoa tani 50 kwa wakulima wa Mvomero na kuwataka waliojimilikisha maeneo bila kuyaendeleza kwenye skimu ya umwagiliaji Dakawa (UWAWAKUDA) watakokwa kupisha wananchi wa kawaida wanaotaka kulima.
Akiwa katika kiwanda cha Sukari cha Mtibwa na kuzindua bwawa la umwagiliaji na awamu ya tatu ya upanuzi wa mashamba na umwagiliaji, Rais Samia aliiagiza menejimenti ya kiwanda kuwashirikisha maofisa mazingira ngazi ya taifa katika ujenzi wa kwamba suala la mazingira litiliwe maanani.
Rais aliahidi kuwa serikali itaendelea kulinda makundi yote na inapotokea imeegemea upande mmoja wa wanyonge, upande mwingine usione vibaya kwa kuwa serikali inasimamia na kutetea maslahi ya makundi yote.
Alisema ikitokea sukari imepanda hadi Sh. 7,000 lazima serikali isimame na wananchi kwani ndio walaji na chakula ndio kila kitu. Alipongeza uongozi wa kiwanda cha Mtibwa kwa kutoa zaidi ya ajira 8,000 kwa vijana na ajira 9,000 kwa wakulima wa nje na kwamba upanuzi ukikamilika zitafikia ajira 11,000.
Aidha, Rais Samia alisema serikali katika kuthamini wawekezaji, imeondoa msamaha wa kodi Sh. bilioni 246 kwa viwanda vitano na kwa Mtibwa pekee, msamaha wa kodi ni Sh. bilioni 80.9 umetolewa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, Seif Ally Seif, alisema kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto ya umeme na kwamba kati ya pampu sita za maji katika bwawa hilo, ni mbili tu zinafanya kazi.
Alimwomba Rais Samia kuwaongezea uwezo wa umeme KVA 132 ambapo kwa sasa zipo 33 ambazo zinashindwa kuendesha pambu zote sita.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED